Hizi Hapa Ni Sababu Za Kwa Nini Unapaswa Kufanyia Wazo Lako Mwaka Huu Na Sio Kusubiri


Natumai kwamba unaendelea vyema. Ni takribani wiki nzima sasa nimekuwa nikiandika makala kuhusu wazo la biashara. Kila siku tumekuwa tunapata makala moja iliyojishosheleza na yenye ujumbe uliokamilika. Sasa leo nimerudi tena kwa lengo la kukueleza kwa nini unapaswa kufanyia wazo lako la biashara mwaka huu na sio mwaka mwingine. Najua kwamba ninachoenda kuandika hapa ni muhimu kwako endapo utakifanyia kazi. Kama unajua kwamba utasoma hapa ila ukaishia kusema kwamba huyu jamaa anaandika vizuri, basi ni bora kabisa usisome il usije ukapoteza muda wako. Mimi binafsi najali sana muda wako, maana najua kwamba muda ni mali. Sasa haina haja ya wewe kusoma hapa ukaishia kusema kwamba huyu jamaa kaandika vizuri wakati huyafanyii kazi yale unayojifunza hapa.

Sasa baada ya kusema hayo kuna sababu NNE za kwa nini unapaswa kuanza mwaka huu kufanyia kazi wazo lako.

MOJA NI Kwamba Usije Ukafa Na Hilo Wazo Lako. Ndio usiogope kwa sababu nimeongelea kifo. Hakuna mtu ambaye ameweka mkataba na kifo. Yaani, wewe hujui kwamba utakufa lini na kwenye hali gani. Na kwa sababu hujui kwamba utakufa lini, hakuna haja ya wewe kuendelea kuogopa kifo, badala yake weka nguvu kwenye kufanyia kazi wazo lako ambalo unalo leo hii.

Ujue unaweza ukawa na wazo ila ukawa hujui kwamba umebeba majibu ya watu wengi. Hivyo, ukifa na wazo lako unakuwa umekufa na majibu ya watu wengi. Ujue unaweza kuwa na wazo ila ukawa hujui kwamba umebeba ajira za mamilioni ya watanzania na watu wa dunia nzima, sasa ukifa na hilo wazo lako basi dunia itakuwa imekosa hiyo fursa uliyokkuwa umebeba kupitia wazo lako.

Ukitaka kunielewa kwenye hili hapa napenda tu nitolee mfano mdogo wa wazo la simu janja (smartphone). Hili lilianza kama wazo dogo kwenye kichwa cha mtu mmoja. Ila ni ukweli kwamba hakujua kwamba wazo hili litakuja kuwa wazo kubwa sana kwenye hii dunia ambalo lingewasaidia watu wengi kama ilivyo leo. Sasa hivi kuna watu maisha yao yote yapo kwenye simu moja tu. Yaani, kipato chote wanachoingiza kinategemea simu.

Wasipokuwa na hiyo simu, basi siku hiyo hawaingizi kipato. Hivi kwa mfano, huyu mtu aliyekuwa na wazo la kutengeneza simu angeamua kufa na wazo hilo unadhani ni watu wangapi hapa duniani wangeathirika kwa kukosa hizi simu? Bila shaka wangekuwa wengi sana. Na wewe inawezekana ukawa ni miongoni mwa hawa watu.

Sasa hapa ndipo nakuja kukwambia ukweli ambao hujawahi kuusikia sehemu. Nilikuwa sipendi kuusema ukweli huu nikiwa wa kwanza ila sina jinsi, lazima niuseme. Ukweli huu ni kwamba wazo ulilonalo ni lako ila sio la kwako. Iko hivi, wewe unaweza ukawa unajiona kwamba wazo hilo lililo bora basi ni la kwako. Ninachotaka ujue ni kwamba wazo linapitia kwenye kichwa chako ila sio kwamba wazo hilo linakuwa la kwako. Wewe unakuwa na wazo kwa ajili ya kuwasaidia watu wengine.

Utanielewa vizuri hapa kama nitakupa mfano ambao unakufaa. Bila shaka hapo ulipo umevaa nguo, tena nguo nzuri tu. Si ndio? Hivi unajua hizo nguo zilitengenezwa na nani? Hivi unamjua mtu wa kwanza kabisa kuwa na wazo la kutengeneza nguo? Alikuwa nani? Humjui. Ila kila siku unavaa nguo. Ni ukweli kwamba wazo la kutengeneza nguo lilikuwa ni wazo kwenye kichwa cha mtu ila akaamua kulifanyia kazi na leo hii wewe unavaa nguo. Wazo la nguo sio lako ila leo hii unafurahia kuvaa nguo na kupendeza.Tena ulivyo wa ajabu kila mara unafikiria kwenda kutafuta nguo ambazo ziko kwenye fashion ili usipitwe na wakati. Kama nakuona vile…

Sasa na wazo ndivyo lilivyo hivyo. Ukilifanyia kazi wazo lako utaweza kuwasaidia watu wengi zaidi. Ndio wengi zaidi, na hata wengine hutawajua kama wewe unavyoishi kwa kutumia mawazo ya watu wengine ambao huwajui. Kama bado huamini kwamba unatumia mawazo ya watu ambao huwajui basi ngoja nikujuze hapa.

