Dhana ya jeshi la mtu mmoja, je ni dhana halisi au tunahitaji kufikiri nje ya boksi?


Moja ya dhana ambazo zimekuwepo miongoni mwa watu wengi ni dhana ya JESHI LA MTU MMOJA, kuna watu wamekuwa wanaamini kwamba kwenye shughuli zao ambazo wanafanya basi wao wanasimama kama jeshi la mtu mmoja.

Wakimaanisha kuwa wao ndiyo kila kitu kwenye shughuli au jambo fulani ambalo wanafanya, sasa ambacho leo hii ningependa tujadili hapa ni kwamba je, dhana ya jeshi la mtu mmoja ni dhana halisi au tunahitaji kufikiri kwa namna nyingine?

Tukitafakari kidogo kuhusiana na dhana hii ya jeshi la mtu mmoja, tuanze labda kwa kujiuliza. Jeshi ni kitu gani. Kujua hili nimezalimika kuangalia kwenye kamusi ya kiswahili sanifu, ambayo inasema kwamba Jeshi ni jumla ya askari ambao wameajiriwa kwa ajili ya kuilinda nchi. Maana ya pili ya neno Jeshi kutoka kwenye kamusi hii hii inasema kwamba jeshi ni jumla ya watu.

Tukiangalia maana hizi zote mbili tunagundua mambo yafuatayo.

Kwanza tunagundua kwamba tunapoongelea JESHI. Tayari tunakuwa hatuongelei mtu mmoja bali kikundi cha watu (jumla ya watu).

Lakini pia ukifuatilia zaidi kwenye maana hiyo, utagundua kwamba jeshi, siyo tu jumla ya watu, bali watu ambao wanafanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha lengo au kusudi fulani. Hilo ndilo jeshi.

Sasa mpaka hapo unafikiri Dhana ya jeshi la mtu mmoja bado ni dhana halisi?

Tukija kwenye biashara kwa mfano. Kwenye biashara kuna vitu vingi ambavyo vinahitajika kufanyika. Unahitaji ufanye masoko, unapaswa kuuza, unapaswa kutengeneza bidhaa na mengine mengi…

Inawezekana kwenye biashara yako uko peke yako, ila kiuhalisia siyo kwamba wewe ni jeshi la mtu mmoja. Bado kuna watu ambao unashirikiana nao, wasambazaji, watu wa usafiri, wateja n.k

Kwa hawa watu wote ambao unashirikiana nao, bado huwezi tu kusema kwamba wewe ni jeshi la mtu mmoja.

Kama wewe ungekuwa ni jeshi la mtu mmoja maana yake ni kwamba ungekuwa unafanya kila kitu mwenyewe bila kuhitaji mtu yeyote, na hata wateja ambao wananunua kwako hawapaswi kuwa wanwanunua kwako, badala yake unapaswa wewe kuwa ndiyo mteja wako kwenye biashara yako, ili tuseme kweli wewe NDIYE JESHI LA MTU MMOJA.

Ili biashara yako ikue, inahitaji watu. tena watu sahihi, kama hauna hawa watu utaishii tu kufanya biashara kama ambavyo watu wengine huwa wanafanya. Kwa namna ya ukawaida.

Hata kwenye maisha ya kawaida ya kila siku, dhana ya jeshi la mtu mmoja haipo. Haipo kwa sababu wewe haufanyi kila kitu mwenyewe. Dhana ya JESHI LA MTU MMOJA ingekuwa halisi kwenye maisha ya kawaida maana yake ungekuwa unapika chakula chako mwenyewe kwa sufuria ambazo umezitengeneza mwenyewe, unajisafirisha mwenyewe kwa gari ambayo umeitengeneza mwenyewe, unalima chakula chako mwenyewe kwa jembe na trekta ambayo umetengeneza, unapanda mbegu zako mwenyewe ambazo umezitengeneza mwenyewe, unaangalia runinga ambayo umeitengeneza mwenyewe na vipindi ambavyo umeviandaa mwenyewe na kuendelea na kuendelea.

Kiuhalisia ni kwamba dhana ya jeshi la mtu mmoja kwenye maisha haipo. Maisha ni kushirikiana na watu.

Upo kwa sababu fulani yupo, na yeye yupo kwa sababu wewe upo.

Ninavyoandika makala hii nimemkumbuka Harmonize maarufu kama Konde Boy ambaye anajiita jeshi.

Akimaanisha JESHI LA MTU MMOJA.

Kwa maoni yako unadhani Harmonize ni jeshi la mtu mmoja?

Siyo kweli kwamba harmonize ni Jeshi la mmoja. Harmonize ana meneja wake. Harmonize ana producer. Harmonize ana watu wa video. Harmonize anafanya kazi na watu wa redio na vyombo mbalimbali vya habari n.k

Hajifanyii interview mwenyewe.

Hasikilizi muziki wake mwenyewe baada ya kuutoa.

Haendi kwenye show kujitumbuiza mwenyewe…..

Ni kwa sababu kuna watu.

Kumbe dhana ya jeshi la mtu mmoja kwenye maisha ya kila siku, haifanyi kazi.

Kijana mmoja alimwambia baba yake kuwa baada ya hapa ninaenda kuwa naishi mwenyewe na nitakuwa sihitaji msaada wa mtu yeyote.

Hili jambo lilionekana kuvuta umakini wa baba yake.

Hivyo alitaka kuhoji na kuuliza zaidi kuwa je, ataanyaje?

Mtoto aliendelea kujieleza kwa kusema kwamba nitatatoka hapa, nitaita TEKSI ambayo itanipeleka uwanja wa ndege.

“Enhee” baba yake alionekana kumakinika.

Mtoto aliendekea kusema kwamba, nikifika uwanja wa ndege nitapanda ndege na kuelekea sehemu ambapo nitaanza kuishi maisha yangu.

Baba yake alivuta pumzi kidogo kisha akamwambia je, kwa nini unawatumia watu kufanikisha mambo yako. Kwa nini usifanye kila kitu mwenyewe. kwa nini wewe mwenyewe usijipeleke uwanja wa ndege. Kwa nini wewe mwenyewe usiwe rubani wako mwenyewe?

Mtoto alibisha kidogo na kusema.

Lakini si nitakuwa nawalipa?

Ndipo baba yake alimwambia “kuwalipa watu hakukufanyi wewe kuwa jeshi la mtu mmoja”

Ukweli ni kuwa, kwenye maisha ya kawaida ya kila siku, naam, kwenye maisha ya kila siku, hakuna jeshi la mtu mmoja. Maana unamkuna mmoja na yeye anakukuna, tunakunana.

Makala hii imeandikwa nami rafiki yako wa ukweli. Godius Rweyongeza

Hakikisha umepata vitabu vyangu ili kujifunza zaidi. Kupata nakala za vitabu vyangu ni rahisi sana. Wasiliana nami kwa 0684 408 755 sasa. Namba hiyo ipo whatsap na inapatikana kwa meseji na simu za kawaida.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X