JE, UNAAMKA SAA NGAPI? UNAFANYA NINI BAADA YA KUAMKA? Mbinu Mpya Na Zilizothibitishwa Zitakazokuwezesha Kuamka Asubuhi Na Mapema


Habari ya siku hii njema sana rafiki, hongera sana kwa siku hii ya leo. Maana leo ni siku njema kweli maishani. Hakikisha unaitumia vyema.

Moja kati ya swali ambalo nimekuwa naulizwa sana, ni swali la ninapata wapi muda wa kuandika makala mpya kila siku?

Hili ni swali ambalo karibia kila mtu ninayekutana naye anapeda kujua ni wapi muda huu nauiba wa kuandika. Ila ukweli ni kwamba hakuna muujiza. Wala sio kwamba mimi Godius Rweyongeza nina muda wa ziada kuliko mtu mwingine yeyote. Kuna maeneno mengi sana, sana ambayo unaweza kupata muda huu ila leo hii nataka nizungumzie muda wa asubuhi.

Nitakuonesha wazi wazi utakavyopata muda wa kukutosha. Utakoutumia kufanya kazi zako ambazo ni tofauti na hizi ambazo umezoea. Lakini pia utaweza kuwa na kitu cha ziada tofauti na watu wa kawaida ambao wamekuzunguka.

Lengo sio kwamba upate muda huu uandike kama mimi. Hasha, bali upate muda huu na uutumie kufanya kile unachokipenda (mimi napenda kuandika ndio maana nautumia kuandika). Lakini pia lengo langu ni kutaka kukuondoa kwenye lile kundi la walalamikaji ambao kwao januari mpaka disemba hawana muda wao wa kufanya kazi zao. Kila siku wanahairisha, na kuhairisha na kuhairisha.

 Rafiki, utapata pia muda wa kuendeleza kipaji chako. Maana kama niishivyo lengo langu kubwa ni kuhakikisha watu wanaishi kile kilichowaleta hapa duniani. Na ili uweze kuishi kile kilichokuleta hapa duniani basi huna budi kuhakikisha kwamba unapata muda ziada kila siku. Ndio kila siku.

KWA NINI KUAMKA ASUBUHI NA MAPEMA?
Kuna ule usemi wa Ben Franklin ambao binafsi huwa naupenda sana, na tangu nilipoufahamu nikiwa sekondari mpaka leo hii huwa nauiishi. Usemi huu unasema hivi, “kulala mapema, kuamka mapema, kunakufanya kuwa mwenye afya njema, tajiri na mwenye busara”

Bila shaka utakuwa unajiuliza ni kwa jinsi gani kuamka mapema kunaweza kunifanya nipate hivi vitu vitatu. Yaani niwe na AFYA BORA,  TAJIRI, na MWENYE BUSARA.

Je, hii ni kweli!
Jibu langu la haraka ni ndio. Kuamka mapema kutakufanya upate muda wa kufanya mazoezi, tofauti na mtu mwingine ambaye atakurupuka baadae sana akiwa amechelewa.

Kuamka mapema kutakufanya upate nafasi ya kutembea na kufurahia dunia. Mfano utakuwa miongoni mwa watu wachache sana ambao wanashuhudia wazi wazi kuchomoza kwa jua. Duuh! Yaani hii raha sana.
Yaani hii ndio kusema kwamba vitamini D ya asubuhi unakuwa wewe wa kwanza kuipata kabla ya mtu mwingine yeyote.

Hivi ni vitu vidogo sana ambavyo vitaimairisha afya yako ya mwili.

Lakini pia kuamka mapema kutakufanya upate muda walau nusu saa ya kusoma kitabu. Hapa utakuwa unaimarisha afya ya akili.
Na kwa kuwa asubuhi bado akili ibakuwa ina nguvu sana basi utapata pia muda wa kutafakari. kutafakari sio tu kunaimarisha afya ya roho bali pia kunaimarisha afya ya mwili. Unaona sasa.

Hizo faida huwezi kuzipata kama wewe unachelewa kuamka kila siku.

