UCHAMBUZI WA KITABU CHA SUGU MAISHA NA MUZIKI. Mambo 14 niliyojifunza kwenye kitabu hiki kinachoeleza Maisha ya Sugu Kutoka Mtaani Mpaka Bungeni


Mwishoni wa uchambuzi huu, nimeeleza jinsi unavyoweza kupata nakala ya kitabu hiki. Nipo tayari kukuchangia kiasi kidogo ili upate nakala ya kitabu hiki kizuri cha Kitanzania.

Kwanza, karibu kwenye uchambuzi wa  cha SUGU. kitabu hiki kimeeleza maisha ya msanii Joseph Osmund Mbilinyi, maarufu kama Sugu. Ambaye ni mmoja kati ya wanahiphop wa kwanza hapa Tanzania, aliyeshiriki kikamilifu katika kuanzisha aina hii ya muziki na baadaye kuikuza. Sugu anasema yeye ni miongoni mwa wasanii wa kwanza kwanza kabisa walioanza kuchana kwa lugha ya Kiswahili na pia kuichana serikali bila kificho.

Anasema kabla yake waliokuwa wanaimba aina hii ya muziki walikuwepo; ila hawakuwa wakichana kwa lugha ya Kiswahili, badala yake  walitumia kiingereza na tena waliiga wasanii wa kizungu waliokuwa maarufu kwa wakati huo. Kuchana kwa Kiswahili   kulimfanya kuwa mtu wa tofauti na hata kupendwa zaidi.

Leo tunaenda kuona sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu hiki cha SUGU: THE AUTOBIOGRAPHY: MUZIKI NA MAISHA. From The Streets To Parliament.
Pale ambapo nitatumia lugha ya kishikaji ambayo sijazoea kutumia kwenye blogu hii, nitaomba uivumilie maana mwandishi kaitumia hapa na pale kwenye kitabu. Sasa bila kupoteza muda haya hapa ndiyo mambo 14 niliyojifunza kwenye kitabu

1. Sugu anasema siyo kwamba amefika hapo kwa bahati au upendeleo kama wengi wanavyofikiri badala yake anasema amesota sana mpaka kufikia hatua ya kuwa SUGU! Ukurasa wa 42 wa kitabu.

2. Sugu anasema amepitia mengi ikiwa ni pamoja na kufanya uhuni akiwa Mbeya Day, sekondari ambayo alisoma. Kitu kilisababisha mpaka afukuzwe shule na baadaye kuhama shule hiyo. Baadaye akiwa kijana alijaribu kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha kitu ambacho hakikufanikiwa na baadaye akiwa tayari amekuwa mwanamziki alienda Ulaya pia kujaribu maisha, ila bado hakuweza kutoboa.

Kila mara alipoenda nje ya nchi alikuwa akikutana na changamoyo kama kufungwa kwa mipaka au kuumwa (home sick) kitu ambacho kilikuwa kinasababisha arudi nyumbani.

Kwenye hili nimejifunza kuwa; zile hadithi za kuwa ukienda sehemu fulani utatoboa haraka, zinaweza kuwa zinavutia, ila ukienda eneo husika wanaposema kuna maisha mazuri, ndipo unauona ukweli wenyewe   Kumbe usidanganyike kwa kutaka kukimbilia sehemu fulani, kisa eti unasikia kuna maisha mazuri, kuna uwezekano ukaenda huko na usiyapate hayo maisha mazuri.

3. Sugu anatuonesha nguvu ya watu waliokuzunguka wanavyoweza kukufanya uinuke au uanguke. Na hili utaliona wazi kwenye maisha yake kuanzia utotoni mpaka ukubwani. Ni marafiki zake wa sekondari waliomfanya awe mhuni.
Ni rafiki yake ndiye alimfundisha kuandika mistari kwa  Kiswahili badala ya kiingereza.
Ni rafiki zake pia waliokuwa wakimpa konekisheni na watu muhimu kwa wakati huo
Na ni rafiki zake au watu waliokuwa wamemzunguka kwa wakati huo waliojenga njama za kumwangusha na hata kupelekea yeye kustaafu muziki bila kutaka.

