Mwandishi: Dale Carnegie
Mchambuzi: Hillary Mrosso
Mawasiliano: +255 683 864 281
UTANGULIZI
How to Win Friends and Influence People, ni moja ya kitabu bora sana kwenye kujenga urafiki, kutanza urafiki, kujenga mahusiano bora na watu na kuongeza ufanisi kwenye kazi na biashara. Ni kitabu kilichojaa hekima za kweli ambazo sio tu zitakushangaza, bali zitakufanya ubadilike na kujifunza namna bora ya kujenga ushawishi, na kuimarisha mahusiano yako na watu. Ni kitabu nilichokisoma kwa umakini mkubwa sana, nimekuandalia mambo 200 niliyojifunza ndani ya kitabu hiki cha ajabu. Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki tujifunze pamoja.
- Katika historia ya uchapishaji vitabu duniani, kitabu hiki cha namna ya kupata marafiki na kuwa na ushawishi kwa watu ndio kimekua kitabu bora sana kutokana na kuwa na mahitaji makubwa kuliko ilivyotazamiwa. Ni kitabu ambacho kimeuza nakala nyingi sana katika historia ya uchapishaji wa vitabu duniani kutokana na umuhimu wa mafunzo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
- Karibia nusu karne nzima, kitabu hiki kimekuwa katika hadhi ya juu sana ya uhitaji, licha ya kuwa ni kitabu kilichoandikwa miaka mingi iliyopita kimekuwa ni kitabu bora kwa zaidi ya nusu karne na kinaendelea kufanya vizuri katika masoko na mauzo yake.
- Kitabu hiki kimenukuliwa sana, kimetumika sehemu nyingi sana, kwenye siasa, mahusiano, urafiki, biashara na kwenye ajira. Kutokana na umuhimu wake, kimetafsiriwa kwa lugha nyingi sana zinazotumika hapa duniani.
- Katika maandalizi ya uandishi wa kitabu hiki, Dale anasema alisoma kila kitu alichokipata kuhusiana na somo la kitabu hiki, alisoma vitabu vingi sana, magazeti mengi sana, majarida, nukuu nyingi, nakala za kimahakama ya kifamilia, falsafa za kale, wasifu wa watu maarufu na pia alimfundisha msaidizi wake ili amsaidie kwenda maktaba kusoma na kuandika kila ambacho hakukisoma au alikisahau kuhusu somo la kitabu hiki.
- Utafiti alioufanya Dale kabla ya uandishi wa kitabu hiki uligharimu zaidi ya dola za kimarekani 25,000. Alitunga maswali 156 na aliwahoji watu wazima wote walioishi Meriden Marekani. Mwaswali yaliuliza, biashara, elimu, ujuzi, namna anavyotumia muda wa ziada, kipato, vitu anavyopenda, vipaji, matatizo, na mambo ambayo angefurahia kujifunza.
- Utafiti huu ulibaini kuwa somo la afya ndio lilipewa kipaumbele na watu wengi, jambo la pili kwa umhimu ni namna ya kuwa na mahusiano bora na watu, namna ya kuwa na ushawishi kwa marafiki na watu wengine.
- Mwandishi Dale anasema alitumia muda mwingi sana kwenye utafiti wake kabla ya kuandika kitabu hiki, alisoma nakala nyingi mno za watu wakuu kama Julius Kaizar, Thomas Edison, Theodore Roosevelt, John D. Rockefeller, Henry Ford, na wanafalsafa maarufu wa kigiriki na Roma, alisoma maisha yao, na namna walivyoweza kuishi na watu na mahusiano yao yalivyokuwa.
- Kitabu hiki hakikuandikwa tu kama vitabu vingine, ni kitabu kinachokua kama mtoto anavyokuwa, ni kitabu kilichotengenezwa kutoka maabara, kimehakikiwa kwa miaka mingi, na kimeakisi maisha yetu ya kila siku tunapoishi na kuhusiana na wanadamu wenzetu hapa dunaini.
- Mwandishi anasema tuna nguvu kubwa ambayo hatujaitumia ipasavyo, hivyo ni kusudi la uandishi wa kitabu hiki kuigundua, kuiendeleza na kufaidika na nguvu hiyo katika kujenga marafiki, kushawishi watu na kuwafanya watu wafanye kile unachotaka.
- Raisi wa Chuo Kikuu cha Princeton, Dr. John G. Hibben, anasema kama umesoma sura tatu za kitabu hiki na hujaona chochote cha kukusaidia kukabiliana changamoto za maisha au hali nyingine za maisha zinazohitaji elimu iliyomo katika kitabu hiki, basi uandishi wa kitabu hiki ni kazi bure na wala hakitakiwi kwenye jamii yoyote.
- Kama tunataka kuongeza uwezo wetu wa kukabiliana na watu, kuishi na watu vizuri na kwa mafanikio tunatakiwa kukisoma kitabu hiki na kuyafanyia kazi yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki.
- Mwandishi anasema, kama unataka unufaike na kitabu hiki unatakiwa utengeneze tamaa na shauku kali ya kujufunza, ona maisha yako hayatakuwa bora kama utakosa uelewa shaihi wa kuishi na watu, chukulia ujuzi huu kuwa wa muhimu sana hivyo utenge muda wa kutosha kujisomea kitabu hiki na kuweka kwenye matendo yale uliyojifunza.
- Mwandishi anasema soma kitabu hiki kwa kurudia kila sura uliyoisoma, usiwe na haraka katika kusoma kitabu hiki, labda kama unataka kusoma kama kujifurahisha. Lakini kama unataka ujuzi na maarifa muhimu kuhusu kujenga mahusiano bora na watu wengine, basi zingatia ushauri wa Dale katika kusoma kitabu hiki.
- Mwandishi anashauri, unaposoma kitabu hiki jaribu kutulia mara kwa mara kisha tafakari uliyojifunza, na ni kwa namna gani unaweza kuyatumia yaliyoandikwa kwenye kitabu hiki kuboresha mahusiano yako na watu wengine.
- Soma kitabu hiki ukiwa na kalamu ya rangi mkononi, ili ukiona sentensi au kitu ambacho unadhani unaweza kukitumia baada ya kusoma kitabu hiki uiwekee alama ili iwe rahisi kwako kurudia wakati mwengine.
- Unaweza kuajiriwa kama injinia, mhasibu, msanifu majengo au kwenye fani nyingine yoyote, mwandishi anasema atakayekuwa analipwa zaidi ni yule mwenye ujuzi mzuri wa fani yake pamoja na uwezo wa kuwa na mahusiano mazuri na watu, kuongoza, na kuwahamasisha wengine.
- Tajiri maarufu John D. Rockefeller aliwahi kusema uwezo wa kuwa na mahusiano mazuri na watu ni ni uwezo unaotakiwa kununuliwa kama sukari au kahawa, na anaendelea kusema atamlipa zaidi mtu ambaye ana uwezo huo kuliko mtu yeyote chini ya jua.
- Ni kawaida kwenye maisha yetu kuongea vile vitu tunavyotaka na tunavyotamani kuliko kuongelea matakwa ya watu wengine. Ndio maana ya kitabu hiki kimejikita kutengeneza tabia mpya hivyo inahitajika uvumilivu katika kuyafanyia kazi maarifa tuliyojifunza katika kitabu hiki.
- Katika utafiti wa Dale alipokuwa anajiandaa katika uandishi wa kitabu hiki aligundua kuwa asilimia kubwa wanataka maarifa kuhusu afya zao, na jambo jingine la pili ni maarifa ya kuishi na watu kwenye familia zao, kazini, au kwenye biashara zao.
- Kama unataka kufanikiwa katika biashara, kazi, au ajira hutakiwi kwenda chuo kikuu cha Harvard kujifunza tungo na mashairi magumu ya Shakespeer, au maneno ya kilatini, unahitaji uwezo wa kuwa na ushawishi, unahitaji kujenga ushawishi kwenye maisha yako.
- Mzungumzaji maarufu William Jennings Bryan aliwahi kusema, kila mtu ni mzungumzaji mzuri sana endapo atakuwa anajiamini na pia atakuwa na wazo linalochemka ndani yake. Mfano, ukikutana na mtu mjinga sana huko mjini ukampiga ipasavyo bila sababu, atainuka na kuanza kuongea kwa ujasiri mkubwa na kwa msisitizo mkubwa kuliko alivyokuwa anaongea kawaida.
- Dale anasema namna nzuri ya kutengeneza kujiamini ni kufanya vile vitu unavyovihofia au kuviogopa ni kuwa na rekodi ya mafanikio katika kufanya yale unayoyaogopa. Maana yake kila unapofanya yale unayoyaogopa unapunguza hofu, unaongeza kujiamini, hivyo rudia mara nyingi kufanya unachokiogopa ili ujenge rekodi nzuri ya mafanikio.
- Ukosojaji sio mzuri kwasababu unamuweka mtu anayekosolewa upande wa kujihami na mara zote atajihami na kutengeneza namna ya kujilinda na kujisafisha. Mwandishi anasema ukosoaji ni hatari sana kwani unazima furaha ya ndani ya mtu, unajenga maumivu, unaondoa hali ya kujikubali na kujiona mtu muhimu, ukosoaji unaleta majuto na wakati mwingine hali ya kulipa kisasi.
- Mwanasaikolojia maarufu sana duniani B.F. Skinner aliwahi kufanya jaribio moja muhimu sana kwa wanyama na kugundua kuwa mnyama anayepewa zawadi wakati anajifunza jambo fulani anaelewa kwa ufasaha zaidi na atakumbuka aliyojifunza kwa usahihi kuliko yule anayejifunza kwa adhabu.
- Mwandishi wa kitabu hiki anasema hata kujenga tabia mpya kwa binadamu ni rahisi endapo kutakuwa na zawadi badala ya kukoselewa na kupewa adhabu. Utajifunza haraka unapokubaliwa na kupewa zawadi pale unapofanya vizuri hata kama ni kwa hatua ndogo.
- Binadamu wengi tuna njaa na kiu ya kukubaliwa, kusifiwa na kuonekana wa maana kwenye maisha, mfanyakazi anahitaji maneno ya kumwinua na kupongezwa kwa juhudi zake, watoto na familia zetu wanahitaji kukubaliwa na kuonekana wanachokifanya ni cha muhimu na wana nafasi muhimu kubwa katika jamii.
