Huhitaji kusubiri mpaka uwe na kila kitu


Ni mara nyingi sana watu huwa wanasubiri mpaka wawe na kila kitu ili waweze kuanza kuanza kufanyia kazi malengo yao, ndoto zao, au kitu ambacho wanafikiria. Mtu haanzi hiyo biashara kwa sababu anasubiri mpaka aweze kupata kila rasilimali ambayo anafikiri anahitaji. Mtu haanzi kufanyia kazi hicho kipaji chake kwa sababu anasubiri mpaka awe na kila kitu ili aweze kufanyia kazi hicho kipaji chake.

Kusubiri  mpaka uwe na kila kitu ili uweze kufanyia kazi malengo na ndoto zako kunaweza kukufanya usianze kabisa. Unakuwa ni sawa na mtu ambaye anasubiri ashibe ili aanze kula. Huwa hatuanzi kula tunapokuwa tumeshiba, bali huwa tunaanza kula hata kama hatujashiba. Wewe pia anza kufanyia kazi malengo na ndoto zako bila kuchelewa.

Unachohitaji kujua ni wapi unaelekea.

Ni rasilimali gani ulizonazo ambazo unaweza kuanza nazo. Hili pia ni muhimu kwa sababu, huwezi kuanza kufanyia kazi malengo na ndoto zako kubwa kama hauna kila rasilimali, unaweza kuanza kufanyia kazi malengo na ndoto zako kwa rasilimali hizo hizo kidogo ulizonazo. Ukweli ni kuwa uhaba wa rasilimali, ndiyo huwa unatengeneza kampuni imara na watu imara. Muda mwingine uwepo wa kila rasilimali huwa unafanya watu wanabweteka na hata wanashinda kutumia vizuri hizo rasilimali. Lakini rasilimali zinapokuwa haba, maana yake ni kwamba hao watu wanaongeza juhudi na bidii katika kuhakikisha kwamba wanatumia kile kidogo walichonacho kufanya makubwa.

Mfano wa nchi ambayo ilionesha uwezo wa kufanya makubwa kwa kutumia rasilimali kidogo ilizokuwa nazo ni Japani. Baada ya vita ya pili ya dunia, Japani ilikuwa kwenye hali mmbaya. Hali yake ya uchumi ilikuwa chini, miji yake miwili mikubwa ilikuwa imelipuliwa na mabomu.

Lakini bado katika mazingira haya, viongozi hawakuachakuota ndoto kubwa ambazo wangeweza kuzifanyia kazi. Hatimaye walianza kuzifanyia kazi.

Kufikia miaka ya sabini na themani, Japani iliingia miongoni mwa nchi ambazo zilikuwa na uchumi mkubwa sana hapa duniani. Lakini hii yote ilitokana na uwezo wa kutumia rasilimali haba ambazo zilikuwepo. Kumbe hii ndiyo kusema kwamba, ukiwa na rasilimali fulani kwa uhaba basi usiogope. Jifunze namna bora ya kuzitumia hizo rasilimali chache kwa ubora, ili ziweze kuleta manufaa makubwa.

INAWEZEKANA KUFANYA MAKUBWA KWA KUTUMIA RASILIMALI CHACHE ULIZONAZO.

Unahitaji pia kujua ni watu gani unaambatana nao. Ukiambatana na watu sahihi, watakuonesha wewe namna unavyoweza kuanza kwa kutumia rasilimali zako hizo. Kumbuka kuwa  wengi unaowafahamu leo hii kama watu waliofanya makubwa hawakuwa watu ambao walikuwa wana kila kitu walipoanza. Walianza kufanya kwa kutumia rasilimali ambazo walikuwa nazo, baadaye wakaendelea kuboresha na kukuza kile walichokuwa wanafanya.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X