
Rafiki yangu mpendwa, nichukue nafasi hii kukupongeza sana kwa kuumalizia mwezi wa Januari. Najua wazi kuwa haujawa mwezi rahisi, hivyo nikupongeze sana kwa hilo.
Mwezi januari unapofikia tamati, ningependa kwa pamoja tufanye tafakari kuhusiaa na mwezi huu wa kipekee. Mwisho wa siku tujiulize kuwa mwezi huu umeubariki au umeualaani? Umekuwa wenye Baraka kwako au wa karaha?
Kila mwaka huwa kuna mwezi Januari na kila mwaka kuna mwezi Disemba.
Na sote tunafahamu kwamba kuna majukumu ambayo yako mbele yetu.
Kwa wengi tunajua kwamba ukifika mwisho wa mwaka na hasa sikukuu, kuna sherehe. Kwa wengi matumizi ya pesa huwa yanakuwa juu. Huwa yanahusisha kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kitu ambacho huwa kinaongeza gharama za matumizi na kuzifanya kuwa kubwa zaidi
Kwa kuwa huwa ni sikukuu huwa tunaenjoy, lakini wakati huohuo ni kama huwa tunasahau majukumu yetu ya muhimu.
Majukum ya januari. Kwa upande mwingine ni kwamba Januari ni mwezi wa kipekee pia. kwa kuwa watoto huwa wanafunga shule disemba yote, januari baada ya sikukuu kuisha, huwa ni muda wa watoto kurudi shule sasa ili wasome.
Na hapa ndipo swali langu la kwanza linapojikita leo. Januari inapoisha umeibariki au umeilaani?
Najua unajua wazi kwamba una watoto wako. Labda mmoja au wawili, watatu n.k
Hiki siiyo kitu ambacho mimi napaswa kukufundisha si ndio?
Lakini pia unajua wazi kwamba watoto hawa wanapaswa kwenda shule Januari au la! Kwa mfano leo hii unaposoma hapa, unajua mwakani kwamba wanao watakuwa wanaenda shule au watakuwa hawaendi. Kama watakuwa wanaenda maana yake maandalizi ya mapema yanatakiwa kufanywa kuanzia leo hii. Changamoto ya watu wengi ukiwaambia wafanye maandalizi ya ada ya mtoto mwkani wanaona ni kitu cha ajabu sana. Wengi wataishia kukwambia siku bado. Lakini sasa unabaki unajiuliza. Bado nini? Sasa mtu huyuhuyu subiri ifike januari.
Ndiyo anaanza kukwambia Januari ni ngumu na hizi ada za watoto. Sasa kwa maneno hayo unakuwa unaibariki Januari au unakuwa unailaani? Je, watoto wako unakuwa unajivunia kuwa nao au unalaumu?
Yaani, ni kama vile hao watoto kuna mtu aliwaleta kwako ghafla na kukuamuru kwamba kuanzia leo hii hawa ni watoto wako, walee. Lakini kumbe watoto umewazaa mwenyewe, umewalea mwenyewe na sasa hivi kukosa kwako mipango ndiyo unaanza kuilaani Januari, na hata watoto wako unaanza kuwaona kama karaha? Haya ni ya kweli? Ebu jirekebishe bwana kuanzia mwaka 2025.
Ujue kama unaweka malengo, huwa kuna malengo ambayo yanajirudia kila mwaka. Lengo la kulipa ada kila januari liweke kama lengo ambalo linajirudia kila mwaka.
Pengine badala ya kusubiri kulipa ada Januari, unaweza kuwa unailipa mapema. Disemba au novemba.
Nakumbuka mwishoni mwa mwaka jana nilikutana na mama mmoja aliyekuwa anajiandaa kwenda uchagaani kwa ajili ya likizo. Lakini kabla ya kufanya maandalizi ya kitu chochote, kitu cha kwanza alichofanya ilikuwa ni kuhakikisha amelipa ada zote za watoto.
Siku hiyo nilikutana naye njiani anatabasamu, ikabidi nimuulize kulikoni, ndipo aliponiambia kuwa nimelipa ada zote za watoto, hapa hata nikienda nyumbani nikajisahau nikatumia hela zote, nitakuwa bado na uhakika wa ada za watoto kuwa zimelipwa.
Nilichojifunza kwa mama huyu ni kwamba, badala ya kusubiri mpaka Januari uanze kulalamika kuhusiana na watoto wako, ANZA KUANDAA HIZI ADA MAPEMA. Kisha jipange kuhakikisha kwamba unailipa mapema kabla hujaila.
Unapolalamika kuhusiana na kulipa ada Januari wakati ni wajibu wako. Ni kama unakuwa unaona karaha kuwa watoto wako. Ni kama unakuwa unawalaani kuwa bora wasingezaliwa.
Makala hii imeandikwa na
GODIUS RWEYONGEZA
Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0755848391