4. Kwenye kitabu hiki anaonesha pia jinsi wazazi walivyo na nafasi kubwa kwenye maisha ya watoto wao. Anamkubali sana baba yake kwa mengi aliyoyafanya na hasa kikubwa kutafuta maisha na kuitunza familia yao vizuri.

Pia kwenye kitabu amemweleza mama yake kama mtu ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwenye uimbaji wake. Mama yake ndiye aliyemruhusu aingie kwenye gemu ya mziki. Hii ni kutokana na ukweli kuwa miaka hiyo, muziki ulikuwa unaonekana ni kitu cha hovyo. Wazazi hawakuruhusu watoto wao wawe wanamziki. Ila hali kwa mama yake Sugu ilukuwa tofauti. Alimruhusu.
Pia mama yake ndiye aliyekuja kuwa mhimili mkubwa sana pale alipotaka kuacha mziki; mwishoni mwa miaka ya 90. Alimpa moyo kwa kusema aendelee.

5. Sugu anasema alijenga historia ya kuwatoa wasanii wawili kwenye albamu yake ya milenia aliyoitoa mwaka 2000. Wasanii hao ni Afande Sele na Lady Jay Dee

6. Sugu anaamini kuwa kusafiri kunakufanya ujifunze mambo mengi ambayo huwezi kujifunza kwa kukaa eneo moja. Na yeye anasema kwamba ameweza kujifunza mengi kwa kusaifiri nje ya nchi kukiko hata wasomi wanavyoweza kujifunza darasani.

7. Sugu anasema kila mti wenye matunda huwa haukosi kupigwa mawe. Kwenye kitabu hiki anaeleza jinsi alivyopitia changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kutopewa mauzo sahihi ya albamu zake. Kuendeshwa kwa kampeni za wazi za kumwangusha na baadhi ya watu wakiwemo wamiliki wa redio ya Clouds, kitu ambacho anasema yeye alikipinga vikali.

8. Muda mwingine ni muhimu kuonesha msimamo wako ili kujenga heshima yako na mazingira mazuri ya kikazi.

9. Usilewe sifa. Ukipata sifa weka kazi zaidi kwenye kile unachofanya. Achana kujisikia kupita kiasi kitu ambacho kinaweza kupelekea upotee kimziki. Yeye anasema ni kitu hikihiki ambacho kimewapoteza wengi kwenye gemu.

10. Ukipata kazi, basi ifanye kwa bidii. Hiki ni kitu ambacho Sugu anakieleza kwa kina kwenye kitabu hiki na anaonesha wazi kuwa kila kazi ambayo aliwahi kupata alikuwa akiifanya kwa moyo wake wote.
Aliwahi kuajiriwa kama mlinzi, lakini kwenye kitabu anaonesha kuwa alikuwa akiifanya kazi hii kwa kujituma na kwa moyo wake wote. Aliwahi kuajiriwa Uingereza kama mtu wa kubeba mizigo kwenye kampuni, kazi anayosema ilikuwa ngumu ila aliifanya kwa kujituma japo alikuwa haipendi kivile.

11. Sugu anaamini kuwa mtu mzuri wa kushirikisha naye ‘kimziki’ ni yule ambaye mna historia kubwa kutoka utotoni na siyo yule ambaye harakati za kikazi zimewafanya mkutane anasema hivyo baada ya vikundi vyote alivyokuwa akijiunga navyo kuishia njiani kwa baadhi ya watu kuacha muziki.  Mfano ni mshikaji wake BBG.

12. Sugu pia kaonesha kuwa kitu unachopenda sana ndicho huwa kinakuumiza sana. Yeye anasema wazi kuwa  kuna vitu vitatu ambavyo alikuwa anavipenda Sana.
Familia yake ya nyumbani
Muziki na
Mrembo mmoja aliyekuwa anaitwa Prude.
Ila hivi viwili vya mwisho vilimuumiza mara kwa mara na hasa mwaka 2002 alipostaafu mziki kwa kulazimika kufanya hivyo na wakati huohuo akawa ameachana na mchumba wake.

