
Moja ya kitu ambacho wazazi bado wanawaambia watoto ni kwenda kusomea kozi au kitu fulani kwa sababu wanahisi kinalipa. Mzazi anamwambia mwanae akasomee uhasibu kwa sababu yeye anahisi unalipa kuliko vitu vingine vyote, au anadhani mtoto wake atapata ajira.
Nafikiri ushauri wa namna hii ulikuwa ni ushauri halisi miaka kadhaa iliyopita, ila leo hii hauwezi kuwa bado ni ushauri halisi. Kwenye ulimwengu wa leo kuna mabadiliko mengi ambayo tayari yanatokea na sisi tunayaona.
Ujio na uwepo wa AI umepindua karibia kila kitu, vitu vingi ambavyo mwanzoni tulikuwa tunadhani haviwezi kufanywa na mashine leo hii tunashuhudia kwa macho yetu vikifanywa na mashine.
Kuna watu wanahudumiwa migahawani na akili bandia
Kuna mashine zinapika chakula
Kuna mashine zinatibu wagongwa
Kuna mashine ziko vizuri kwenye kufanya hesabu na zinakupa ushauri mzuri kutokana na takwimu ulizonazo.
Kwa lugha ya vijana naweza kusema kwamba disco limevamiwa na mmasai. Hakuna kozi, au kitu chochote ambacho unafikiri kwamba mwanao anaweza kusomea ambacho hakiwezi kufanywa na mashine. Kama mashine zinaweza kufanya ulinzi ambao kwa miaka mingi uliaminiwa mikononi mwa polisi na jeshi unadhani zitashindwa kulima, kumwangilia au kuzuia wadudu shambani?
Kama kuna sehemu ambazo hazina mashine basi ujue pengine watu wanaofanya kazi kwenye eneo husika hawajaanza kuzitumia au hawajafuatilia kujua kama zipo. Lakini ni suala la muda tu hizo mashine wataanza kuzitumia.
Sasa kwenye ulimwengu unaobadilika kwa kasi hivyo, ni vigumu sana kumwambia mwanao kwamba nenda shuleni usome kozi fulani kwa sababu inalipa zaidi
Mimi kwa maoni yangu naona huu ni ushauri wa kizee. Badala yake mzazi unapaswa kumshauri mwanao.
- Aendeleze kipaji, elimu au kitu chochote ambacho roho yake inapenda. Afanye kitu roho inapenda, ila siyo kufanya kitu ambacho analazimishwa kufanya. Kumbuka hiki kitu anaenda kukifanya kwa miaka mingi inayokuja mbele yake. Na kama hiki kitu akikifanya vizuri, nakuhakikishia kwamba hatakosa hela ya kula. Kuna watu wapo tayari kumlipa, endapo atakuwa anafanya hicho kitu kwa bidii na kwa nguvu zake zote.
- Mwanao afahamu wazi kuwa kufanya kazi kwa bidii kunalipa sana. Kunaweza kumkutanisha na wafalme, hata kama siyo mfalme.
- Aaminike. Katika ulimwengu ambapo watu wanasema kwamba uswahili na utanzania umetawala. Katika ulimwengu ambapo mtu anaweza kukuahidi kitu na asikifanyie kazi. Katika ulimwengu ambao mtu anaweza kuwa na haraka na kazi ila akazungushwa licha ya kwamba amelipia. Mwambie mwanao aaminike. Mwambie kwamba akimwambia mtu njoo kesho uchukue kazi yako, iwe ni kesho kweli na asirembe mwandiko kwenye hilo. Nakuhakikishia kitu kimoja cha uhakika kwamba, mwanao ataweza kupata soko la uhakika miongoni mwa watu kuliko pale akisomea hicho kitu ambacho unadhani kwamba atalipwa vizuri huku akiwa hafanyi kazi kwa bidii.
- Ndiyo yake iwe ndiyo yake na hapana yake iwe hapana yake. Akisema neno, ahakikishe analitimza. Atalipwa zaidi ya mtu mwingine yeyote, nakuhakikishia.
- Ajenge sana ujuzi wa kuwasiliana. Sisi ni watu na tutaendelea kuwa watu. Hata kama zinakuja mashine,. Haziondoi utu wetu. Bado nitapenda kuhudumiwa kiutu. Kuna vijana wamesomea kozi nzuri sana, wanajua vitu haswa, ila hawajui kuhudumia watu na hawajui kuongea vizuri na wateja. Ninvyoandika hapa, jana kompyuta yangu ilipata shida, nikaipeleka kwa fundi. Fundi huyu yuko vizuri sana kwenye kutengeneza hizi mashine, ila changamoto yake ni moja tu, uwezo wake wa kuwasiliana na watu ni mdogo sana. Huwa ninamtumia kwa sababu tu, ANAIWEZA KAZI. Iila kwa mfano akitokea mtu ambaye anaiweza kazi kama yeye na anajua kuongea vizuri na watu, anajali n.k. nakuhakikishia huyu fundi naweza kumhama ndani ya usiku mmoja tu. Kwa sababu utu bado tunaupenda. Ni kupitia kuwasiliana ndiyo tunajua namna unavyojali utu wa watu au la! Mwambie mwanao ajifunze sana kuwasiliana na watu itamsadia kwenye kazi yake
- Mwmabie mwanao pamoja na hicho ambacho anataka kusomea au kufanyia kazi, ajifunze kuuza pia. kwenye uliwengu wa leo, kuuza ni lazima. Kujua kitu bila kujua kuuza ni kazi bure. Lazima ajue namna ya kuwashawishi watu wngine ili wawezekununua kitu hicho.
- Mwambie pia mwanao kwamba hata baada ya kuwa amemaliza masomo asiache kujifunza. Kwake kujifunza kuwe ni kila siku. Atenge muda asome kitabu, atenge muda ajifunze kozi mtandaoni. Katika ulimwengu ambao unabadilika kwa kasi. Kujifunza ni tiketi muhimu ya yeye kuendelea kuwa mbele na kufanya makubwa. Mwambie kamwe asiache kujifunza.
- Mwambie kwamba muda ni mali. Aache na dhana ya kwamba hakuna haraka barani afrika, badala yake ajali muda siku zote. Apangilie ratiba zake vizuri na azifuate. Akimwambia mtu kwamba tukutane saa 10 ahakikishe kwamba hiyo saa 10 ameweza kukutana naye kwelikweli.
Kuna mengi ya kumwambia ila kwa sasa mwambie azingatie hayo. Nakuhakikishia kuwa mwanao ataweza kufanya makubwa kwenye ulimwengu huu unaobadilika kuliko tu wewe kumwambia kwamba akasomee kozi fulani kwa sababu inalipa, bila kumwambia vitu vya ziada kama hivi.
Imeandikwa na Godius Rweyongeza
Unaweza kuwasiliana na mwandishi kupitia namba ya simu 0755848391