- Kama wewe ni meneja wa kampuni fulani na kazi yako ni kuhakikisha wafanyakazi wanazingatia uvaaji wa kofia na zana za kazi wakati wanapokuwa kwenye kazi zao, hutakiwi kusimamia wafanyakazi na kutoa kauli za mamlaka kwa ambaye hajavaa kofia hizo eneo la kazi, badala yake unatakiwa uzungumze naye kwa lugha nzuri na kisha umueleze umuhimu wa kuvaa kofia hizo eneo la kazi.
- Asili ya binadamu wengi hatupendi kuamrishwa na mtu yeyote, hivyo kama unataka kuwa kiongozi au msimamizi mzuri ambaye watu watafuata kile unachowaambia huna budi kujifunza kujua kuwa kauli za kimamlaka haziwapendezi watu, wengi hawapendi waonekane wapo chini yako au watu wanaopokea maelekezo, wengi wanataka wao ndio wathaminiwe na wawe katika mashirikiano katika maamuzi.
- Kama unataka watu wafanye kile unachokitaka wakifanye basi usiwe mtu wa kutoa maelekezo, wala mtu wa kuongea kwa mamlaka, usiwafanye watu waone wako chini yako kufuata maekekezo yako, wafanye watu wajione wao ni wa muhimu na wanastahili heshima na wananafasi kubwa kwenye yote muhimu, wape watu umuhimu mkubwa, hapo ndipo watakapofanya yote uliyowaambia.
- Kama kuna mambo unataka watu wayafuate, wahusishe kwenye maamuzi, watu wanapenda sana wawe sehemu ya maamuzi, maana hii itajenga umoja na watatekeleza unachotaka, lakini ukiwa ni mtu wa kutoa maagizo tu, bila hata kuwajulisha italeta ugumu na upinzani katika utekelezaji.
- Tunatakiwa kujifunza kuwa tunapowakosoa watu kwa kutokufanya jambo fulani haisaidii sana kuleta matokeo ya kudumu, siku zote wale tunaowakosoa na kuona ni wakosaji huwa wanatabia ya kujihami na mara zote watatumia kila njia kujiona wao hawajakosea na wapo sahihi. Hivyo njia ya ukosoaji haiwezi kuleta ushirikiano mzuri baina ya mkosoaji na aliyekosolewa.
- Wengi tunatamani kuwabadilisha watu wengine, kuwakosoa wengine, kuwaongoza wengine, kuwarekebisha wengine. Mwandishi Dale Carnigie anasema kwanini unahangaika kuwabadili watu ambao huwajui, huna historia nao, hujui wana waza nini au kwanini wanafanya hicho wanachofanya, badilika wewe mwenyewe, jiboreshe na jiongoze wewe mwenyewe kwa mafanikio kwanza.
- Dale Carnagie anasema, inafaida sana kujikosoa mwenyewe kuliko kukosoa wengine, inafaida na inamaana sana kujiboresha wewe mwenyewe ili uwe mtu bora kuliko kuhangaika kuwabadili wengine wawe kama unavyotaka wewe wawe. Hizo nguvu unazotaka kuzitumia kubadili wengine zitumie kwako mwenyewe na utakuwa mtu bora sana.
- Moja ya mwanafalsafa maarufu wa China, Confucius aliwahi kusema jambo muhimu sana kuhusu kuona makosa kwa wengine, alisema, usilalamike kuhusu barafu kuganda kwenye paa la nyumba ya jirani yako, wakati ngazi za mlango wako ni chafu. Maana yake kama unaona uchafu kwa jirani yako ni huenda hujasafisha dirisha lako vizuri.
- Tukumbuke mara zote kuwa tunapoishi na watu huwa tunaishi na watu wasiofikiri kwa mantiki kila mara, tunatakiwa kujua watu ni viumbe wa hisia, viumbe wanaopenda kutiwa moyo, kuhamasihwa na kuambiwa vitu wanavyovipenda.
- Inahitajika zaidi diplomasia tunapoishi na watu au kuchukuliana na watu, usiwe mtu mgumu kwa watu, usikaze sura yako kwa watu, usijifanye mjuaji unapokuwa na watu, waseme watu kwa mema, waseme watu vizuri, kila lililojema liseme kwa watu.
- Kama unataka kupoteza marafiki au kokosa marafiki, basi uwe ni mtu wa kukosoa kila kinachofanyika, ukiwa mkosoaji sana watu hawatakupenda, hawatakusikiliza, hawatafanya kile unachotamani wafanye.
- Mtu mkuu ni yule anayeonyesha ukuu wake kwa namna anavyo watendea watu walio chini yake. Ukuu au cheo kisikufanye ukawadharau watu walio katika hali ya chini. Kamwe usiwadharau watu kwa namna yoyote ile, hakuna sababu nzuri ya kuwadharau watu, hakuna!
- Badala ya kuanza kuwadharau na kuwasema watu vibaya kwa yale waliyoyafanya, jaribu kuwaelewa, wakati mwingine jaribu kuvaa viatu vyao, jaribu kufikiria nafasi waliyonayo ungekuwa nayo wewe. Kama unataka kuwa kiongozi mwenye ushawishi kamwe usionyeshe dharau kwa watu.
- Jiepushe na kuhukumu wengine kwa wanayoyafanya, acha kabisa tabia ya kuhukumu watu wengine. Mwandishi anasema hata Mungu mwenyewe amechagua kutokuhukumu wanadamu sasahivi, amesema atahukumu siku za mwisho, wewe ni nani hadi uanze kuhukumu wengine?
- Wape watu nafasi kubwa ya kukosea na kukukosea, elewa makosa hutokea, hivyo unatakiwa kuwa mwenye uelewa kwa watu na pia itakusaidia kuwahurumia, kuwavumilia na kuwasaidia.
- Kuna njia moja to hapa duniani, na juu mbinguni, na chini ya jua, njia ya kumfanya mtu afanye kila unachokotaka, njia hiyo ni kumfanya mtu huyo apende kufanya unachotaka akifanye.
- Mwandishi anasema, unaweza kumlazimisha mfanyakazi akafanya kile unachokitaka hata kama hakipendi, unaweza kutumia nguvu zako kuwafanya watoto wako wafanye jambo fulani bila wao kutaka, lakini njia hizi hazilete matokeo mazuri na zinaweza zisileta mahusiano mazuri baina yenu.
- Njia nzuri na yenye tija ni kujua watu unaotaka wafanye unachotaka wanapenda kitu gani au wanataka kitu gani kwanza, kisha wape hicho wanachotaka kisha watafanya kile unachokitaka wakifanye.
- Usitumie vitisho, na adhabu ili watu wafanye unachokitaka, kumbuka hata watoto wako hutakiwi kutumia vitisho ile wafanya unayoyataka, jaribu kutumia zawadi na maneno mengine mazuri ya kusifia ili aweze kufanya unachokitaka wakifanye.
- Kumbuka siku zote kwenye maisha yako, moja ya hitaji kubwa la binadamu yeyote ni tamanio la kuwa wa muhimu, binadamu yeyote anatamani aonekane ni wa muhimu, na anataka watu watambue watambue umuhimu alionao. Matamanio na kiu ya kuonekana ni wamuhimu zaidi ya wengine ni moja ya tofauti kubwa iliyopo kati ya binadamu na wanyama.
- Kila mtu ndani ya moyo wake ana kiu na njaa kali sana ya hisia za kutaka kujulikana, kuonekana mtu wa maana na mwenye mchango mkubwa, mtu mkuu na muhimu. Binadamu wote wanatamani waonekane wao ni wa muhimu kuliko wenzao.
- Ni matamanio ya kutaka kujulikana ndio yalimsukuma Dickens kuandika moja ya riwaya bora sana. Ni tamaa ya kutaka kujulikana ndio hufanya watu wengine kwenye miji yetu kujenga majumba makubwa kuliko hata matumizi wanayohitaji.
- Ni tamaa ya kutaka kujulikana ndio ilimfanya tajiri maarufu duniani Rockefeller kujikusainyia utajiri mwingi sana, mali nyingi sana ambazo hakuweza hata kuzitumia.
- Ni matamanio ya kutaka kujulikana ndio hukufanya utamani kununua vitu vya gharama kubwa au kwenda na fasheni, kununua gari mpya na kuanza kuongelea kuhusu vipaji na uwezo mkubwa wa kiakili walionao watoto wako.
- Ukiniambia namna unavyopata hisia zako za kuwa mtu muhimu, naweza kukwambia wewe ni nani, maana yake ni rahisi kujua jinsi mtu alivyo kwa vile anavyovijali na vinavyompa kujiona muhimu kwenye maisha yake. Mfano, John D. Rockefeller alipata hisia zake za kuwa ni mtu muhimu kwa kutoa fedha kujenga hosipitali huko Peking China kusaidia mamilioni ya watu masikini ambao hawajui na hakuwahi hata kuwaona.
- Dillinger ambaye alikuwa jambazi, mwizi na muuaji mkubwa alipata hisia za kuwa yeye ni mtu muhimu kwa kazi zake za uhalifu wizi na uuaji. Na aliona fahari kujulikana kama mtu katili na aliyeshindikana. Hata wakati anakamatwa na polisi alijiita mimi ndio Dillinger, aliona fahari kwa jinsi alivyokuwa.
- Kuna tofauti kubwa sana kati ya John D. Rockefeller na Dillinger kwa namna walivyokuwa wanapata hisia zao kuwa ni watu muhumu. Hii inatukumbusha kuwa sisi binadamu tuna asili ndani yetu ya kutaka kujulikana, kutambulikana na kuchukuliwa kama watu muhimu na wenye mchango mkubwa hapa duniani.
- Historia ya dunia hii imejawa na mifano ya watu wengi maarufu waliopambania wajulikane au waonekane watu wakuu. Mfano ni George Washington Rais wa Markeni alitaka ajulikane au aitwe Mkuu sana, na rais Marekani. Kuna ambao waliomba watambulike kama wakuu wa kijeshi na makamanda wa ngazi za juu jeshini. Hata mke wa aliyewahi kuwa Raisi wa Marekani, Abraham Lincolin alitaka kujulikana kama mwanamke mwenye hadhi ya juu kwenye utawala wa nchi.