13. Sugu anatufundisha pia kutokuwa ving’anganizi wa maamuzi hata kama ni mabovu. Anaonesha hili kwa jinsi alvyoacha muziki na kwenda nje nchi. Ila akiwa huko alishauriwa kurudi kwenye gemu, kitu ambacho alikifanya kwa mara nyingine na aliporudi akawa ameweza kuendeleza harakati zake.

Kumbe ukifanya maamuzi, na baadaye ikatokea unataka kubadili hayo maamuzi (baada ya kuwa umejua kuwa  kuna maamuzi mengine bora ya hayo). Unaruhusiwa kubadili mtazamo. Siyo dhambi. Ila kwa maoni yangu mchambuzi; Ni dhambi kunga’ngania kitu kile kile hata baada ya kugundua kuwa uamuzi huo haukuwa sahihi.

14. Sugu anasisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na chanzo zaidi ya kimoja cha kukuingizia fedha. Anaeleza jinsi ambavyo muda mwingine alikuwa akihangaika na hasa ilipokuwa inatokea anafuria.

15. Ni muhimu sana kutafuta fedha na kuwa nazo. Bila ya kuwa na fedha utalazimika muda mwingine kufanya vitu hata kama vinakuumiza au vinaenda kinyume kabisa na misingi uliyojiwekea kimaisha. Mfano mzuri wa hili ni Sugu kukubali kurekodi albamu mojawapo na jamaa ambaye alikuwa akiuza kazi zake bila kumlipa vizuri.

Alifanya  hivyo baada ya kuwa anahitaji sana fedha za kwenda nje ya nchi ila hakuwa nazo. Hivyo, alilazimishwa kurekodi albamu na jamaa ambaye alikuwa anajua wazi kuwa anamwibia maana hilo ni sharti alilowewekewa. Aliambia kama unataka fedha, niachie albamu ili nikupe fedha.

Pia sugu kaeleza kisa kingine ambacho kilimfanya akiuke misingi yake, ila alilazimika kufanya hivyo, maana hakuwa na fedha. Ulikuwa uzinduzi wa albamu yake ya nne. Alilazimika kufanya kazi na watu wa Clouds, ambao yeye anasema kuwa hakuwa akiwapenda ila hakuwa na jinsi ambavyo angeweza kuzindua kazi yake bila wao. Hivyo, alilazimika kufanya hivyo, kitu kikichopelekea kulipwa kidogo sana na matarajio yake, na bado akasumbuliwabkwa kutolipwa fedha yake yote mpaka leo (leo hapo inamaanisha wakati anaandika kitabu; pengine sasa hivi watakuwa wameshamlipa)!

Ok kitabu hiki ni kizuri na kina mengi ya kujifunza ndani yake. Kitabu hiki kina kurasa 147, ambazo ni hakika huwezi kuzizungumzia kiundani kwenye uchambuzi mfupi kama huu. Kama utapenda kukisoma kitabu hiki, Niko tayari kukuchangia kiasi kidogo ili upate nakala yako. Kitabu hiki kinauzwa elfu 20. Binafsi nitakuchangia 5,000/- na wewe utalipia 15,000/- ila gharama za usafiri zitakuwa juu yako. Nitafanya hivyo kwa watu watatu tu.

Kwa hiyo basi kama utapenda kupata nakala yako kwa bei hiyo, tuwasiliane Sasa 0755848391.

Umekuwa nami,

GODIUS RWEYONGEZA

Hakikisha Umesubscribe kwenye Channel yangu ya youtube kwa KUBONYEZA HAPA

Jiunge na mfumo wa kupokea makala maalumu kwa njia ya barua pepe kwa KUBONYEZA HAPA

Jipatie nakala za vitabu vyangu vya kiswahili kwa KUBONYEZA HAPA

Kama ungependa kujifunza kuhusu uandishi kutoka kwangu wasiliana nami kwa 0755848391

kila la kheri


4 responses to “UCHAMBUZI WA KITABU CHA SUGU MAISHA NA MUZIKI. Mambo 14 niliyojifunza kwenye kitabu hiki kinachoeleza Maisha ya Sugu Kutoka Mtaani Mpaka Bungeni”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X