Uakifishaji ni uwekaji wa alama za uandishi kama vile nukta, mkato, mshangao, kiulizo, funga semi na fungua semi pamoja alama nyingine nyingi ambazo kimsingi, ndiyo nguzo ya uandishi wa aina yoyote ile.
Leo ninazungumza na ndugu zangu waandishi wa vitabu. Ni ukweli usiyopingika kwamba, hakuna namna unaweza kujiita mwandishi kama hujui matumizi sahihi ya alama hizi.
Unaweza ukasoma kitabu cha mtu mpaka ukahisi kuchanganyikiwa kwa sababu, aya nzima yenye mistari zaidi ya mitano, hajaweka alama yoyote ya uandishi, yaani hata zile alama za kawaida kabisa ambazo huwezi kuzikwepa (nukta na mkato), hazipo. Ameandika tu kiasi kwamba ukisoma, unasikia kama unapigiwa kelele masikioni. Hili ni kosa katika uandishi, badilikeni.
Ndugu zangu waandishi, ninajua mnajua umuhimu wa alama hizi, ninachokifanya hapa ni kuwakumbusha tu ili tuzibe panapovuja na jumbe zetu ziifikie jamii kama ilivyokusudiwa.
Ni vyema ieleweke kwamba, ukiukaji wa matumizi ya alama za uandishi, unaweza kupotosha ujumbe mzima na hadhira unayoiandikia ikapokea kitu kingine kabisa ambacho ni tofauti na matakwa yako.
Kwa mfano, unataka utoe taarifa kuhusu ujio wa Juma halafu wewe unaandika hivi…
Baba Juma amekuja
Unadhani kwa uandishi huo, hiyo taarifa itafika kama ilivyokusudiwa! Kimsingi sentensi hiyo ilitakiwa iandikwe hivi…
Baba, Juma amekuja.
Sentensi tajwa hapo juu, zina maana tofauti kabisa ingawa maneno yaliyotumika yanafanana. Sentensi ya kwanza inatoa taarifa kuhusu ujio wa baba yake Juma na sentensi ya pili, ndiyo inayotoa inayotoa taarifa kuhusu ujio wa Juma. Kitendo cha kuacha kuiweka alama ya mkato kwenye neno baba katika sentensi ya kwanza, kimepotosha taarifa mzima ambayo mwandishi alikusudia kuitoa.
Sasa unaweza kuona namna ambavyo maudhui ya kitabu chako, yanavyoweza kupotoshwa kama usipozitumia kwa usahihi alama za uandishi.
Ukitaka upate matokeo bora katika kazi yako, lazima ufanye kilicho bora.
Hivyo, tujitahidi kuzingatia matumizi ya alama hizi ili kazi zetu ziwe bora na si bora kazi.
Asante kwa kufuatilia makala zetu za uandishi, tukutane wakati mwingine.
Jina langu ni
Magdalena Donacian Kamambi
Mhariri