Kazi ni nini?


Rafiki yangu mpendwa salaam. Hongera sana kwa kazi na kwa mapambano makubwa ambayo unaendelea kuyafanya.

Unastahili pongezi kubwa sana na hasa katika kipindi hiki ambacho watu wengi wanapenda sana fedha bila ya kupenda kufanya kazi na kujituma kwenye kazi zao.

Lakini sote tunajua wazi kuwa kazi ndiyo kipimo cha utu.

Kazi zinatupa utambulisho,

Kazi ndiyo njia ya uhakika ya kupata chochote unachotaka.

 

Juzi, tulisherehekea sikukuu ya wafanyakazi. Ni sikukuuu ambayo siyo tu inamhusu mwajiriwa, lakini pia inakuhusu wewe mpambanaji ambaye unajishughulisha na kupambana kila siku kuhakikisha kwamba unazalisha kazi ambazo ni bora sana.

 

Mambo muhimu kuhusu kazi ambayo ningependa ufahamu kuhusu siku ya leo ni kwamba

  1. Sasa ni wakati wa kupambana ili kuhakikisha unafanya kazi ambazo ni bora. Unajituma kwenye kazi na kuhakikisha unazalisha matokeo ambayo ni bora zaidi.
  2. Usikubali watu wakuzidi kwenye kazi, wanaweza kukuzidi kwenye hali ya uchumi walio nao sasa hivi, wanaweza kukuzidi kwenye kipaji walichonacho, wanaweza kukuzidi kwenye konekisheni walizonazo, ila hakuna mtu hata mmoja anayepaswa kukuzidi kwenye kuchapa kazi. wakati vitu hivyo vingine vipo nje ya uwezo wako, ila kuchapa kazi ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako, fanya kazi kwa bidii hata kama huoni matokeo makubwa leo hii, ukweli ni kuwa hakuna juhudi yako hata moja ambayo inapotea bure. Kuna siku utaona matunda ya juhudi zako kubwa ambazo unaweka kila siku.
  3. Usiruhusu kazi yoyote ambayo utafanya itoke mikononi mwako ikiwa haijakamilika. Mara zote hakikisha kwamba kazi yoyote unayofanya, inatoka mikononi mwako ikiwa imenyooka.

Ulimwengu wa leo umebadilika sana

Una vijana wengi wanaoshinda wakiangalia video na vibonzo mbalimbali ambavyo watu wameweka mtandaoni, ila wanachosahau ni kuwa wao wanageuka kuwa walaji, badala ya kugeuka kuwa wazalishaji (wachapakazi). 

Mtandao wa intaneti rafiki yangu utumie kuzalisha (kufanya kazi) badala ya kuutumia tu kumeza kila kitu kinachowekwa huku.

Kwa kazi yako yoyote ile ambayo unaifanya, unaweza kuiweka mtandaoni na kufanya vizuri.

Hivyo, hakikisha unakuwa na akaunti kwenye hii mitandao ya kijamii. Lakini pia hakikisha kwamba unakuwa na blogu au tovuti.

Na kazi yoyote ile ambayo utaweka mikono yako basi hakikisha pia umeiweka kwenye hii mitandao ya kijamii.

Kila la kheri.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X