KUWA ORIGINAL


Siku moja mwaka 2016 wakati naanza uandishi nilikaa mezani na kufikiria kitu cha kuandika, ila nikawa nimeshindwa namna ya kuanza kuandika na hata nikawa sielewi nawezaje kuendelea kuandika. Baada ya kukaa kwa muda bila kuona matokeo yoyote yale, niliamua kuingia whatsap na nikawa nasoma makala za hapa na pale.

Hapo ndipo nikakukutana na makala ya Daktari Makirita Amani, baada ya kuisoma na kuipenda, nikaamua kuondoa baadhi ya vipengele na kuifanya ile makala iwe ya kwangu.

Nikabadili kichwa cha habari kidogo, nikaondoa na jina lake mwishoni na kitu chochote kile kilichokuwa kinaonesha kuwa yeye ndiye kaandika ile makala. Nikabandika jina langu, nikaanza kuisambaza hiyo makala kama ya kwangu. Nilikuwa na namba za watu kadha wa kadha, ambao walikuwa whatsap pia. Nikawatumia wote hao ule ujumbe wa ile makala.

Baadhi ya watu wakaniuliza hii makala umeandika wewe, nikawa nimewajibu kuwa kweli nimeandika mimi. Na wengine wakatoa pongezi za hapa na pale ambazo kiuhalisia sikustahili kupokea.

Sasa kwa bahati mbaya, sijui niseme bahati mbaya au nzuri. Ila naona hii ilikuwa ni habati nzuri. Katika kusambaza ile makala nikawa nimeituma na kwa Dkt. Makirita Amani mwenyewe.

Siku hizo, whatsap haikuwa kama ilivyo sasa hivi ambapo unaweza kutuma kitu na kufuta. Kale ka kipengele ka delete for everybody hakakuwepo. Kama ulituma kitu kwa mtu kikaenda ulikuwa hauna namna ya kukifuta kabla hajakiona. Labda ukamwibie simu yake. Hahaha

Baada ya muda kama ilivyotazamiwa ile makala Dr. makirita akawa ameisoma. Baada ya kuituma alinitumia ujumbe ambao nakumbuka ulikuwa unasema hivi,

Godius hii makala mbona kama nimeaiandika mimi..

Ukiendelea na tabia hii, hutajenga hadhira nzuri ya wasomaji. Maana watu watajua kuwa unachukua makala zangu na kuzifanya kuwa za kwako, kwa hiyo hakuna mtu ambaye atajisumbua kusoma maandiko yako. Badala yake atatafuta kusoma maandiko yangu.

Kwa lugha nyingine ni kuwa hakuna mtu ambaye angejisumbua kusoma makala zangu ambazo nimekopi, na kuacha makala original za Dkt. Makirita. Kwa hiyo, nilipaswa kuwa original na kutoa kitu cha kwangu kama cha kwangu na siyo kukopi na kupaste.

Huwa wanasema za mwizi ni arobaini, ila arobaini zangu zilifika siku hiyohiyo bila kuongeza siku ya ziada.

Ilikuwa ni aibu kubwa kwa upande wangu, lakini ilibidi nianze kujikomaza kwa kuanza kuandika kidogo kidogo hata kama ninachokiandika siyo kizuri sana.

Leo hii nafurahi sana kuwa nilikamatika siku hiyohiyo ya kwanza, la sivyo ningeendelea na hiyo tabia ya kuiba makala na kuzifanya kuwa za kwangu, mwisho wa siku ningelemaa na nisingeweza kuandika kitu cha maana.

Kitu cha aina hii nimekuwa nakiona kwa vijana wengine pia ambao huwa wanaiba makala za baadhi ya waandishi huku wakizifanya kuwa za kwao. Ujumbe wangu kwao ni kuwa wanapaswa kuwa original, wakae chini na waanze kuandika, hata kama itakuwa kazi ngumu mwanzoni, ila kwa kujifunza na kufanya mazoezi endelevu, itafikia hatua ambapo watakuwa wanaandika maandiko mazuri na ya kipekee sana. ila wanapaswa kufanya mazoezi endelevu.

Hakuna aliyezaliwa anajua kila kitu

Hakuna aliyezaliwa anajua kila kitu. Ujuzi wowote ule unauona mtu anao, wewe pia unaweza kujifunza huo ujuzi na kuwa nao. Japo tangu zamani nilikuwa napenda kuandika, ila sikuwahi kuandika mpaka pale nilipoanza kujifunza kuandika. Mpaka leo hii naendelea kujifunza zaidi kuhusu uandishi kila kukicha. Kwenye vitabu ambavyo huwa nasoma kila mwezi, walau huwa kinakuwemo kitabu kimoja kuhusu uandishi. Achilia mbali kozi ambazo huwa nafuatilia hapa na pale na mafunzo mengineyo mengi.

Kumbe unavyoona uandishi wangu wa leo, namna ambavyo napangilia mtiririko wa maneno na vitu vingine kama hivyo, siyo kwamba ni kwa bahati mbaya, bali ni mkusanyiko wa vitu ambavyo nimekuwa najifunza kwa siku nyingi, na bado sikomi kujifunza.

Nikisoma kitabu cha mwandishi, sisomi tu ilimradi nimesoma, badala yake nakuwa naangalia ni kitu gani naweza kuondoka nacho kutoka kwenye hicho kitabu, lakini pia nakuwa naangalia mpangilio ambao mwandishi ametumia kwenye kuandika na namna gani ambavyo naweza kuutumia mimi pia kwa namna yangu. siyo kukopi kwake na kupaste.

Makala zangu za kwanza hazikuwa bora sana, ila kwa sababu niliendelea kuandika ndio maana hizi za sasa hivi zinazidi kuwa bora zaidi. na hivyo kuendelea kunipa upekee zaidi.

Kama kitu mtu anaweza kukipata kwa mwingne hakuna haja ya kuja kwako

Kwa kitu chochote kile unachofanya, usiige na kukopi mtu fulani anavyofanya. Badala yake tafuta namna ya kujitofautisha wewe mwenyewe. Kama mtu anaweza kuona igizo fulani kwa mwingine ambaye ni OG, hakuna haja ya kuja kuangalia igizo kwako wewe ambaye unakopi. Kama mtu anaweza kusoma makala kwa mtu fulani ambaye ni OG, hakuna haja ya kuja kwako wewe ambaye ni unakopi.

Kama mtu anaweza kusikiliza nyimbo kwa mtu fulani ambaye ni OG, hakuna haja ya mtu huyo kuja kwako ambaye ni gharasha. Kwa hiyo basi, tafuta uOG wako ulipo na ukuze huo.

Hivi ndivyo unaweza kuishi maisha ambay ni original

1.Usitake kuwa kama watu wengine. Kila mtu kaumbwa kwa ajili ya kusudi na jambo fulani, ukiamua kuiga maisha ya mtu mwingine maana yake huwezi kuwa wewe mwenyewe.

2. usijilinganishe na watu wengine ambao wamefika sehemu au wameweza kufanyia kazi jambo fulani na kulifikisha kwenye viwango fulani. Mtu pekee ambaye unapaswa kujilinganisha naye ni wewe wa jana na wewe wa leo. Ni wewe wa mwaka jana na wewe wa leo hii

Makala hii imeandikwa na Godius Rweyongeza

0755848391

Morogoro-Tz

Subscribe kwenye channel yangu ya youtube kwa kubonyeza hapa


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X