Uchambuzi Wa Kitabu: The Monk Who Sold His Ferrari


Kitabu: The Monk Who Sold His Ferrari
Mwandishi: Robin Sharma
Mchambuzi: Hillary Mrosso
Simu: +255 683 862 481

Utangulizi

Habari ndugu msomaji wa uchambuzi wa kitabu hiki maarufu cha The Monk who sold his Ferarri, hiki ni moja ya kitabu maarufu sana duniani, umaarufu wake umefanya kitabu hiki kuuzwa na kusomwa na watu wengi, hii ni kutokana na uandishi mzuri na visa vya kusisimua ambavyo vinaweza kubadili maisha yako, kama vilivyobadili maisha ya Julian ambaye ndie muhusika mkuu aliyezungumziwa zaidi katika kitabu hiki. Mwandishi Robin Sharma ameandika mambo muhimu sana ya kuboresha maisha yetu, ameonyesha kuwa inawezekana kuishi maisha ya ndoto zetu, maisha ya utoshelevu na maisha bora. Karibu katika uchambuzi wa kitabu hiki, kwa ufupi nimekuandalia kwa lugha nyepesi kabisa mambo 100 niliyojifunza katika kitabu hiki bora kabisa.

 1. Kila tunachopitia kwenye maisha yetu kiwe kizuri au kiwe kibaya vyote vinatakiwa kuchukuliwa kama mafunzo muhimu ya kuboresha maisha yetu.
 2. Mwandishi anakiri kuwa kushindwa kwa namna yoyote ile kwenye maisha kiroho, kimwili, kiuchumi, au kitaaluma ni muhimu sana katika kutukuza na kutuongeza katika ngazi fulani.
 3. Hutakiwi kujutia yaliyopita, kama yalitokea kwenye maisha yako basi yachukulie kama zawadi na kama mafunzo muhimu ya kukukomaza kiimani, kiroho na kimwili, usijutie, badala yake yafurahie na yatumie kama nyenzo ya kufanya kwa uboreshe sehemu nyingine kwenye maisha yako.
 4. Unawezaje kusema unajali wengine wakati hwezi kujijali wewe mwenyewe? Mwandishi anasema onyesha kujali kwenye maisha yako mwenyewe kwa kuwa na uwezo wa kutawala na kuzuia mambo hasi yasiingie kwenye maisha yako.
 5. Unawezaje kufanya mazuri wakati wewe mwenyewe hujisikii vizuri? Siwezi kupenda kama siweze kujipenda mwenyewe, ni muhimu sana kipimo cha kweli kikawa ni wewe mwenyewe na miendendo yako.
 6. Mwandishi anasema kama kuna uwekezaji bora unaoweza kufanya kwenye maisha yako ni kuwekeza kwako mwenyewe kwanza. Maana sio kwamba uwekezaji huo utakufanya uwe bora tu, bali utawafanya na wote wanaokuzunguka kuwa bora.
 7. Watu wenye furaha na kuwa na maisha mazuri yenye utimilifu sio watu tofauti na wewe, sio watu walioumbwa tafauti na wewe, ni watu wenye damu na yama kama sisi na wametoka kwenye chanzo kimoja pamoja na sisi.
 8. Kila mabadiliko mazuri unayoyataka kwenye maisha yako yanawezekana kabisa, hakuna kisichowezekana, unaweza kuamua kuboresha maisha yako yakawa kwa viwango vya ubora unaotaka.
 9. Mwandishi wa kitabu hiki anasema mtu wa kawaida anaweza kuwa na mawazo zaidi ya 1000 kwenye ufahamu wake, na cha kushangaza ni kwamba 95% ya mawazo hayo ni ambayo aliyawaza siku ya jana.
 10. Jinsi tunavyofikiri inatokana na tabia tulizo nazo, tabia zetu zina msukumo mkubwa sana wa namna tunavyofikiri kila wakati.
 11. Kuna uwezo mkubwa sana katika fahamu zetu, mwandishi anasema hata mtu bora sana katika kufikiri huwa anatumia ailimia chache sana za uwezo wake wote alio nao.
