Hivi Ndivyo Unaweza Kutoa Hotuba Yako Kwa Watu Kama Vile Uko Mbele Ya Mkutano Wa Umoja Wa Mataifa.


Mikutano ya umoja wa mataifa ni mikutano yenye watu kutoka kila nchi.  Hivi kwa mfano leo hii ukiambiwa umepewa nafasi ya kwenda kuongea mbele ya mkutano mmojawapo wa umoja huu wa mataifa, utafanyaje? Je, unaweza kwenda au kukataa? Je, kama utaamua kwenda nini unapaswa kuzingatia?

Na Je, badala ya umoja wa mataifa ukiambiwa kuna kikundi cha watu kumi au kumi na tano na unapaswa kwenda kuongea mbele yake utakuwa tayari?

Mtu mmoja amewahi kusema kwamba, idadi ya watu ambao upo tayari kuhudumia inaonesha kiwango gani cha pesa utaingiza. Ukihudumia watu kidogo maana yake utatoa huduma kidogo na mwisho wa siku utapata kidogo na ukiwa tayari kuwahudumia wengi basi baraka nyingi zitakuja kwako.

Sasa tukirudi kwenye mada. Kuongea mbele ya watu sio kitu lelemama. Iwe unaongea mbele ya mkutano mkubwa kama wa umoja wa mataifa au unaongea kwenye kikao cha familia. Kuna mambo ya muhimu utapaswa kuzingatia ili kutoa hotuba iliyoshiba wakati wote.

1. Unapaswa kujua aina ya watu utakaoenda kuongea mbele yao.

2. Jua kitu gani ambacho kinahitajika kuongelewa (mada).

3. Andaa mada mapema sana, usisubiri kukurupuka siku ya mwisho ili uanze kujiandaa.

4. Fanya mazoezi ya kuongea chumbani kwako kwanza, kisha Waite watu wako wa karibu kama watano  uongee mbele yao kama sehemu ya mazoezi.

5. Kama hotuba yako umeiandika jua vitu vya msingi ambavyo utapaswa kuongea. Andika hotuba yako ila usijiandae kwenda kusoma kila kitu. Hotuba za kusoma kila kitu huwa hazinogi. Binafsi nikiona mtu anasoma kila kitu nasema bora angenipa karatasi nikaenda kusoma mwenyewe muda wangu wa ziada.
Kwa hiyo siku ya kutoa hotuba usisome neno kwa neno. Soma tu zile pointi za muhimu na utoe maelezo yake.

6. Fanya mazoezi mengi uwezo.

7. Siku ya tukio fika mahali husika mapema. Ukichelewa utahaha, kiasi cha kusahau kila kitu.

8. Kunywa maji kiasi dakika 30 mpaka SAA moja kabla ya kuongea. Maji ya uvuguvugu ni bora zaidi.

9. Muda wa kuongea ukifika, tafuta mtu mmoja wa kuangalia wakati wa hotuba yako. Kama ni mzoefu unaweza kuangalia wasikilizaji wako kwa wakati mmoja baada ya mwingine.
Kama hujazoea mtafute mtu mmoja na komaa na huyo mpaka umalize hotuba yako.

Haifai kutoa hotuba ukiwa umeinama chini. Hii ni ishara kubwa ya kuwaogopa watu.

Umekuwa nami,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA

,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X