Ngoja niendelee kidogo. Maana mpaka hapo nimezungumzia juu ya kuamka mapema kunavyoweza kukufanya tajiri. Hahaha! Inaonekana kama upumbavu fulani hivi ila ni ukweli mtupu.

Ni asubuhi na mapema ndipo unaweza kuamka na kutafakari juu ya biashara mpya ambazo unaweza kufanya.

Ni asubuhi na mapena ndipo unaweza kuamka na kupangilia ratiba ya siku nzima, ufanye nini na usifanye nini!

Ni asubuhi na mapema unaweza kutafakari juu ya kitu gani uborehse kwenye biashara yako au mahusiano yako na hata kazi   unayoifanya iweze kupendeza na kuwa bora zaidi ya  ilivyokuwa jana.

Soma zaidi: Hii ni Kauli Ambayo Unapaswa Kuiepuka

Je, bado mpaka hapo unahitaji nikwambie kwa nini unapaswa kuamka mapema?  Kabla sijakwambia unawezaje kuamka mapema, naomba nikumbie jambo moja la ziada (bonus point).

Asubuhi mtu anakuwa anatembea mzima mzima, ila jioni mtu anatembea na miguu.
Hahahah! Usishangae, asubuhi akili yako inakuwa na uwezo mkubwa wa kuchakata, kuamua mapema, na kufanya vitu vingi zaidi. Kadri siku inavyosogea akili inazidi kuchoka na uwezo wa kufanya maamuzi unapungua. Sasa unajua nini kinatokea, unaanza tu kutembea kwa miguu lakini akili ishachoka zake kitambo.

Tujikumbushie tena, Asubuhi mtu anakuwa anatembea mzima mzima, ila jioni mtu anatembea na miguu.

SASA NAWEZAJE KUAMKA ASUBUHI NA MAPEMA?
Bila shaka unajiuliza swali hilo hapo.
Na mimi nakuuliza unaamka saa ngapi? Jibu hapa kwanza.

Sasa hapa unaweza kufanya mambo haya ili uweze kuamka mapema

Moja amka dakika moja kabla kila siku. Kama leo umeamka saa moja kamili. Basi kesho amka saa kumi na mbili dakika hamsini na tisa. Na kesho kutwa saa kumi na mbili dakika hamsini na nane. Endelea hivyo mpaka ufikie muda mzuri unaotaka kuamka.
Watu waliofikia mafanikio makubwa sana huamka kati ya saa 10 asubuhi na saa 12 asubuhi na sio zaidi ya hapo.

Soma Zaidi: Mambo Manne (04) Unayopaswa Kufanya Unapoamka Asubuhi

Pili lala mapema. Kama tulivyoona hapo juu. Ili uweze kuamka mapema basi huna budi kulala mapema. Na mimi siku zote najua hivi, kulala mapema, kuamka mapema, kunakufanya kuwa mwenye afya njema, tajiri na mwenye busara”

Tatu punguza muda wa kuangalia runinga (TV).

Nne usiangalie tamthilia au matangazo ya mauaji, rushwa, wizi, majini, au uchawi kabla ya kulala. Hii itakufanya usilale kwa raha maana unachoona dakika za mwisho kabla ya kulala kinajitokeza sana usiku unapokuwa umelala.

Kiukweli nahisi leo nimekuandalia kitu kikubwa sana sehemu moja. Nikiongelea juu ya kuamka asubuhi, umuhimu wake na jinsi unavyoweza kuamka asubuhi na mapema bila kuharibu ratiba zako.

Rafiki kwa leo naishia hapo,

Kalamu naweka chini, Chini hapa kwa dawati,
Kuamka asubuhini,  dawa ya zote nyakati,
Uwe wa kaskazini, Au hapo katikati,
Kuamka asubuhi, ni dawa ya zote nyakati.

Asante sana, tukutane kwenye jukwaa la wanamafanikio.

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA


HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA


One response to “JE, UNAAMKA SAA NGAPI? UNAFANYA NINI BAADA YA KUAMKA? Mbinu Mpya Na Zilizothibitishwa Zitakazokuwezesha Kuamka Asubuhi Na Mapema”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X