 12. Kinachotutofautisha kama binadamu ni uwezo wetu wa kuchakata taarifa na kutumia uwezo ulio ndani yetu kufanya makubwa kwenye maisha yetu.
 13. Unapojitoa vya kutosha katika kuboresha utu wako wa ndani, unafanya maisha yako kutoka kuwa ya kawaida na kuyafanya kuwa ya viwango vikubwa sana. Hakuna kitakachokupa uhalisia kwa asilimia 100, hapa duniani rafiki yako wa dhati uliye naye sasa anaweza kuwa adui yako mkubwa baadaye.
 14. Uwezo wako wa kusema ninaweza ni wa muhimu sana kuliko IQ yako, utaweza pale utakapoamua kuwa unaweza na kufanyia kazi maamuzi yako.
 15. Haijalishi ni kitu gani kimetokea kwenye maisha yako, ni wewe tu peke yako ndio unaweza kuamua upokee vipi kile kilichokuja kwenye maisha yako.
 16. Amua kuchagua upande chanya kwenye kila changamoto inayokuja kwenye maisha yako, ukiweza kuchagua upande chanya hata kama mambo yamekuwa magumu, utakuwa umejiweka kwenye upande wa mafanikio na usalama zaidi kwenye maisha yako.
 17. Wachina wanasema neno changamoto au matatizo au majanga ni fursa, hivyo wao wanatazama changamoto na majanga yanayokuja kwenye maisha yao kama fursa ya kuboresha maisha yao.
 18. Kama Ribon Sharma anavyosema, hakuna makosa kwenye safari ya maisha, ni masomo tu, na kupata uzoefu, hivyo badili namna unavyotazama mambo yaliyopo kwenye maisha yako, ona kila kilichopo kwenye maisha yako ni nafasi ya kufanya vizuri na kuwa mtu bora.
 19. Tumia maumivu, majanga, changamoto, mikosi na makosa uliyoyafanya, au yaliyopo kwenye maisha yako kwa faida yako mwenyewe, yatumie hayo ili kwa kuyatatua yakufanye uwe moja binadamu bora kabisa kuwa hikushi hapa duniani.
 20. Unawezaje kufurahia kilele cha mafanikio kama hujui shida za kukaa chini, huwezi kufurahia kufikia kilele cha mlima mrefu bila kujua shida ulizopata ukiwa katika bonde chini ya mlima.
 21. Unawezaje kufanya mazuri kama huyajui mabaya? Usiyahukumu mambo kwa haraka kama ni mabaya au ni mazuri, mwandishi anasema, yachukulie mambo yote kama sehemu ya kujifunza ili uborehe maisha yako.
 22. Mwandishi wa kitabu hiki anataka tuache kuwa watumwa wa mambo yaliyopita, anatakwa tutazame upya changamoto na magumu tunayokutana nayo kama mafunzo na darasa muhimu la kuimarika na kuwa mtu mwenye maadili bora kabisa.
 23. Kuanzia leo na kuendelea, achana na mambo yaliyopita, unaweza kutengeneza historia bora yenye kumbukumbu nzuri zaidi kwa siku zilizobakia za kuishi maisha yako hapa duniani, anza leo.
 24. Kama vile Malaka Chand alivyowahi kusema, aliona mbegu ya fursa kila alipokuwa kwenye maumivu au katika nyakati za maumivu.
 25. Unapovutiwa na kusudi kubwa la maisha yako, inakufanya kufanya mambo kwa viwango vikubwa, kuboresha maisha yako na maamuzi yako ili vyote vikusaidie kutimiza kusudi la kuumbwa kwako.
 26. Mafanikio ya nje yanatakiwa yawe yametokana na mafanilio ya ndani yako, maana yake fanikiwa sana ndani yako kabla ya nje.