Hivi unajuwa ni mtu gani alikuwa wa kwanza kuja na wazo la kutengeneza barabara? Ila si kila siku unatumia barabara?

Hivi unajua ni mtu gani alitengeneza runinga au redio? Ila si kila siku unavitumia vitu hivi? Intaneti je? Unajua ilitengenezwa na nani? Si unanufaika nayo? Bila shaka na wewe unaenda kulifanyia kazi wazo lako leo hii. Kiukweli unapaswa kujua kwamba kwa wazo lako hilo tu mimi hapa ninakudai.

Ndio ninakudai. Inawezekana wewe hapo una wazo la kuimba wimbo mzuri ila hata hujachukua hatua ya kuanza kuuimba. Na huo wimbo sio kwamba utakuburudisha wewe tu, bali utaburudisha jamii nzima nikiwemo mimi hapa na familia yangu. Sasa huoni kwamba unaninyima burudani kwa kukataa kuimba huo wimbo wako.

Inawezekana wewe hapo una wazo la kujenga hoteli nzuri. Na mimi kila siku nahangaika kutafuta hoteli nzuri ambapo nitaenda kutumia wikendi yangu vizuri, Kumbe hiyo hoteli unayo tu kichwani mwako. Kwa nini huifanyii kazi? Sipendi kabisa hii tabia yako ya kuwa na mawazo ukakaa nayo kichwani.

Au tuseme kwamba wewe wazo lako ni kuanzisha biashara. Ila sasa zimepita siku na hujalifanyia kazi kabisa wazo lako. Laiti kama ungekuwa umefanyia kazi wazo lako ungekuwa tayari umekuza biashaara yako kiasi cha kuweza kuajiri hata vijana kumi. Ila hao vijana wapo mtaani wanazurura kwa kukosa ajira na wazo la biashara, ambalo lingewaajiri unalo wewe ila hulifanyii kazi.

Cha kushangaza kila mara watu wakianza kusema kwamba hakuna ajira, wewe mwenywe unashiriki kusema kwamba kweli serikali haitoi ajira. Wakati wewe tu una biashara ambayo ilipaswa kuwa tayari imeajiri watu 10. Kwa nini unafanya hivyo? Aisee, mimi ninakudai. Ninakudai! Ndio ninakudai, kwa sababu, ya uzembe wako huo wa kutotaka kufanyia kazi wazo lako la biashara.

PILI, sitaki kusikia hii stori tena.

Aisee, kuna hii stori huwa siipendi. Siku ukikutana na mimi ukasema hii stori sitakuvumilia kabisa. Stori hii huwa inatolewa na wazee na watu wazima. Utawasikia wakisema, mtu fulani alianza kimasihala ila sasa hivi hashikiki. Au utawasikia wakisema kwamba, mtu fulani nilisoma naye ila sasa hivi tayari mtu huyu ni tajiri na ametengeneza utajiri mkubwa sana. Muda mwinginie utawasikia wakisema kwamba, mtu fulani alikuwa anaishi hapo tu na maisha ya kawaida ila sasa hivi ameshakuwa mtu wa viwango vingine.

Wakati hawa wazee huwa nawavumilia, ila wewe niseme tu kwamba sitakuvulia hata kidogo. Niwe tu mkweli. Yaani, hawa watu wengine hawawezi kuwa wanapambana wanafanyia kazi mawazo yao kila siku wewe umelala na unasubiri siku uje uanze kutupa stori kwamba ulisoma nao. Au kwamba walikuwa marafiki wako enzi za ujana. Hii stori haikubaliki kabisaa!

Haikubaliki kwa sababu sasa hivi una nguvu na uwezo wa kupambana na kuweza kufanya makubwa. hivyo hakuna haja ya wewe kuja kusubiri ili mambo yote yakae sawa sawia. Fanyia kazi wazo lako.

Siku moja nakutegemea wewe uwe unatoa stori ya kuhamasisha na kuwaonesha vijana njia kuwa ulikuwa na wazo, ukalifanyia kazi na sasa umeweza kufikia hatua fulani.

Tatu, kijana mchachari.Usipofanyia kazi wazo lako leo hii inawezekana kuna watu ambao wataenda kulifanyia kazi eneo jingine. Na hapa nipo siriazi kabisaa! Hivi hujawahi kusikia kuwa mtu alikuwa na wazo ila akachelewa hilo wazo likafanyiwa kazi na mtu mwingine. Kama hujawahi kusikia kitu kama hiki hapa ngoja nikupe tu mfano ambao utauelewa. Wazo la kutengeneza simu ya kwanza kabisa kama tunavyoifahamu leo hii linaelekezwa kwa  Alexander Graham Bell. Hata hivyo, kipindi hicho kulikuwa na watu ambao walikuwa na wazo la aina hiyo hiyo. Ila kwa sababu walichelewa kulifanyia kazi Alexander Graham Bell ndiye alikuwa baba wa uutengezaji wa simu. Japo walikuwepo wengine wenye wazo ila hawakuchukua hatua.