- Mshairi wa mapenzi na Mwanasiasa maarufu wa Ufaransa, Victor Hugo alikuwa hataki kingine kikubwa zaidi ya kutaka jiji la Paris liitwe kwa jina lake, hata mwandishi mashuhuri wa mashairi duniani William Shakespere alitamani kuitwa mkuu wa wakuu. Ukifuatilia historia imejaa watu maarufu waliotawaliwa na kiu na njaa ya kusaka kuwa wakuu au kuwa watu muhimu kwenye jamii.
- Ndugu msomaji wa uchambuzi wa kitabu hiki, asili ya binadamu ni kutaka kuonekana anafaa, ana umuhimu, ana ukuu na ni mtu anayweza. Hivyo kwenye kila eneo la maisha, mahusiano, biashara, kazi nk, tunatakiwa kutumia siri hii kuwapa wengine sifa wanazostahili, hii itafanya kuwa mwenye ushawishi na watu watakuwa karibu na wewe, kwasababu umewatambua ukuu wao.
- Usiwe sehemu ya kuua, kuharibu, kumtia aibu mtu mwingine, kumbuka binadamu wote wanapenda kuonekana wa maana na wenye umuhimu, hivyo hakikisha katika maisha yako ya kukutana au kuishi na watu utawakumbusha kuwa wao ni bora, wao ni muhimu, kamwe usiwakosoe au kuharibu ile hali yao ya kujisikia ni watu muhimu kwenye maisha.
- Unajua kunawatu wanadiriki kutumia hata njia ambazo sio sahihi ili tu apate umakini wako apate kuambiwa maneno mazuri ya faraja na kuinuliwa, watu wanataka tu na wewe uwaone kuwa wao ni watu wa muhimu, zingatia hilo katika maisha yako.
- Kuna watu wamekuwa kama hawana akili sawa sawa wanapofanya mambo yao, hii ni kwasababu wanataka wachukuliwa kama watu wenye umuhimu, au waambiwe kuwa wao ni watu wenye umuhimu sana kwenye jamii.
- Kwa bahati mbaya dunia yetu haipo tayari kuwafanya watu wajisikie ni watu muhimu, inawafanya watu wajione wanyonge, watu dhaifu na wasio na mchango. Hivyo kama unataka kuwa na ushawishi kwa watu inatakiwa ujue moja ya njaa kali aliyonayo binadamu ni kuonekana kuwa yeye ni wa muhimu.
- Mwandishi wa kitabu hiki ansema, kuna watu wengi nchini Marekani wana matatizo ya kiakili kwasababu tu ya kukosa kuambiwa wao ni watu bora na watu wenye umuhimu hapa duniani, kuna wengi sehemu nyingine duniani wana msongo wa mawazo na matatizo mengine ya kiakili kwasababu hawajaambiwa na mtu yeyote kuwa wao ni watu muhimu.
- Mwandishi anasisitiza kuwa kuna watu wenye matatizo ya kiakili yaliyosababishwa na magonjwa kama syphilis ambayo husababusha uharibifu wa seli za ubongo na kupelekea watu kuwa na matatizo ya kiakili, lakini mwandishi anaeleza zaidi kuwa, nusu ya watu waliopata matatizo ya kiakili ni kutokana na seli kuharibika kutokana na uvimbe kwenye ubongo, sumu, ulevi/pombe na ajali. Hata hivyo nusu iliyobakia wanaopata matatizo ya kiakili ni kutokana na kukosa hisia za upendo, kukubaliwa, na kuonekana watu wenye umuhimu.
- Watu wengi ambao wanamatatizo ya kiakili walifanyiwa vipimo na kuchunguza uharibifu wa seli ambazo huenda ndio zimasababisha watu kuwa na matatizo ya kiakili, utafiti wa kitabibu ulibainisha kuwa wengi wao, seli za ubongo wao zilikuwa zenye afya tele, na kulikuwa hakuna ugonjwa wowote kwenye seli za ubongo wao. Hivyo watu wenye matatizo ya kiakili wanaweza kuwa wamekosa umuhimu tu kwenye maisha yao ndio maana wanakuwa na msongo mbaya wa mawazo unaowapelekea kuonekena kama wamechanganyikiwa.
- Dale Carnegie baada ya kufanya mahojiano ya kina na madaktari bingwa kwenye kitengo cha afya ya akili ili aweze kubaini kwanini watu wanapata matatizo ya kiakili na kuonekana kama wamechanganyikiwa, daktari yule alijubu, hajui hasa kwanini watu wanakuwa na matatizo ya kiakili ila inawezekana wengi wanataka kusikia habari njema kama wao ni watu wanaofaa na wenye umuhimu kwenye jamii.
- Mwandishi anasema kama watu wana njaa ya kuonekana watu muhimi kiasi hiki cha kufikia kuwa na matatizo ya kiakili, sasa fikiria namna unavyoweza kuwasaidia na kuinua tena matumaini ndani yao kwa kuwaambia ukweli kuwa wao ni watu muhimu na wana umuhimu mkubwa sana kwenye maisha.
- Watunuku watu, wape zawadi watu, washukuru watu, wapende watu, wainue matumaini yao, waonyeshe wao ni watu muhimu, waonyeshe wao wanastahili kilicho bora. Kwa kufanya hivyo watakuwa tayari kufanya chochote unachowaambia wafanye bila shida.
- Hakuna kitu kinaua ndoto nyingi kama kuhukumiwa na kukosolewa na watu walio juu yako au watu unaowaheshimu sana. Mwandishi anataka tuache kutumia njia hii ya kukosoa watu, tuwapongeze hata kwa hatua ndogo wanazochukua kila siku ili kuboresha maisha yao na kufikia ndoto zao.
- Watu duni na wakawaida hawana utamaduni wa kuwasifia au kuwapongeza watu wengine wanapofanya vizuri, hawawezi hata kutoa zawadi, wananyamaza tu mtu anapofanya jambo zuri. Lakini mtu anapokosea, wanaanza kumkosoa, kumuhukumu, na kumsema vibaya, jambo ambalo linakatisha sana tamaa na kuondoa ari ya kufanya kazi kwa ufanishi.
- Usitegemee kwamba ukimkosoa mtu kwa kila anachokifanya ndio atakifanya vizuri zaidi. Sio mara zote kukosoa kunaleta matokeo mazuri, wakati mwingine unawavunja moyo wale unaowakosoa. Mwandishi anasema, njia nzuri na yenye matokeo ya kudumu ni kupongeza na sio kukosoa na kuhukumu pale mtu anapokosea, hata kama mtu amekosea kwenye kufanya jambo lake tafuta namna nzuri ya kumuelekeza na kumsifia kwa juhudi zake na sio kumsema vibaya.
- Carnegie alifanikiwa sana katika kujenga na kuwa na mahusiano mazuri na watu wengi kwasababu aliwasifia na kuwapongeza watu bila unafiki, na alifanya hivyo mbele ya watu wengi, mbele ya uma na umati wa watu, pia anasema aliwapongeza pia hata wakiwa faragha.
- Kuna wengi wetu tunafanyiwa vitu vizuri na watu lakini hatujawahi kuwajali au kuwapongeza au kutambua umuhimu wao kwenye maisha yetu. mfano, inawezekana kuna sehemu unakula kwenye mgahawa hapo mjini, chakula ni kitamu, na kila siku unaenda kula na kulipa tu, hujawahi kumwambia mpishi au yule anayekuhudumia umuhimu alio nao kwako, kwa namna anavyopika chakula kizuri, kwa namna anavyo jitahidi kila siku kufanya kazi nzuri ya upishi.
- Ni vizuri kutambua mchango na umuhimu wa watu kwenye maisha yetu, kazi zetu, mahusiano yetu, familia zetu na kwenye biashara zetu. Tambua jitihada zao, wapongeze na waambie jinsi unavyoguswa na kufurahishwa na juhudi zao za kila siku. Mfano, John D. Rockefeller alitambua jitahada za msaidizi wake wa masuala ya fedha, licha ya kwamba yule msaidizi wake alihusika katika upotevu wa asilimia 60 ya pesa, lakini Rockefeller hakuangalia kwenye makosa aliangalia kwenye yale mazuri aliyoyafanya na kumpongeza. Jambo ambalo lilimfanya msaidizi wake kuongeza umakini na kufanya kazi kwa karibu zaidi na bosi wake.
- Kwenye utafiti uliofanyika kwenye masuala ya mahusiano na ndoa, umegundua kuwa wengi wanaokimbia mahusiano yao, au kukimbia familia zao au kuvunja ndoa zao ni kutokana na mmoja au wanandoa wote kushindwa kutambua mchango wa mwenza wake. Wengi hawajali wanaishi kwa mazoea na kuona ni haki yake kufanyiwa anavyofanyiwa, hii inaleta mpasuko.
- Hatutakiwi kuchukuliana poa poa kwenye mahusiano, tunatakiwa kujua mahitaji muhimu ya kila mmoja, pia tunatakiwa kuwa watu wa shukrani, unaweza kufanyiwa jambo kidogo na mpenzi wako, lakini usishukuru hii inaleta ukakasi sana kwenye mahusiano, shukuru kwa kila kizuri anachokufanyia mwenza wako. Hii itaongeza ukaribu na kila mmoja atajiona ana umuhimu mkubwa kwa mwenzake.
- Kuna wakati tunaboresha sana miili yetu kwa kuipa virutubisho vyote muhimu, tunafanya hivyo kwa watoto wetu, marafiki zetu na ndugu zetu, lakini ni mara ngapi tumekuwa tukiwapa maneno mazuri ya kuinua hamasa yao ya ndani, ni mara ngapi tumewaambia maneno ya matumaini yatakayowafanya wajione ni watu wenye umuhimu kwenye maisha yetu? Mwandishi anasema, tusilihse mwili pekee tulishe na nafsi zao hasa eneo la hisia ambalo huwagusa wengi.
- Kumbuka siku zote, chakula unachompa kitapita, lakini maneno mazuri hayatapita, yatabakia kuwa kumbukumbu nzuri kwenye maisha yake. Maneno yana nguvu tumia nguvu hiyo kuwatia wengine nguvu ya kufanya makubwa kwenye maisha yao.