 27. Ufahamu wako unaweza kuwa mtumwa wako mzuri sana, lakini pia inaweza kuwa kiongozi wako katili sana, kama umekuwa ukifikiri na kuwaza vitu hasi ni kwasababu hukuwa na muda wa kutosha kulinda ufahamu wako usiingiliwe na kutawaliwa na vitu hasi.
 28. Gharama ya kuwa mtu mkuu ni kuwajibika na kila wazo linalokuja kwenye ufahamu wako, mwandishi anasema fungua milango ya fahamu zako ili mawazo bora, mawazo chanya yaingie kwenye fahamu zako.
 29. Mipaka iliyopo kwenye maisha yako ni ile uliyoitengeneza mwenyewe, hakuna aliyekuwekea. Kama unataka kuishi maisha ya maana na yenye amani lazima ufikiri na kufanya mambo yenye maana na kuwa na mawazo ya aina hiyo.
 30. Jitahidi kuweka umakini wako wote kwenye mambo unayo yafanya, usitawanye umakini wako, kwa kufanya hivyo utakuwa mtu wa maana na utazalisha vitu vikubwa kwa muda mchache.
 31. Angalia kile kitu ambacho ukikifanya utakuwa kama umepata uhai kwenye maisha yako, angalia kile unachokipenda sana ndio ukifanya na ukipe umuhimu wako wote.
 32. Usiwekeze nguvu zako kwenye hofu na mashaka, hofu na mashaka zinaondoa sana nguvu na umakini wako, amua kuweka nguvu zako kwenye kufanya vitu vyenye tija.
 33. Jitie ujasiri kufanyia kazi ndoto zako, ili uziishi ndoto zako na maono yako unahitaji sana ujasiri, maana hutaweza kufikia kilele cha mafanikio ukiwa mwenye hofu, woga, hasira, uchungu au dhaifu, unahitaji sana ujasiri na ukakamavu.
 34. Kuna watu wanasema hawana muda wa kuboresha mawazo yao, mwandishi anasema mtu anayesema hana muda wa kuboresha mawazo yake ni kama mtu anayesema hana muda wa kuweka gari yake mafuta wakati anataka kuendelea na safari.
 35. Kila siku ya maisha yako, haijalishi hiyo siku upo bize kiasi gani, kumbuka kupumzika na kupitia mawazo yako, pitia siku yako, hii itakufanya uongeze umakini kwenye unayoyafanya na kuyawaza.
 36. Kuna nguvu kubwa sana ipo katika ukimya, unapokaa kwenye ukimya na ukatuliza ufahamu wako, utapata nguvu sana ya kukusaidia kufokasi. Unaweza kujifunza kufanya tahajudi au meditation hii inasaidia sana kukomaza umakini, na kuimarisha ufahamu wetu.
 37. Ukiwa na ufahamu dhaifu hata matendo yako yatakuwa dhaifu sana, fanya ufahamu weko kuwa imara kwa kuongeza nidhamu kwenye maisha yako na fahamu zako.
 38. Kama kuna utupu kwenye maisha yako ni kwasababu kuna utupu kwenye mawazo yako, unatakiwa kuwa na picha ya kile unachokitaka kwenye mawazo yako ili kitokee kwenye maisha yako.
 39. Kamwe, usijaribu kupima maisha yako na thamani yako kwa utajiri alio nao mtu, thamani yako hailinganishwi na utajiri, fedha au mali yoyote ile, thamani yako ni kubwa kuliko unavyodhani.
 40. Usishushe maisha yako, usithaminishe maisha yako na vitu, usithaminishe utu wako kwa vitu, umeumbwa na ukuu ndani yako, na mwenye dira yote ya maisha yako ni Mungu, mpe nafasi akusaidia kutumia vipawa vilivyoko ndani yako kuwa mtu mkuu.
 41. Hakuna kitu cha maana utakachopata kwa kuwafanya watu wengine kuwa duni, sio umaarufu wala ufahari kujiona wewe ni bora na una thamani kuliko watu wengine.
 42. Usiharibu maisha ya watu wengine ili uborehe maisha yako binafsi, mbingu zitakukataa, na malaika hawatakuwa upande wako, utakosa furaha kwenye maisha yako kwa kuwa mtu wa dhuluma.
