NGUVU YA RIBA MKUSANYIKO-Utangulizi


 

Riba mkusanyiko ni nini?

Riba mkusanyiko ni muunganiko wa vitu baada ya kuwa vimefanyika kwa kipindi kirefu katika kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Vitu  vikifanyika mara kwa mara kwa muda mrefu, huleta nguvu ya pamoja ambayo kwa kufanya kitu kwa wakati mmoja isingewezekana. Kwa mfano ni nadra sana kuangusha ukuta kwa kupiga nyundo moja tu. Hata hivyo, ukipiga nyundo nyingi unakuta mwisho wa siku zinapelekea kuanguka kwa ukuta. Hapa inakuwa siyo kwamba ukuta umeanguka kwa sababu ulipiga ile nyundo moja ya mwisho, bali kwa mkusanyiko wa nyundo zile nyundo kwa pamoja. Na hiyo hapo ndiyo inakuwa nguvu ya RIBA MKUSANYIKO. 

Riba mkusanyiko inafanya kazi katika maeneo mengi ya maisha na wewe unaweza kuitumia kunufaika katika mambo mengi. Unaweza kuitumia nguvu hii kwa namna chanya kwenye kuweka akiba, kuwekeza, kusoma vitabu, kujenga mahusiano, kujenga tabia mpya mpaka kuandika vitabu.

Nguvu hii pia huwa inatumiwa na watu kwa namna hasi kwa kujua au kutojua na hivyo kuwapelekea kupata matatizo au kuingia kwenye ubaya. Kuna watu wameingia kwenye uraibu wa kunywa pombe kwa kuanza kidogo na baadaye kujikuta wameshakuwa wanywaji wakubwa.

Na hii siyo tu kwenye uraibu wa pombe bali karibia kwenye kila eneo hasi, Kama ilivyo kuwa unaweza kuitumia nguvu hii kujenga unaweza pia kuitumia kubomoa. 

Kwenye kitabu hiki cha NGUVU YA RIBA MKUSANYIKO tunaenda kuona ni kwa jinsi gani utaweza kuitumia nguvu hii kwa namna chanya kwenye maeneo mbalimbali na ukapata matokeo makubwa. Je  , upo tayari kwa ajili ya safari hii? Imani yangu ni kuwa baada ya kuwa umesoma kitabu hiki, utachagua kitu kimoja ambacho utakifanyia kazi kwa kutumia NGUVU YA RIBA MKUSANYIKO. Nakutakia usomaji mwema.

Godius Rweyongeza

Jumatatu, 9 Agosti, 2020

Morogoro


2 responses to “NGUVU YA RIBA MKUSANYIKO-Utangulizi”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X