- Mwandishi Dale anasema tuepuke kuwapa watu sifa za kinafiki, tusiwapake watu mafuta kwa mgongo wa chupa; ingawa huwa inatokea watu wenye njaa ya kutaka kuonekana wao ni bora na watu muhimu wanachukua tu sifa zozote bila kujali ni za kinafiki au ni za kweli. Hii ni kwasababu mtu mwenye njaa anaweza kula kila kitu hata kama ni kibaya.
- Dale anasema, tofauti kati ya sifa za kinafiki na sifa za kweli ni kwamba, moja inatoka kwenye vilindi vya moyo na nyingine inatoka kwenye meno. Tujifunze kutoa kutoka moyoni, usiseme tu ili mradi upate unachotaka, kuwa mkweli kwako mwenyewe kwa kumpa mtu sifa anazostahili.
- Moja ya falsafa maarufu sana ilikuwa ikitumika na aliyewahi kuwa shujaa na mkuu wa majeshi ya Mexico Jenerali Alvaro Obregon, alisema, usiogope maadui wanaokushambulia, bali waogope marafiki wanaokupa sifa za kinafiki. Maana yake ni marafiki wanaokusifia kinafiki wanaweza kukudhuru muda wowote maana unaishi nao karibu kuliko adui anayekushambulia.
- Mfalme George wa tano, aliweka moja ya kauli zake maarufu na kuzibandika sehemu anayojifunzia, kauli hiyo ilimaanisha, Nifundishe kabla ya yote kutopokea sifa za kinafiki au sifa nyepesi nyepesi. Kwa siku za karibuni hapa Tanzania watu wanaweza kukusifia kuwa “unaupigwa mwingi”. Mwandishi anasema usikubali kupokea sifa za bei rahisi, wala usitoe sifa za kinafiki kwenye jambo unalojua uhalisia wake.
- Mwandishi Dale anasema, moja ya tunu iliyopotea katika jamii yetu ya sasa ni shukrani, watu hawana shukrani kabisa, watu hawaoni umuhimu wa kutambua juhudi za watu wengine kwenye maenedeo yao, mfano tunashindwa kuwapongeza watoto wetu wanapofanya vizuri shuleni, tunashindwa kuwapongeza mabinti zetu wanapojitahidi na kujifunza kupika au kuoka mkate, hatuoni umuhimu wa kuwapongeza wale wanaojitahidi kufanya usafi kwenye maeneo yetu.
- Hapa duniani tunapita, tunaishi mara moja tu, hivyo kama kuna wema wowote unaotakiwa kuufanya ufanye, kama kuna mambo mazuri yanatakiwa kufanyika yafanye kwa nguvu zako zote maana, inawezekana usipate nafasi ya kuja kufanya mambo hayo tena.
- Tunatakiwa kuishi kwa unyeyekevu hapa duniani, kwasababu hatujui kila kitu na kila mtu unayekutana naye kuna kitu anakuzidi, kuna kitu anakijua ambacho wewe hukijui, hivyo kuwa tayari kuwapa watu heshima na pia kuwa tayari kujifunza kutoka kwao.
- Kila mtu hapa duniani anaongea vitu anavyovitaka, anaongea matakwa yake au matamanio yake mwenyewe. Hivyo kama unataka kuwapata watu na kuwa na ushawishi mkubwa kwa watu unatakiwa uongee agenda zao, unatakiwa kujali yale wanayoyatamani kuyapata, unatakiwa kuwa karibu na matamanio yao, kisha waonyeshe namna ya kufikia matamanio yao na ndoto zao.
- Ukitaka kuwa kiongozi mzuri ambaye utadumu kwenye uongozi kwa muda mrefu, acha kujali zaidi matakwa yako, jali zaidi matakwa ya wale unaowaongoza, waambie kutoka moyoni namna unavyojali shida zao, namna utatatua hangamoto zao, namna utawapa haki zao, ukiwa tayari kufanya hivyo utakuwa na wafuasi wengi wa kweli ambao wanaweza kukufuata hata gerezani.
- Kama unatamani watu waache kuvuta sigara, usiwafuate na kuanza kuwahubiria waache sigara, ukifanya hivyo hawatakusikiliza wataendelea na uvutaji wa sigara kwasababu unataka wafuate matakwa yako, lakini ukitaka kuwafanya waache sigara waonyeshe namna sigara inavyoweza kuzuia kuzifikia ndoto zao wanazozitamani sana, waonyeshe vitu wanavyovijali sana kwenye maisha yao kisha waambie endapo wataendelea na uvutaji wa sigara hawataweza kuzifikia ndoto zao na matamanio yao.
- Harry Overstreet kwenye moja ya kitabu chake maarufu kilichoitwa, “Influencing Human Behaviour” alisema, matendo ni matokeo ya matamanio ya mtu, akimaanisha ili mtu afanye au atende jambo fulani lazima jambo hilo liwe limetokana na matamanio yake. Maana yake matamanio huzaa matendo, kama tunaweza kujua matamanio ya watu tunaweza kuyatumia matamanio yao kufanya yale tunayoyataka ili watimize matamanio yao.
- Ili tuweze kufanikiwa kwenye biashara, mahusiano, kazi na kwenye siasa lazima tujifunza kuyatambua matamanio ya watu, tujue kwa kina ni kitu gani watu wanakihitaji sana, tukishajua watu wanachokitaka kazi inabaki kuwatafutia kitu hicho, wakikipata walichokihitaji basi watakupa unachikihitaji pia.
- Shida yetu tunatanguliza sana mambo yetu mbele mno, tunataka wateja waje wanunue tu ili sisi tupate fedha, tunataka watu watupigie kura ili tuwe viongozi tutimize ndoto zetu, tunataka watu watufanyie kazi tu ili tutimize ndoto zetu, kwenye mahusiano tunataka tupewe zaidi umakini na kusikilizwa zaidi. Mwandishi anasema, hakuna kanuni inayofanya kazi kwa namna hii, kama tunataka kufikia ndoto zetu, basi tuwasaidie wengine kuzifikia ndoto zao pia.
- Usichukue tu pesa ya mteja wako, angalia ni namna gani na yeye ataongeza thamani kwenye maisha yake endapo atanunua au atafanya biashara na wewe, angalia na jali zaidi maslahi ya mteja wako kuliko kuangalia tu fedha anayokupa, kwa kufanya hivyo utakuwa na wateja wa kudumu wanaopenda kuja kununua bidhaa zako.
- Upande wa mahusiano, usiwe mtu wa kupokea tu bila kuangalia upande wa mwenzako, usione kuwa wewe ndio unastahili kutendewa mambo mazuri zaidi kuliko mwenzako, kama mpenzi wako anakupa zawadi, au fedha, muda au chochote kile, usiwe mpokeaji tu, angalia namna unaweza kumfanyia ili na yeye aone thamani ya uwepo wako kwenye maisha yake, kila mtu ajitahidi kuongeza thamani ya mwenzake, kila mtu amfanye mwenzake aonekane ni wa maana na ni wa muhimu kwenye maisha yake. Kwa kufanya hivyo kutakuwa na mahusiano mazuri na kila mmoja ataona umuhimu kwa kuwa na mwenzake, usimlemee mwenzio kwenye mahusiano.
- Kwenye siasa, kama watu wamekupa ridhaa ya kuwawakilisha kama kiongozi wao, jihadhari usije ukawasahau, kama uliwaahidi utawafanyia jambo fulani, hakikisha unawafanyia, kama uliapa kuisimamia katiba ili kulinda mali ya uma fanya hivyo kwa nguvu zako zote. Angalia, inawezekana umetimiza matamanio yako kwa kupata nafasi ya uongozi, fanya juhudi kutimiza matamanio ya waliokupa ridhaa ya kuwaongoza, ili ujiepushe na lawama za watu.
- Bilionea Henry Ford aliwahi kusema, kama tunataka kuwa na mahusiano bora na watu tunatakiwa kuwa makini sana kwenye mazungumzo yetu, alimaanisha tuwe na uelewa wa kuelewa mitazamo na mapendekezo ya mtu mwingine. Toa nafasi ya mazungumzo kwa mtu mwingine ili aeleze jambo lake na mitazamo yake, usiwe mtu wa kutaka mawazo yako tu ndio yaonekane bora kuliko mawazo ya mtu mwingine.
- Moja ya sanaa bora sana kwenye kujenga urafiki na kuwa na ushawishi kwa watu ni kujali sana mawazo na mitazamo ya watu wengine, kamwe usiwakosoe watu wanapojaribu kuelezea mitazamo na maoni yao, yape umuhimu na uzito mazungumzo ya watu wengine, hii itawafanya wajione wanasikilizwa na pia watajiona ni watu wenye umuhimu sana kwako.
- Unapokuwa na wenzako usitake kutawala mazungumzo, wape watu wengine muda mwingi wa kuzungumza hisia zao na mitazamo yao, waoneyeshe kuwa upo pamoja nao kwa kuwapa umakini wako wote, na pia unaweza kuwahimiza wazidi kuongea zaidi kuliko wewe. Kitendo cha kuwapa wengine nafasi kubwa ya kujieleza na kuongea hisia zao na mitazamo yao kinawafanya wajiamini na wajione wao ni wa muhimu na wataishia kukupenda sana na watatamani kuwa karibu na wewe zaidi.
- Moja ya saikolojia muhimu kwenye biashara yoyote, unapokuwa na wazo la biashara usilifanye wazo hilo kuwa ni lako mwenyewe, au ukakaa nalo mwenyewe, washirikishe watu wako wa karibu ambao unafanya nao biashara, na wao walione wazo hilo kama lao, kwa kufanya hivyo utaweza kuboresha biashara yako, maana watafanya kama ni wazo lao.
- Angalia kile anachikitaka mwenzako, kisha unganisha na kile unachokitaka wewe kwa kutimiza kile anacho kitaka mwenzako ili mwenzako afanye kile unachokitaka wewe. Usiwe mbinafsi kwa kutaka mambo yako tu ndio yaenda, na ya wengine pia yanatakiwa yaende ili wote muwe na ufanisi wa kufanyika kazi ndoto zenu.
- Unaweza kupata marafiki wengi kwa muda mfupi, unaweza kupata watu wengi wanaokufurahia kwa muda wa miezi 2 kwa kuonyesha unajali sana mambo yao, kuliko kutumia zaidi ya miaka miwili kutaka watu ndio wakufurahie wewe tu au wakufuate wewe tu.