 43. Uchovu na kuchoka vinatengenezwa na fahamu zetu, mara nyingi uchovu unawatawala wale ambao hawana cha kufanya, wamezikatia tamaa ndoto zao.
 44. Siku zote ishi kwenye wakati uliopo, fanya kwa ubora kile kilichopo mikononi mwako kwa wakati huo, huwezi kuboresha kilichopita, lakini unaweza kuboresha maisha yako ya baadaye kwa kuboresha leo yako.
 45. Ukiwa na muda wa kutosha wa kujifunza kuhusu wewe mwenyewe utakuwa mtu bora sana, maana yake usihangaike kutaka kuwaelewa watu wengine, jitahidi ujielewe wewe mwenyewe kwanza, hii ndio hekima.
 46. Hakuna majanga au hatari utakayoipata kwa kutaka kujifunza na kujielewa wewe mwenyewe, badala yake utakuwa na muda mwingi wa kutengeneza maisha unayoyataka na yatakayoendana na upekee wako.
 47. Mwandishi wa kitabu hiki anasema hutapata furaha kwa kukaa tu bila kufanya chochote kwenye maisha yako, hutapata furaha kwa kulala sana, furaha inakuja kwa kufanyia kazi kusudi la kuwepo kwako hapa duniani, furaha ya kweli inakuja kwa kufanya kazi.
 48. Jifunze bila kuchoka, bila kukata tamaa, jifunza kwa watu wakuu na wenye mafanikio makubwa, kama unawaona waliofanikiwa na kufika mbali ni kwasababu walijifunza kutoka kwa watu waliofika mbali na wenye mafanikio.
 49. Tenga muda wa kuandika mipango yako na malengo yako unayotaka kuyafikia, hakuna anayelenga shabaha asiyoiweka, andika malengo yako na yapitie kila mara kuona mwenendo wa kuyafikia upoje.
 50. Mwandishi Robin Sharma, anasisitiza sana tutumie nguvu kubwa kujigundua wenyewe, tumia nguvu kubwa kwako mwenyewe, itakusaidia sana kuboreha maisha yako.
 51. Jitahidi kila siku ufanye mambo muhimu na yenye tija kwenye siku yako, usifanya mambo ambayo yatakurudisha nyuma, wekeza kwenye mambo muhimu hata kama ni machache.
 52. Ili uongeze ufanisi kwenye siku yako usiweke malengo ambayo hayana muda, weka muda kwenye malengo yako, sema nitafanya jambo hili kwa siku 10, nitaandika makala kwa siku 100, nitasoma kitabu hiki kwa siku 5 nk.
 53. Ni vizuri ukawa na kitabu chako utakachoandika malengo yako ya kifedha, kifamilia, kiroho, kuimarisha mwili nk, hii itakuwa ni mwongozo mzuri wa kurejea kila wakati.
 54. Unaweza hata kuambatanisha na picha ya namna unataka kufikia malengo yako, weka picha ambazo zitakusukuma kufanyia kazi malengo yako kila siku.
 55. Namna ya kupanda tabia mpya kwenye maisha yako ni kutumia nguvu nyingi na umakini wako wote kwenye kuifanyia kazi tabia mpya, kiasi kwamba ile tabia ambayo huitaki ikose ushirikiano na ipotee yenyewe kwenye maisha yako.
 56. Usifanye kitu chochote ili mradi tu unakifanya, kifanya kitu hicho kwasababu ni kitu sahihi kufanyika. Onyesha na kuwa na shauku kila mara unapofanyia kazi ndoto zako na malengo yako.
 57. Hakikisha unafurahia safari yako ya mafanikio, maana yake usisahau kuishi wakati unapambania ndoto zako na malengo yako, uwe unafurahia kila hatua, hii itaongeza kujituma na kuwajibika zaidi.