Huwa nayapenda sana magazeti na vyombo vingine vya habari. Maana ikitokea mtu kafanya kitu kizuri. huwa unakuta kabisa kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti wameandika kwamba KIJANA MACHACHARI AMEFANYA KITU HIKI HAPA. Sasa kama wewe hutachukua hatua kulifanyia kazi wazo lako. Basi kuna siku utakuja kusikia kwamba KIJANA MACHACHARI NCHINI CHINA AMEGUNDUA…

Halafu ukija kufuatilia utagundua kwamba kitu alichogundua ndilo lilikuwa wazo lako ambalo wewe mwenyewe ulitaka kulifanyia kazi. Sasa kwa nini usubiri kuja kuona kwenye magazeti kwamba kijana machachari sehemu nyingine amefanyia kazi wazo kama lako sehemu nyingine. Kwa nini hao watu wengine wasikuone wewe hapo kwenye magazeti ukiwa umeweza kuvumbua kitu ambacho ni wazo lako kwa sasa. Kwa nini wasikuuone ukiwa umeweza kufanikisha ndoto yako kubwa ambayo unayo. Yaani, kama utasoma hapa na ukabaki hivyo hivyo bila kulifanyia wazo lako, basi utajikwamisha tu.

Nne thamani ya mawazo inaongezeka unapolifanyia kazi wazo lako. Umeshawahi kuona watu wanasema kwamba wazo fulani lina thamani ya milioni kadhaa za hela? Nakuuliza, umeshawahi kuona kitu kama hicho. ndio najua kuwa ni ukweli kuwa kuna baadhi ya watu na taasisi ambazo huwa zinawekeza kwenye wazo au mtu mwenye wazo, ila ninachotka kukwambia ni kwamba,watu watakuwa tayari kuwekweza katika katika wewe pale tu wanapokuwa wanajua mwelekeo wako. Pale wanapokuwa wanajua kwamba mtu huyu akiwa na wazo lazima tu atalifanyia kazi na litakuja kwenye uhalisia, hapo ndipo watu watakuwa tayari kuwekeza kwenye wazo lako kabla hata hujaanza kulifanyia kazi/

Mwaka juzi Donald Trump alipata adha ya kufungiwa na mitandao yote ya kijamii. Na mitandao mingine ilimfutilia mbali kabisa. baada ya matukio hayo Donald Trump aliazimia kuwa angeazisha mtandao ambao ungekuwa mshindani wa mitandao ya kijamii iliyopo. Hivyo, wazo lake lilikuwa ni hilo. Kuanzisha mtandao ambao utakuwa mshindani kwa mitandao ya kijamii iliyopo. Kwa sasa wazo lake hilo tu linatathiiwa kuwa na thamani ya dola bilioni 10. Na hajaanza kulifanyia kazi.

Sasa swali langu kwako wewe ni Donald Trump? Nakuuliza? Usije ukaanza kusema, ooh unajua kama Donald Trump aliweza kufanikisha hilo mimi nitashindwaje? Wewe umewahi kufanya kitu gani kikubwa ambacho kinafahamika kwenye jamii. Umewahi hata kuitisha watu mcheze ngoma ya mseleleko wakaja? Natania tu.

Ila ninachotaka kukwambia ni kwamba wazo la Donald Trump limekuwa na thamani hivyo kwa sababu tu yeye ameshafanya vitu vingi ambavyo vinaonekana. Sasa wewe na wazo lako hilo unapaswa kuanza kulifanyia kazi la sivyo, nakwambia kwamba halitakuwa na thamani yoyote ile. Sijui unanielewa?

Ukilifanyia kazi wazo unalipa thamani, hata ukiwaita waje kuwekeza, kweli watakuwa wamekuaja kuwekeza kwenye kitu ambacho kinaonekana. Wenyewe tu watakuwa wanajivunia kufanya hivyo.

Kwa leo acha niishie hapa,

Kitu kikubwa cha kuondoka nacho kwenye makala ya leo ni kwamba unapaswa kuanza kufanyia kazi wazo lako, tena unapaswa kuanza kulifanyia kazi leo hii. Kila la kheri

Umekuwa nami,

GODIUS RWEYONGEZA

Hakikisha Umesubscribe kwenye Channel yangu ya youtube kwa KUBONYEZA HAPA

Jiunge na mfumo wa kupokea makala maalumu kwa njia ya barua pepe kwa KUBONYEZA HAPA

Jipatie nakala za vitabu vyangu vya kiswahili kwa KUBONYEZA HAPA

Kama ungependa kujifunza kuhusu uandishi kutoka kwangu wasiliana nami kwa 0755848391

kila la kheri

, , ,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X