- Mwanasaikolojia maarufu wa Vietinamu, Alfred Adler, kwenye kitabu chake kilichoitwa “What Life Should Mean to You”, alisema, mtu pekee anayepitia magumu kwenye maisha yake ni yule ambaye hamfurahii mwenzake, Adler anaendelea kusema kuwa mtu wa aina hii ndio anasababisha majeraha kwa mwenzake na pia mtu wa aina hii ndio kushindwa hutokea kwake mara zote.
- Kama huwezi kuwafurahia watu kwenye maisha yako, huwezi kuwa na hadithi nzuri za mafanikio, kuwafurahia watu ni muhimu sana kwenye safari ya mafanikio, kama huwafurahii watu hutaweza hata kuwapa zawadi, huwezi hata kuwaandikia kitabu kizuri.
- Kuwafurahia watu wengine ni muhimu sana kwenye biashara, maana kama huwafurahii watu hutapata watu wa kuwauzia bidhaa zako, kama hufurahii watu hutaweza kuwaandalia bidhaa bora, hutaweza kuwapa huduma nzuri.
- Ukiwa na tabia ya kuonyesha kuwafurahia watu unaweza kupata fursa na muda wa kukutana na watu maarufu, makampuni makubwa na pia unaweza kupewa ushirikiano ambao usingetegemea uupate kirahisi.
- Ili kujenga mahusiano mazuri na watu, waonyeshe kuwa unawajali na unawafurahia bila unafiki wowote, waonyeshe kwa vitendo ni gharama gani unaingia kwasababu yao, waonyeshe wewe upo na unafanya mambo mazuri kwasababu ya umuhimu walionao kwako.
- Muonyeshe rafiki, mteja, mfanyakazi, au msaidizi wako jinsi unavyopendezwa naye, muoneyeshe jinsi alivyo muhimu na anastahili huduma bora kutoka kwako.
- Unajua tunaposoma uchambuzi wa kitabu hiki sio kwamba tunagundua ukweli mpya ambao tunatakiwa kuufahamu, hapana, hapa tunasoma kanuni zilizofanya kazi miaka mingi iliyopita hata kabla ya Kristo kuja duniani, kama ilivyoandikwa katika moja ya mashairi maarufu ya Roma, yaliyoandikwa na Pubililius Syrus, ambaye aliandika kuwa; “tunavutiwa sana na wale wanaovutiwa na sisi”. Maana yake, unapopendezwa na watu, watu pia watapendezwa na wewe, unapowafurahia watu, watu watakufurahia pia.
- Professor James V. McConnell, ambaye pia ni mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani alisema kitu kimoja kuhusu kutabasamu, alisema, watu ambao wanatabasamu wanaweza kufundisha na kuuza kwa ufanisi lakini pia wanaweza kukuza watoto wenye furaha sana. Professor James anasema, kuna taarifa nyingi kwenye tabasamu kuliko kukunja sura; ndio maana kupongeza ni njia nzuri ya kufundisha kuliko adhabu.
- Meneja wa masuala ya ajira nchini Marekani aliwahi kusema kauli moja ya ajabu sana, alisema, ni bora kuajiri mtu wa kawaida ambaye hajahitimu shule, lakini mwenye tabasamu linalipendeza na kuvutia kuliko kuajiri msomi wa shahada ya uzamivu (PhD) mwenye uso uliokunjamana na usioonyesha furaha.
- Tabasamu lina nguvu sana hata kama halionekani, makampuni ya simu nchini Marekani walikuwa na programu moja iliyoitwa nguvu ya simu (phone power), ambayo ilitumiwa na mfanyakazi kuuza bidhaa au huduma zao. Moja ya masharti ya matumizi ya simu hii ilikuwa ni kutabasamu unapoongea na simu, wakiamini kabisa kuwa tabasamu lako linatokea kwa njia ya sauti. Matokeo ya program hii yalizaa matunda maana kila aliyepokea simu na yeye alitabasamu, hivyo kufanya mazungumzo kwenda vizuri na huduma kufanyika kwa ubora.
- Wachina ni watu wenye hekima sana hasa kwenye mambo ya kidunia, kuna moja ya mithali zao maarufu sana kuhusu tabasamu, inasema, “mtu ambaye hana tabasamu usoni hatakiwi kuuza duka”. Ikimaanisha muonekano wa sura yako ni muhimu sana katika biashara, hivyo kitu muhimu kinachotakiwa kuonekana kwenye sura yako ni tabasamu la kweli endapo unataka kufanya biashara na kuwa na wateja wengi.
- Mwandishi wa kitabu hiki Dale Carnigie, anatushauri tuwe watu wa kutabasamu, maana tabasamu linatoa mvuto kwa msikilizaji, pia linafanya mazungumzo kwenda vizuri na ni rahisi kuafikiana kwenye mazungumzo au majadiliano.
- Jitahidi kuwa na changamko la furaha moyoni mwako, hii itafanya uwe na hisia nzuri za furaha ambazo zitakufanya ufanye mambo yako kwa furaha na kwa ufanisi mkubwa.
- Kila mtu hapa duniani anatafuta furaha, na kuna njia moja ya uhakika ya kupata furaha, njia hiyo ni kuthibiti mawazo yako, maana yake uwe na maamuzi au mamlaka ya mwisho juu ya mawazo yako. Furaha haitengemei hali ya mambo ya nje yanavyokwenda, furaha inategemea hali ya mambo inavyokwenda au ilivyo ndani yako.
- Sio ulivyo navyo au jinsi ulivyo au sehemu ulipo au unachokifanya ndio kinakufanya uwe na furaha au usiwe na furaha. Bali ni vile unavyofikiri. Mfano manaweza kuwa sehemu moja, kufanya kazi moja, kulipwa kiwango sawa cha mshahara na faida nyingine, lakini unaweza kukuta mmoja ana furaha na mwingine hana furaha, kwanini? Ni kwasababu ya namna wanavyofikiri kwenye fahamu zao.
- Mwandishi anakiri kuona watu wengi masikini wakiwa na furaha katikati ya hali duni na ya kusikitisha na jua kali wakifanya kazi mashambani kwa zana duni kabisa, halikadhalika, ameona pia nyuso zilizokosa furaha zimekaa kwenye viti vya kuzunguka katika ofisi za kifahari kwenye miji mikubwa duniani kama vile New York, au Los Angeles, Marekani. Hii ina maaana kuwa hakuna kibaya wala kizuri, ni mitazamo yetu tu ndio huvifanya viwe vibaya au vizuri, kama alivyonukuliwa gwiji wa mashairi William Shakespere.
- Tumepewa nguvu ya uumbaji ndani yetu kupitia mawazo yetu, maneno yetu na matendo yetu, unachokiwaza kinaweza kutokea, unachokifanya kinaweza kutokea, unachokiomba kinaweza kutokea, hivyo basi tuna sifa ya kiungu ndani yetu, tuitumie vizuri kwa manufaa kujenga na sio kubomoa.
- Tabasamu lako ni ujumbe mzuri wa matumaini, tabasamu lako ni nuru kwa wote wanaokuona, tabasamu lako ni kama nuru ikipasua mawingu, tabasamu lako ni muhimu sana maana wengi wanaopitia changamoto za maisha wanaweza kuona matumaini kwako, usiwaonyeshe watu uso uliokata tamaa na usio na matumaini, waonyeshe watu nuru kwa kuonyesha tabasamu usoni pako.
- Tabasamu lako linaashria kuna matumaini duniani, hatakugharimu chochote kuonyesha tabasmu kwenye uso wako, huitaji kuwa tajiri wala masikini ndio uonyeshe tabasamu, kila mtu anaweza kutabasamu na kufungua milango ya furaha, mashirikiano na faida kwa wengine.
- Aliyekuwa mfanya biashara na CEO wa kampuni ya Ford, Jim Farley, aligundua mapema sana kwenye maisha, kuwa kila binadamu anavutiwa zaidi na jina lake kuliko majina yote yaliyopo duniani. Hivyo basi kama unataka kujenga urafiki mzuri na watu, jitahidi kukumbuka na kutaja au kuandika majina yao kwa usahihi.
- Majina ya watu yana maana sana kwao, watu wanayapenda majina yao, watu wanapenda kuitwa kwa majina yao. Muhimu sana ni kujua majina ya watu unaohusiana nao, yatamke vizuri na kwa usahihi wa hali ya juu, na endapo unashindwa kutamka au kuandika jina la mtu kwa usahihi kwasababu ni gumu, ni bora umuombe akusaidie namna linavyoandikwa na namna linavyotamkwa.
- Endapo utashindwa kutamka jina la mtu kwasababu ni refu au ni gumu, unaweza kulifupisha, ili liwe na mvuto, mfano, kama mtu anaitwa Nikodemas, unaweza kumuita “Nick’. Chukulia kwa uzito sana majina ya watu.
- Watu wanajivunia sana majina yao kiasi kwamba anataka jina lake liendelee kuwepo kwa vizazi vingi. Mfano, P.T. Barnum ambaye alikuwa mtu maarufu sana kwenye maonyesho mengi, alijisikia vibaya sana kwa kuwa hakuwa na mtoto wa kuchukua jina lake, hivyo alitoa dau kubwa sana kwa mjukuu wake aliyeitwa C.H. Seeley, kiasi cha dola 25,000 ili ajiite Barnum badala ya Seeley.
- Karibu kila kanisa duniani lina majina ya watu waliotoa au kufadhili ujenzi wa kanisa hilo, ukiangalia kwenye kuta nyingi za makanisa hayo makubwa utaona majina ya wafdhili hao yakiwa yamepambwa na kupendezeshwa kwa heshima kubwa. Hata majengo ya vyuo vikuu vingi vina majina ya wafadhili waliojitoa kujenga au kugharamia ujenzi, hivyo wanaenzi majina na mchango wao kwa heshima kubwa kiasi cha kuyaandika kwenye majengo na kwenye kampasi zao mbali mbali.
- Uwezo wa kukumbuka majina ya watu ni muhimu sana kwenye kila eneo la maisha, iwe ni biashara, kwenye jamii au kwenye siasa.