 58. Mwanafalsafa Epictatus alwahi kusema, hakuna mtu aliye huru ambaye hana uthibiti kwenye maisha yake. Maana yake huwezi kusema upo huru au una uhuru kama umekosa uthibiti kwenye maisha yako, kama umeshindwa kuthibiti mambo kwenye maisha yako huwezi kuwa huru.
 59. Unapokazana kuboresha ufahamu wako, kazana pia kuboresha hali yako ya kiroho, ili uwe na nguvu za kukusaidia kustahimili changamoto.
 60. Jisukume kila siku kuboreha ufahamu wako na mwili wako, rutubisha roho yako, fanya vitu unavyovihofia, ishi kwa furaha na kufanya mambo yako kwa shauku na furaha kubwa.
 61. Jitahidi kuondoka kwenye comfort zone, jiweke siku zote kwenye sehemu ambayo itakufanya ujisukume na uende mbele zaidi, ondoka kwenye mazoea.
 62. Kuwa mtu ambaye kila mara unatamani kuwa, kuwa mtu wa ndoto yako, fanya yale uliyotamani kuyafanya kwenye maisha yako, jikague, jiboreshe na endelea mbele zaidi.
 63. Jiandae kila wakati, maana bahati huja na kuwapata waliojiandaa, nenda hatua za ziada zitakazokudai utumie nguvu zilizolala ndani yako.
 64. Ainisha mambo yanayokurudisha nyuma, kama unaogopa kuongea mbele za watu, au unaogopa kuingia kwenye mahusiano mapya, au huna mitazamo chanya? Zipitie hizo changamoto na uzifanyie mpango wa kuondokana nazo mapema sana.
 65. Ukizishinda hofu zako, umeshinda maisha yako, maana yake ukipata ushindi kwenye mawazo umepata ushindi kwenye maisha yako. Ondoka kwenye hofu haraka sana.
 66. Usiendeshe maisha yako bila tathimini ya kina, hata kama umetingwa na mambo mengi kiasi gani, chukua muda ndani ya siku yako kufanya tathimini na kupitia siku yako yote.
 67. Tenga muda wa kufanya mazoezi ili mwili wako uwe katika muonekano mzuri na wenye afya, ukiwa na mwili dhaifu hutaweza kutimiza ndoto zako, imarisha afya ya mwili wako.
 68. Katika wiki moja kuna masaa 168, inashauriwa uchukue masaa 5 kati ya hayo ufanye kazi za kuushughulisha mwili, kama vile kutembea, kulima, kuogelea, kutegeneza bustani, kucheza mpira, kukimbia nk
 69. Kama unaweza kujifunza kufanya tahajudi kila siku asubuhi ni nzuri sana kwa ajili ya kutufanya kuongeza umakini na ufanisi kwenye kazi zetu, jifunze meditation au tahajudi.
 70. Jitahidi kula vyakula vilivyo hai, hapa namaanisha vyakula kama matunda, mboga mboga, nk, vyakula ambavyo vinaiva na kukomaa kutokana na mwanga wa jua, udogo na hewa ya kutosha. Mwandishi anasema ukiangalia wanyama wanaokula majani na matunda ni wanyama wenye afya na nguvu sana na wanaishi miaka mingi mfano, sokwe, tembo, nyati nk.
 71. Usile vyakula ambavyo vitachukua muda mrefu kumeng’enywa, vyakula vigumu kumengenywa huwa vinatumia nguvu kubwa ya mwili katika mchakato wa umeng’enyaji, mfano nyama.
 72. Kuwa msomaji, soma vitabu bora ili uwe na mawazo bora, mwili wako huwa na misuli imara kwa kuwa unafanya mazoezi, hivyo na fahamu zetu zitakuwa imara kwa kusoma na kuzizoesha kusoma vitabu na mawazo mapya bora.
 73. Ipe akili yako vitu bora na mawazo bora ya kutafakari, utaweza kufanya hivyo kwa kuwa msomaji wa vitabu na maandiko bora. Mfano kitabu cha Think and Grow Rich, ni kitabu bora sana cha kusoma kwa bindamu yoyote.
