JICHANGAMOTISHE


Uliwahi kufanyika utafiti kwa madereva waliokuwa wanaendesha taxi zao kwenye jiji la LONDON, moja ya kitu cha kipekee sana kilichogundulika kwa madereva hawa wa jiji la LONDON ilikuwa ni kwamba ubobgo wao ulionekana kuwa imara sana, ukilinganisha na madereva wengine ambao walikuwa hawaendeshi magari yao kwenye mazingira yenye barabara nyingi na idadi kubwa kama London.

Ikagundulika kwamba kwamba, kumbe changamoto za kuendesha gari kwenye mazingira yenye idadi kubwa, barabara nyingi, kona nyingi na vingine vingi, vilifanya ubongo wa watu kuwa imara zaidi.

Leo nataka niongee na wewe rafiki yangu ambaye siku zote huwa unaogopa changamoto na vikwazo. Unaviona kama jela vile. Ukweli ni kuwa changamoto na vikwazo ambavyo unakutana navyo kila mara vipo kwa ajili ya kukuimarisha. Vinakupa somo jipya kwenye maisha ambalo kama ukilifanyia kazi utazidi kuwa imara zaidi na utaweza kufanya makubwa.

Vikwazo vinaibua ukuu uliolala ndani yako. hivyo, usiogope unapokutana na vikwazo, bali vipende vikwazo, vikumbatie.

Huwa napenda kuwaambia watu kuwa vikwazo ni kama darasa. Ukishavuka darasa unaona maswali ya darasa la nyuma ni rahisi. Lakini ukweli ni kuwa kuna wakati maswali hayahaya yalikuwa yanakugalagaza, ila kwa sababu hukuyakimbia ndiyo maana sasa hivi ukiangalia nyuma unaona ni rahisi sana.

Hivyo, na wewe usiogope vikwazo, nakuhakikishia kuwa utakapokuwa umeweza kuvuka hivi vikwazo. Utaangalia nyuma na kuona kwamba ni rahisi sana kuvuka hivi vikwazo, utaangalia nyuma na kusema kwamba, mbona hapo ni rahisi?

Lakini usipovuka hivi vikwazo, utabaki kusema kikwazo fulani ni kigumu sana.

Na hata wengine utawaambia kwamba haiwezekani kuvuka kikwazo fulani, utawaambia kwamba haiwezekani kwa sababu, wewe mwenyewe ulishindwa kuweka juhudi kuvuka hicho kikwazo kwa wakati husika.

Ni kikwazo gani ulichonacho kwa sasa hivi? Je, ni kikwazo cha kuweka akiba? Unaona kwamba ukiweka akiba, hela haitoshi? Hiki kinaweza kuwa kikwazo kwa sasa hivi, ila fanya kitu kimoja, amua kwamba liwalo na liwe. Mimi nitaweka akiba tu. Kama nitakutana na changamoto au kikwazo chochote, nitapambana mpaka nishinde. Nakuhakikishia kuwa utashinda na kuna siku utaangalia nyuma na kuona kwamba MBONA HAPO NI RAHISI TU?

Pengine kikwazo chako ni kwenye kufanya KIPAJI CHAKO KIJULIKANE. Hilo ndilo jambo ambalo unapaswa kuwa unalipambania. Lipambanie kwa nguvu zako zote, na kamwe usirudi nyuma. Kuna siku utaangalia nyuma na kusema kwamba MBONA HAPO NI RAHISI tu, utaweza kusema hivyo kwa sababu tu, uliweza kuvuka kikwazo ambacho kilikuwa mbele yako kwa wakati husika. Hukutaka kubaki nyuma na wala kukwamishwa na mtu au kitu chochote.

Kwa leo tuishie hapa

Makala hii imeandikwa na Godius Rweyongeza.

Tuwasiliane kwa 0755848391


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X