- Napoleon wa tatu, mtawala wa Ufaransa, ambaye alikuwa ni binamu ya Napoleon mkuu, aliwahi kusema pamoja na majukumu yote ya kifalme, aliweza kukumbuka majina ya kila mtu aliyekutana naye, moja ya mbinu yake kuu ilikuwa kama hakusikia jina la mtu vizuri aliomba msamaha na kusema, samahani, sikuweza kusikia jina lako vizuri, na kama sio jina la kawaida, aliuliza kama anaweza kutaja herufi za jina lake ili alinakili na kutamka kwa ufasaha.
- Mambo haya yanagharimu muda, lakini kama alivyowahi kusema mwanafalsafa, Emerson, kila kitu kizuri kinachukua muda, lakini tabia njema zinatengenezwa kwa sadaka kubwa au gharama kubwa; tabia ya kukumbuka majina ya watu ni muhimu na ni jambo zuri kulifanya ili kuboresha mahusiano.
- Mwandishi wa kitabu hiki anasisitiza sana kuwa msikilizaji zaidi kuliko kuwa mzungumzaji. Kuna watu wamejiandaa tu kuongea na kusikilizwa, lakini masikio yao hayajafunguka kusilikiliza wengine wakiongea.
- Mafanikio yoyote kwenye biashara, sio kwasababu ya miujiza, ni kama alivyoshauri aliyekuwa raisi wa Chuo kikuu cha Harvard Charles Eliot kuwa ni kumpa umakini wako mzungumzaji, au mteja wako. Maana yake hakikisha unawasikiliza zaidi wateja wako, uwe msikilizaji mzuri.
- Watu wengi wanakosa watu wa kuwasililiza, kuna watu wanapata hadi magonjwa ambayo yanawapeleka kwa dakatri, mwandishi anasema kuna watu hawahitaji kumuona daktari, wanahitaji hadhira ili waweze kuelezea hisia zao na mambo waliyoyabeba kwenye mioyo yao.
- Tengeneza tabia nzuri ya kusikiliza watu, usichague watu utakao wasililiza, hata kama ni mtu masikini na unaona kama hana cha kuongea, jaribu kumsikiliza na kumpa umakini wako pale anapotaka kukueleza au kuzungumza jambo lake, fanya hivyo kwa watu wote bila kujali cheo, umri, kazi au hadhi ya mtu.
- Kuna watu watapona endapo watapewa nafasi ya kuzungumza na kusikilizwa, mfano aliyekuwa Raisi maarufu sana wa Marekani, Abraham Lincolin, aliwahi kusema haitaji wazungumzaji, anahitaji wasikilizaji wazuri ambao watamsikiliza kwa makini ili azungumze yaliyoujaza moyo wake, kusikilizwa pale unapozungumza ni kama vile kutua kitu kizito, unabakia kuwa mwepesi.
- Dunia inahitaji zaidi wasikilizaji wazuri kuliko wazungumzaji, mfano kama unafanya biashara kuna wale wateja wanaleta malalamiko kwenye biashara yako, usianze kubishana nao, waache waongee yote yaliyo moyoni mwao, unachotakiwa kufanya ni kuwa mpole na kuwasikiliza kwa makini, jambo hili linamfanya mteja apunguze hasira na awe huru na mwepesi zaidi.
- Kama umepewa nafasi ya kuzungumza punguza kujizungumzia mafanikio yako, punguza kujifagilia, na usiongee kwa muda mrefu, kama kuna mwingine anataka kuzungumza, nyamaza, mpe umakini wako na umuache azungumze hadi atakapo maliza.
- Usimkatishe mtu mwingine katika mazungumzo yake, usimkosoe au kumpiga pale anapoelezea jambo lake, subiria hadi anapomaliza mazungumzo yake ndio na wewe uzungumze. Unachotakiwa kufanya ni kumpongeza kwa mambo uliyojifunza kupitia mazungumzo yake na sio unasimama na kuaza kumkosoa, kumfanya aonekane hajui, jambo hili ni baya na linaondoa urafiki.
- Aliyekuwa Raisi wa muda mrefu wa Chuo Kikuu cha Columbia, Dr. Nicholas Murry Butler, aliwahi kusema, watu wanaojizungumzia wao wenyewe wanafikiRI kwa ajili yao wenyewe, ni watu wasio na matumaini, ni watu ambao hawajaelimika, hata kama walijifunza na kusoma kiasi gani bado ni wajinga na wasioelimika. Usipende kujisifia mbele za watu kwenye mazungumzo yako, wasifie wengine na tambua mchango wao kwenye mafanikio uliyonayo au hatua unazochukua.
- Kama unataka kuwa mzungumzaji bora, kuwa msikilizaji bora kabisa, kama unataka watu wakufurahie, wafurahie wao kwanza. Uliza maswali ambayo mzungumzaji atajisikia vizuri kuyajibu, muhamasishe unayemsikiliza azungumze zaidi kuhusu yeye mwenyewe na mafanikio yake. Kwa kufanya hivi utakuwa mtu bora sana ambaye kila mtu atataka kuwa karibu na wewe.
- Kumbuka watu unaozungumza nao au wanaokusiliza wanajali mara mia zaidi maslahi yao na shida zao kuliko maelezo yako na shida zako, watu wanajali kile wanachokitaka, wanajali namna ya kutatua changamoto zao, hivyo usiwachoshe kwa kuzungumza mambo ambayo hawayapendi, zungumza namna unavyoweza kutatua changamoto zao, hapo watakusikiliza hata masaa 10.
- Mtu mwenye maumivu ya jino anajali sana kuhusu maumivu anayoyapata kuliko majanga ya njaa yanayoua watu huko China na Somalia; mtu anayeumwa na tumbo anajali sana tumbo lake kuliko matetemeko ya aridhi yanayoua mamilioni ya watu huko Afirka. Hivyo ndio asili ya binadamu ilivyo ndugu yangu.
- Moja ya aliyewahai kuwa Rais wa maarufu wa Marekani, Theodore Roosevelt alipokuwa anatarajia kutembelewa na mgeni, alikuwa ana tabia ya kukesha usiku kutafuta na kusoma kuhusu mambo anayoyapenda mgeni wake, alisoma wasifu wake na kufuatilia mambo anayoyajali na kuyapenda mgeni wake, kwasababu alishajifunza kuwa moja ya kitu kinachofanya maongezi yawe mazuri na mgeni wako ayafurahie ni kuzungumza vitu anavyovijali mgeni wako.
- Jifunze kuongea na kuzungumza yale anayoyajali zaidi mwenzako, usilete mada zinazokinzana na yale anayoyapenda mwenzako. Kama mpo katika mazungumzo angalia sana namna unavyowasilisha jambo lako, epuka kumtolea mwenzako kauli za mamlaka, au kutoa maelekezo ya moja kwa moja, jitahidi kuwa mwanadiplomasia.
- Ukweli ni kwamba kila mtu unayekutana naye kwenye maisha yako, anajisikia kuwa yeye ni bora zaidi kuliko wewe kwa namna fulani, na anatamani na wewe utambue hilo, hivyo unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unatambua jambo hilo na kuhakikisha hushushi au kumfanya aonekane hana umuhimu kwako.
- Kumbuka kama alivyowahi kusema Emerson, kila mtu anayekutana naye kwenye maisha yake ni bora kwakwe kwa namna fulani, maana yake kuna vitu havijui kutoka kwa mtu huyo, kuna vitu anaweza kuvifanya mwenzako wewe huwezi, hivyo jitahidi kutambua umuhimu wa mtu huyo na uwe tayari kujifunza kutoka kwake.
- Kwenye kuishi kwako na watu, siku zote wafanye watu wajione na kujisikia wao ni bora zaidi, sio mtu anakuja kwako anajiona mnyonge, hana umuhimu, hana heshima. Kama unataka kutengeneza ushawishi wa kudumu kwa watu, wafanye watu wajione na kujisikia wao ni watu muhimu, wao ni watu bora, wao ni watu wanaostahili heshima.
- Mwandishi wa kitabu hiki anasema, njia bora ya kushinda malumbano ni kuyaepuka, usiruhusu malumbano na mtu yeyote, kwasababu ukiingia kwenye malumbano na kuanza kushindana na mtu mwingine au mteja wako, maana yake unampoteza mteja au mtu huyo hata kama umeona umeshinda kwenye malumbano hayo.
- Dale anasisitiza kuwa huwezi kushinda malumbano, maana ukishindwa umeshindwa, na ukishinda umeshindwa pia. Fikiria umeanza malumbano na mtu, ukaongea na ukaona umemshinda kwa kila pointi, utajisikia vizuri kwa muda fulani, lakini fikiria upande wa pili wa uliyeshindana naye, utakuwa umuondolea hadhi na heshima fulani kwenye maisha yake, utamfanya aonekane mnyonge sana, utamfanya aonekane hajui chochote na hana umhimu, hivyo ukaribu utapungua, na kama ni mteja wako hatakuwa na furaha kuja kufanya biashara na wewe.
- Yaepuke malumbano kwa nguvu zako zote, Dale anaema, yaepuke kama nyoka mkali au kama matetemeko ya ardhi, kwasababu utakayemshinda kwenye malumbano hatakuwa na nia njema sana na wewe, manaweza kutengeneza uadui.
- Chuki haiondolewi na chuki bali upendo, ubaya hauondolewi na ubaya bali wema, kutoelewana hakuondolewi na malumbano bali diplomasia, maridhiano, na hali ya uelewa wa upande mwingine. Kitabu cha Biblia kinasema, usishindwe na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.
- Siku zote jitahidi kuzuia hasira zako, kumbuka unaweza kumpima mtu kwa kile kinachomfanya akasirike. Sikiliza kwanza, mpe nafasi ya kuzungumza, mwache amalize mazungumzo yake, usimpinge au kumkatisha mazungumzo yake. Kwa kufanya hivyo utakuwa mtu bora mwenye hekima, na uvumilivu na anayeweza kuchukuliana na mambo ya watu wengine.
- Tengeneza daraja la maelewano, usitengeneze mlima mkubwa wa kutoelewana, angalia maeneo ambayo mnaweza kukubaliana. Ukishamsikiliza mpinzani wako kwenye mazungumzo yake, angalia zaidi pointi ambazo unakubaliana nazo. Usimkatalie na kumpiga mtu moja kwa moja.