 74. Muda wa kuwa peke yako na kujitafakari na kujifanyia tathimini itakufanya ujue mambo ya kuboresha kwenye maisha yako, bila tathimini ya kina hutajua mambo ya kuboresha kwenye maisha yako. Namna nzuri ya kuiboresha kesho ni kujua ni kitu gani umefanya vibaya leo, mana yake ukiiboresha leo utakuwa umeiboresha kesho yako.
 75. Furaha inakuja kutokana na kuamua vizuri, na kuamua vizuri kunatokana na uzoefu, na uzoefu unatokana na maamuzi mbaya uliyowahi kufanya siku za nyuma.
 76. Pata muda wa kutembea kwenye mwanga na kwenye jua, hii itasaidia sana kuhuisha nafsi na roho yako, ndio maana nchi za Mashariki ya mbali huabudu jua kwasababu jua hufanya mimea kuchanua na kuzaa, hivyo jua linaweza kukufanya roho yako kuchanua pia.
 77. Usisahau umuhimu wa kupata usingizi mzuri, cha muhimu sio wingi wa masaa ya kulala bali ni ubora wa usingizi unaopata. Maana yake unaweza kulala masaa macheche ukapata usingizi bora kuliko kulala masaa mengi yenye usumbufu na ukakosa usingizi bora.
 78. Hakikisha unakula mapema kabla ya kwenda kulala wakati wa usiku, mfano kama unalala saa 4 usiku, ikifika saa 2 usiku unatakiwa uwe umeshakula, usile usiku sana, usile na kwenda kulala muda huo, hii inapunguza ubora wa usingizi wako.
 79. Kabla ya kwnda kulala usingalie habari, usingalia movie, usingalie TV, wala usinywe kahawa au vinywaji ambavyo vinakata usingizi, unaweza kusikiliza miziki laini ili ulale mapema ulale ukiwa umerelax.
 80. Kwenye sala na maombi yako mbele za Mungu yanatakiwa yawe ni maombi yaliyojaa shukrani zaidi, shukuru kwa kila kilichotokea kwenye maisha yako, mshukuru sana Muumba wako.
 81. Kuwa na muda wa kucheka, mwandishi mahiri William James aliwahi kusema, hatucheki kwasababu tunafuraha, tunafuraha ndio maana tunacheka, hivyo anza leo kucheka.
 82. Kuna watu ni wagumu sana kucheka, wengine wanadhani ni sifa, sio sifa unajinyima furaha kwenye nafsi yako, hivyo cheka kwa ajili ya kuburudisha na kuhusiha nafsi yako.
 83. Jiulize kila siku, kama leo ndio siku yangu ya mwisho hapa duniani ningefanya nini? Hili swali litakufanya uongeze umakini na ufanye kila kitu kwa kujituma sana na kwa ubora mkubwa.
 84. Kuwa na wakati wa kusikiliza miziki laini, hii itakufanya ubongo wako urelax na kukuletea masuluhisho mengi kwenye maisha yako, punguza kukaza kichwa kila wakati, uwe na muda wa kuituliza akili yako na kukubaliana na mambo ambayo yapo nje ya uwezo wako.
 85. Kila siku jisemee mimi nina nguvu, mimi ni jasiri, jisemee maneno ya kukuinua kila wakati, acha kujisemea maneno dhaifu na ya kinyonge, usijiongelee unyonge kwenye maisha yako.
 86. Maneno yana nguvu hata kama ni ya kuongea au ni kuandikwa, kuwa makini na maneno unayoongea yasije yakakukwamisha, jitamkie maneno ya baraka, ushindi na mafanikio.
 87. Hakuna atakayekutengenezea ujasiri usipojitengenezea mwenyewe, hakuna atakayekupa furaha usipojipa mwenyewe, amua kuwa msimamizi wa maisha yako kwa asilimia 100.
 88. Usijitazame kinyonge, watu watakutazama hivyo pia, jipe nafasi ya kuwa bora kila siku, tembea kwa kujiamini, fanya mambo yako kwa kujiamini na watu watakuamini pia.