- Kuwa mwadilifu, angalia maeneo ambayo umefanya makosa na kiri kufanya makosa hayo, omba msamaha kwa makosa yako, hii itamfanya mpinzani wako apunguze hasira, chuki na pia itaondoa hali ya kujihami kwa mpinzani wako.
- Ahidi kwa mpinzani wako kuwa utafikiria na kufanyia kazi maoni yake, usiseme hivi ili tu kumridhisha mpinzani wako, maanisha kabisa kuwa utayafanyia kazi maoni yake. Hii itamfanya akukubali na aone matumaini makubwa kufanya kazi na wewe, usimwache mpinzani wako aondoke bila suluhisho la maoni yake.
- Unaweza kuwaambia watu mnakosea sana, hampo sawa, lakini fikiria unafikiri watakubaliana na wewe? Mwandishi anasema, kuwaambia watu wamekosea moja kwa moja inawashushia watu hao heshima, umuhimu wao na kuwafanya waonekane hawana akili, epuka kuwahukumu watu kwa yale unayoyaona kwao.
- Unapowashutumu au kuwahukumu watu kuwa wanakosea au wanafanya makosa, inawafanya waanze kujilinda na na kujiandaa kukujibu kwa hasira na kujitetea. Lakini haitasaidia wabadili mawazo yao, hata kama utaleta na kutumia falsafa za Plato au kina Immanuel Kant, kamwe hutaweza kubadili maoni yao, maana umeumiza hisia zao.
- Mwandishi Dale anasema, unapoanza mazungumzo, au unapomjibu mpinzani wako, usianze kwa kusema, ngoja nikuthibitishie jambo hili, au mimi ni mwerevu zaidi, au ngoja niwaambie mambo yatakayobadilisha mitazamo yenu. Ukishaanza na kauli hizo tu, ujue umeshatengeneza vita kwenye mawazo ya wasilikizaji wako, utafanya wanaokusililiza waanza kukupinga hata kabla hujaanza kuongea.
- Dale Carnagie anasema, unajua ilivyo ngumu kubadili fahamu za watu hata katika hali ya mazingira mazuri. Hivyo epuka kufanya mambo kuwa magumu zaidi, jua namna nzuri ya kuanza mazungumzo yako ili watu watamani kukusikiliza bila kukupinga.
- Kama kwenye mazungumzo yako unadhamiria kuwahakikishia watu waamini kitu fulani, usiseme kama unataka kuwasahihisha jambo fulani, tafuta namna nzuri ya kuweka mazungumzo yako ili useme bila wao kugundua.
- Alexander Pope, alifafanua vizuri jambo hili, alisema, watu wanafundishwa kama vile hawafundishwi, na vitu ambavyo havijulikani kama vile vimesahaulika, maana yake namna ya ufundishaji wako usiwe katika hali ya kukosoa, kuhukumu, au kuwafanya watu wajione wajinga, fundisha kama vile unawasilisha mapendekezo kwenye jambo ambalo wanalijua, fundisha kama vile kuna vitu umevisahau unajaribu kuvipendekeza.
- Mwanasayansi maarufu sana duniani, Galileo Galilei aliongeza msisitizo kwa kusema, huwezi kumfundisha binadamu jambo lolote, unachotakiwa kufanya ni kumsaidia ajifunze mwenyewe. Hii ina maana katika kufundisha watu, usifundishe kama vile wewe ndio unajua kila kitu, au usifundishe kama vile unaowafundisha hawana akili.
- Lord Chesterfield wa Uingereza, alimwambia mwanae wa kiume awe mwerevu na mwenye hukima kuliko watu wote kama anaweza, lakini asiwaambie watu hivyo. Maana yake usiwaambie watu kuwa wewe una hekima sana, au wewe ni mwerevu au mjanja sana.
- Mwanafalsafa maarufu duniani, Socretes, alisema moja ya kauli maarufu sana kwenye masuala ya ujuaji na kujifanya unajua sana alisema, anajua jambo moja tu, na jambo hilo ni kwamba hajui chochote. Hivyo basi, acha kujifanya una hekima na busara kuliko Socretes, kamwe usiwahukumu watu na kuwaambia wanakosea, maana hujui.
- Hatakama unajua anayezungumza amekosea, usiende moja kwa moja na kumjibu kuwa amekosea, unachotakiwa kufanya ni wewe kueleza yale unayoyajua, mfano unaweza kuanza kwa kuesema, nafikiri namimi naweza kuchangia jambo hili, sijui kama nipo sawa katika jambo hili ninalochangia, lakini ngoja tuangalia baadhi nukuu fulani.
- Waambie watu kwenye maelezo yako kuwa unaweza kukosea, na mara kwa mara unakosea, ili mjaribu kuangalia ukweli. Hakuna atakaye kupinga kwenye jambo hilo, hata mbingu na ardhi hazitakupigna.
- Hautaingia matatani kwa kukubali kuwa unakosea, bali itamfanya mpinzani wako aache malumbano na pia intamfanya ajisikie nafuu, itamfanya awe na upeo mkubwa wa kufikiri kwa mapana, jambo ambalo litamfanya nayeye akubali kuwa anaweza kukosea au amekosea sehemu fulani.
- Usianzishe malumbano na mteja wako, au mwenza wako, usimwambie mteje wako amekosea, usimwembie mpenzi wako amekosea, tumia zaidi diplomasia kwenye mahusiano yako na watu, tumia zaidi lugha mwanana kujibu mteje wako au mpenzi wako.
- Unapolinda heshima na utu wa mwenzako kwenye mazungumzo yako, unafungua fursa nzuri ya maelewano na ushirikiano kwenye jambo lolote, unawafanya watu wajisijie huru na salama kuwa karibu na wewe au kufanya kazi na wewe.
- Miaka zaidi ya 2200 iliyoipta Yesu Kristo aliwahi kusema, patana na mshitaki wako mapema, kabla hajakupeleka gerezani. Kama unataka hoja yako ipite na isikilizwe jifunze namna bora ya kuwasilisha hoja yako mbele ya watu, kama vile aliyewahi kuwa mfalme wa nchi ya Misri, Mfalme Akhtoi alivyo mshauri mwanaye kwamba kama anataka hoja yake na mawazo yake yapate kibali, inabidi ajue diplomasia, ajue kuwasilisha hoja yake kwa njia ya diplomasia.
- Mwanamapinduzi wa haki za binadamu, Dr. Martin Luther King, aliwahi kuulizwa swali namna anavyowachukulia watu, King alisema, anawajaji watu kulingana na kanuni zao wenyewe na sio kanuni zake, maana yake hatumii mitazamo yake na kuwahukumu watu, anawahukumu kwa mitazamo yao wenyewe.
- Kuna wakati kukiri kosa ulilofanya kunapunguza hasira za mtu anayetaka kukushitaki au kukuadhibu. Mfano, kama umekamatwa na polisi kwa kukiuka sheria za barabarani unatakiwa kukiri tu kosa lako, usianze kubishana na polisi maana yeye anajua na ana ushahidi umekiuka sheria za barabarani, hivyo ukishindana naye yeye atataka kuonekana mkubwa zaidi hivyo huwezi kushinda, atakushinda na utapewa adhabu.
- Ni vizuri kukiri makosa yako mapema kabla ya anayetaka kuyasema, waambie ni kweli nimekosea, ni kosa lako, ni wewe muhusika, ni kweli nastahili adhabu kulingana na kosa nililofanya, laikini pia hapo hapo unaweza kuomba kama kuna namna anaweza kukusamehe, maana ukishampa mtu mamlaka ya kukuadhibu, mpe pia na mamlaka ya kukusamehe.
- Mara nyingi utapoteza pale unapojaribu kujitetea na kujisafisha, kama umefanya kosa, kiri kosa, hii itamfanya mpinzani wako akose nguvu juu yako. Kwa kujitetea na kujilinda unaweza kupoteza vingi kuliko kupata, kuwa mkweli na pia kuwa mwadilifu kwenye maisha yako.
- Kuna mfano mzuri sana umetolewa kwenye kitabu hiki kuhusu mashindano kati ya upepo na jua, nani anaweza kumvua bindamu koti, upepo ulisema mimi naweza na nina nguvu, nitamvua binadamu koti lake. Mashindano yakaanza, upepo ukaanza, ukavuma kwa nguvu sana, ili koti litoke kwenye mwili wa binadamu, lakini jinsi upepo ulivyokuwa unatumia nguvu kubwa ndivyo koti lilivyong’ang’ania kwenye mwili wa binadamu, kwa hivyo upepo ukashindwa kabisa kumvua binadamu koti lake.
- Ikafika zamu ya jua, kumvua binadamu koti lake, cha kwanza alichofanya jua ni kutabasamu kwa kumuangalia binadamu, kisha jua likaongezeka, joto likapanda, binadamu mwenyewe kwa mikono yake akavua koti lake kwasababu ya joto lililoletwa na jua. Hapa tunajifunza kuwa, namana ya kuwafanya watu wachukue hatua na kufanya unayoyataka sio kwa kutumia mabavu, nguvu na hasira, wakati mwingine unahitaji kutabasamu tu, na mtu atapendezwa na wewe kisha atafanya unachokitaka bila mabavu.
- Njia nzuri ya kuwafanya watu wachukue hatua au kufanya jambo fulani kwenye maisha yao ni kwa kufanya jambo hilo liwe rafiki kwao, upole, unyenyekevu na heshima. Usiwafokee watu ili wafanye jambo fulani, tumia njia rafiki ambazo hazitaleta madharau.
- Kama unaongea na watu, usianze mazungumuzo na mambo ambayo mnatofautiana, anza na yale unayoona mnaelewana, endelea kusisitiza zaidi yale ambayo unaona kabisa mnaweza kuyafanya pamoja na wote mnakubaliana nayo. Tofauti zenu wekeni pembeni, wekeza nguvu kwenye yale yatakayokupa matokeo.
- Fikiria unafundisha na wanafunzi wako wakakukataa mwanzoni kabisa mwa somo lako, au fikiria una biashara na wateja wakakukataa mwanzoni kabisa mwa biashara yako au fikiria unataka mahusiano bora na mpenzi wako akakukataa mwanzoni kabisa. Itakugharimu nguvu na hekima za malaika ili kubadilisha mitazamo waliyo nayo watu waliokukataa. Hivyo basi, usifanya mambo yakawa magumu mwanzoni mwa kazi zako, biashara yako, au mahusiano yako, angalia mambo mnayokubaliana ndio yawe nguzo ya mafunzo, biashara na hata mahusiano yenu.
- Wafanye watu waseme ndio kwenye mazungumzo yako, usifanye watu wakasema hapana, moja ya watu wenye hekima sana na mwanafaslafa Socretes, aliwahi kusema, kwenye mahusiano yako na watu, wafanye wasema ndio mwanzoni mwa mazungumzo yako.
- Wachina ni jamii iliyojifunza sana masuala ya asili ya binadamu kwa zaidi ya miaka 5000, hivyo wamejikusanyia hekima na mithali nyingi zenye manufaa kwa binadamu hasa kwenye masuala ya mahusiano na watu wengine; moja ya mithali yao inasema, anayepiga makasia taratibu atafika mbali au kama ilivyoandikwa. “He who treads softly goes far.” Maana yake, anayetumia nguvu nyingi kwenye mambo yake hafiki mbali.
- Kwenye maisha hata marafiki zetu, watapenda sana endapo tutazungumzia mafanikio yao kuliko mafanikio yetu wenyewe. Maana yake watu hawapendezwi sana na wewe kuelezea mafanikio yako kwao, hawapendi wewe uwazidi, wanatamani uelezee yale wao waliyofanikiwa.
- Moja ya mwanafaslsafa wa Ufaransa aliyeitwa La Rochefoucauld, aliwahi kusema, kama unataka maadui, fanikiwa kuliko marafiki zako, lakini kama unataka marafiki, waache marafiki zako wafanikiwe zaidi yako. Hii ni kauli ngumu sana kuiamini, lakini tunaweza kushuhudia mengi kwenye jamii yetu hata kwenye mahusiano yetu na watu wetu wa karibu.
- Marafiki zetu wanapofanikiwa, wanajisikia wao ni watu muhimu na wa maana sana, lakini pale tunapofanikiwa kuwazidi marafiki zetu, wengi wao wanajiona wanyonge, na kuona kama hawana thamani, hali hii inapunguza ukaribu, inatengeneza wivu, hatimae urafiki unaweza kufa kabisa.
- Mwandishi Dale anasema, ili uweze kutunza urafiki na mahusiano mazuri na watu, epuka kutangaza utajiri au mafanikio yako kwa marafiki zako, pia wasifie marafiki zako pale wanapokamilisha malengo yao, unaweza kuonyesha kuvutiwa na mazungumzo yao pale wanapoelezea mafanikio yao kwako.
- Utazungumza mafanikio yako tu pale ambao wamekuuliza kufanya hivyo, lakini kama hawajakuuliza usizungumzie kuhusu mambo uliyofanikiwa kwenye maisha yako, ukiwa muongeaji sana wa kujisifia mafanikio yako mbele ya marafiki zako, wengi hawatakupenda, pia wanaweza hata kukutenga.
- Kama unataka ufanisi kazini au kwenye biashara yako, washirikishe wafanyakazi wazo lako, walifanye liwe kama wazo lao na sio la kwako peke yako. Kama mgurugenzi au bosi wa kampuni unaweza kuwaulize wafanyakazi wako, ni kitu gani wanahitaji akifanye kama bosi ili kuongeza ufanisi kazini, bosi atakachoambiwa anatakiwa akifanye kwa silimia zote, kisha bosi awaulize wafanyakazi wake ni kitu gani ategemee kutoka kwao ili waongeze ufanisi, hapo inatakiwa kila kitu kiandikwe vizuri sana, baada ya wafanyakazi kusema watakachofanya basi hapo hilo linakuwa ni wazo la wote, na wataonyesha ufanisi.
- Madhara ya kulifanya wazo liwe lako pekee, inapunguza uwajibikaji na watu wataona wao hawahusiki sana na hilo wazo lako, hivyo hawatajitoa kikamilifu kilifanyia kazi wazo hilo, lakini kama wazo wamelifanya kuwa lao, watajitoa kulifanyia kazi ili lifanyikiwe kwa viwangu vya juu.
- Karne zaidi ya 25 zilizopita, Lao-tse, Mchina mwenye hekima alisema jambo muhimu sana ambalo msomaji wa kitabu hiki hapaswi kukosa kulifahamu, alisema, unajua kwanini mito na bahari zinapokea maelfu ya mifereji ya maji kutoka milimani, jibu ni kwamba ni kwasababu mito na bahari zipo chini ya milima ndio maana maji yote ya mifereji na mito huishia kwenye mito na bahari. Maana yake uwezo wako wa kutawala, kuwa mkuu na mwenye mafanikio unakuja tu pale unapokubali kuwa chini, kuwa mnyenyekevu, mtu ambaye hutaki mashindano.
- Lao-tse anasisitiza kama unataka kuwa mbele ya watu, inabidi ukubali kuwa nyuma ya watu, kama unataka kuwa juu inabidi ukubali kuwa chini. Na hata ikitokea ukapewa nafasi ya kuwa mbele au juu zaidi ya wengine, Lao-tse anasema hutawaumiza wala kuwagandamiza, pia watu hawatajali sana.
- Sema kuhusu makosa yako kabla ya kukosoa wengine, watu wanajichukulia wao wenyewe kwa uzito kuliko wanavyokuchukulia wewe. Hvyo usijaribu kubishana nao, wala kuongea vitu vitakavyoshusha heshima yao.
- Huna haki ya kusema au kufanya chochote kitakacho shusha hadhi ya mtu mwingine, cha muhimu sio kile unachofikiri wewe kuhusu mtu huyo, bali kile anachofikiria mwenyewe.
- Usianike makosa ya watu, jaribu kificha makosa yao, maana yake jaribu kulinda heshima yao. Kama tunataka watu wabadilike tutumie zaidi zawadi na pongezi kuliko adhabu. Mfano, tunapomfundisha mbwa tabia mpya hatumpigi, tunampa nyama maana ndio anachokipenda. Hivyo hivyo kwa binadamu, tusitumie fimbo, tutumie namna nyingine kama zawadi.
- Sifa ni kama nuru usoni pa mtu, kama mtu amefanya jambo zuri anahitaji kusifiwa hadharani na sio kusubiria hadi anapokosea ndio tunatokea na kuanza kutoa maoni yetu ambayo mengi ni ya ukosoaji, wivu, chuki na ujuaji ambayo hayamsaidii sana aliyekosea.
- Saikolojia imebaini kuwa mtu anaposifiwa anapojitahidi kufanya jambo fulani uwezekano ni mkubwa sana wa mtu yule kuweka bidii sana ili awe bora na afanikiwe zaidi, lakini pia ukosoaji hauleti matokeo mazuri sana kwa mtu.
- Kama unataka mtu afanye mazuri mpe jina zuri, kama ilivyo ukitaka kumua mbwa mpe jina baya. William Shakespear aliwahi kusema, kama huna tabia njema au maadili, jifanye kama mwema na endapo utafanya jambo hilo jema, utapongezwa mwisho wa siku utakuwa mtu mwenye maadili.
- Mfano, kama mtoto wako anataka kuwa daktari utampa jina la dakatari, kisha utamwambia ili uwe daktari mzuri lazima asome kwa bidi afaulu masomo yake ya biolojia, kemia na fizikia. Hii itamfanya ajitume sana, hii inaweza kutumika kazini, kwenye biashara na mahusiano.
- Hata kama rafiki yako amekosea, usilifanye alione kosa lake ni gumu kusahihishwa, au changamoto yake ni ngumu kupatiwa ufumbuzi, msaidie aone changamoto yake ni rahisi kupatiwa suluhisho. Fanya hivyo kwa mwenza wako, watoto wako, na wafanyakazi wako pale wanapokosea.
- Mfanye mtu afurahie kufanya kile ulichopendekeza, usifanye mambo yawe magumu kwa mtu mwingine.
- Mambo tuliyojifunza kwenye kitabu hiki yatafanya kazi tu pale mtumiaji atakapomaanisha, kutoka moyoni mwake, sio mbinu za ujanja ujanja tu, ni namna tunavyotakiwa kuchukulina kama binadamu.
- Vigezo vinavyokupa furaha wewe sio lazima viewe ndio vigezo hivyo kwa mtu mwingine. Ni muhimu kutambua jambo hili hasa kwenye eneo la mahusiano, unaweza kuwa unafurahia mahusiano uliyonayo lakini mwenzako hana furaha kama wewe.
- Kwenye kitabu chake kinachoitwa “Growing Together in a Family”, Leland Foster Wood, ameandika, mafanikio kwenye maisha ya ndoa sio suala la kutafuta mtu sahihi, ni suala la kuwa mtu sahihi. Maana yake, kuwa mtu bora na sahihi kwa mwenzako, kabla ya kudai mwenzako ndio awe sahihi kwako.
- Kuna namna tunaishi maisha yetu kinafiki sana, yana unakuwa mwema kwa mgeni ambaye humjui, lakini unakuwa katili, jeuri na usiye mwema kwa mpenzi wako au mwenza wako. Wema uanzie nyumbani kwako, kwa watu wako wa karibu kabla hujaupeleka sehemu nyingine duniani.
- Kama vile Doroth Dix alivyonukulikwa akisema, tunashangaza sana lakini ndio ukweli ulivyo, sisi ni watu pekee ambao tunaongea maneno mabaya, matusi, na maneno ya kuumiza kwa watu wa nyumbani mwetu.
200.Dhamiria kuweka kwenye matendo haya uliyojifunza kwenye kitabu hiki, mwandishi anasema, utaona kama miujiza kwenye maisha yako, maana utapata matokeo mazuri.
MWISHO…
Hiki ni moja ya vitabu bora sana kuwahi kuvizoma kwenye maisha yangu. Kitabu hiki kimesheheni mifano na tafiti nyingi za kweli ambazo majibu yake ni halisi, ni kitabu bora sana hasa kwenye kujenga urafiki, mahusiano na ushawishi kwa watu. Ni kitabu kinachomfaa kila binadamu. Usiache kumshirikisha na rafiki yako uchambuzi wa kitabu hiki.
Hillary Mrosso_02.02.2023
One response to “Kitabu; How To Win Friends And Influence People”
[…] Soma zaidi: Kitabu: How to Win Friends and Influence People […]