 89. Punguza mahitaji yako, usipopunguza mahitaji yako hautatosheka kamwe, kila mara utajikuta kama mcheza kamari, hutosheki kabisa, unahitaji zaidi na zaidi, na hiyo itakufanya ukose furaha kwenye maisha yako.
 90. Jitahidi kuwa jasiri na kuwa hodari, dunia ipo upande wa watu majasiri na walio hodari, hakuna dunia ya watu dhaifu na waoga, kuwa jasiri rohoni na mwilini, itakusaidia sana kutembea kwenye hii dunia.
 91. Usipambane na watu ili uwe bora, pambana na wewe mwenyewe ili uwe bora, maana yake usishindane na watu, shindana na wewe mwenyewe, vunja rekodi zako mwenyewe, kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa jana.
 92. Jenga nidhamu kali kweli kweli, jenga nidhamu hii kwako mwenyewe ili uweze kufanya yote unayotakiwa kufanya ili ufikie ndoto zako.
 93. Tamani na kuwa na shauku kubwa kuona ndoto na maono yako yanatimia, jitoe bila huruma kufanyia kazi ndoto zako, usitoe nafasi ya kukata tamaa, wala usitoe nafasi uvivu ukaingia kwenye maisha yako.
 94. Jenga nidhamu na maadili ya viwango vya juu sana ambavyo malaika wataona fahari kutembea na wewe, mbingu zitafurahia uwepo wako na kukusaidia kutimiza malengo yako.
 95. Jiambie kila siku unayoishi hapa duniani, kuwa mimi ni zaidi ya ninavyoonekana sasa, mimi ni zaidi ya ninavyojiona na wanavyoniona wengine, nina nguvu za kutisha, nina uwezo wa kiungu ndani yangu, ninaweza kufanikiwa sana, ninaweza kutimiza ndoto na maono makubwa niliyo nayo, ninaweza.
 96. Mungu Mwenyezi ndie chanzo cha uhai wako, nguvu zako na ndoto kubwa zilizopo ndani yako, katika safari ya kupambania ndoto zako usimuache Mungu hata hatua moja.
 97. Pigana vita dhidi ya mawazo dhaifu na mawazo hasi yanayotaka utawala kwenye fahamu zako, pigana vita kweli kweli kuyaondoa, simika utawala wa mawazo yenye nguvu, mawazo yenye afya na mawazo chanya, pigana vita hivi na ushinde kwa ushindi mkuu.
 98. Usihadaike na furaha za muda mfupi zenye kuleta majuto ya muda mrefu kwenye maisha yako, jiondoe kwenye fungu la udhaifu. Kuwa komandoo na jasusi na mpelelezi kwenye bustani ya ufahamu wako, hakikisha kitu chochote kinyonge na dhaifu hakiingii kwenye fahamu zako, ongeza umakini kwenye kusimamia ufahamu wako usichafuliwe na mawazo mabaya.
 99. Kuwa kiongozi na amiri jeshi mkuu wa maisha yako, jisimike nidhamu ya hali ya juu kama askari anayetii maagizo yote ya kijeshi bila kutoa sababu wala visingizio.
 100. Jitoe kwenye kundi la wengi wanaotoa visingizio na sababu nyingi, badala ya sababu nyingi na maneno mengi weka matendo mengi zaidi. Tumia muda wako kufanya mambo ya maana, muda ukienda haurudi kamwe, usipoteze muda kuhofia usiyoyajua na yaliyopo nje ya uwezo wako kuyafanya.

MWISHO: Binafsi nimefurahia sana usomaji wa kitabu hiki, ni kitabu chepesi sana kukisoma, unaweza kukisoma hata kwa siku moja, nashauri kisomwe na kila mtu maana kina mafunzo yanayomfaa kila binadamu. Kama una kiu ya kusoma vitabu, karibu kwenye kundi letu la WattsApp ambapo tunasoma kitabu kimoja kwa mwezi. Wasilina name tusome pamoja, karibu sana!

@Hillary Mrosso_30.05.2023


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X