AMSHA UUNGU ULIO NDANI YAKO: Sifa 3 Za Kimungu Unazopaswa Kuzitumia Kuanzia Leo


 

Mwaka 2017 nilipata kusoma kitabu cha FROM VICTIM TO VICTOR. Nilipata kujifunza mengi sana Kutoka kwenye kitabu hiki kuliko unavyoweza kufikiria.

Kitabu hiki kilichoandikwa na Mzimbabwe Joseph C. Musharika kina mafunzo mengi ambayo na wewe yanaweza kubadilisha maisha yako. Mwandishi amezaliwa katika familia ya kikristo kama ilivyo asilimia kubwa ya Waafrika. Kalelewa na kupewa makuzi na maadili ya kikristo na baadaye kwenye maisha yake akawa mwijilisti.

Kitu kimoja kilichoanza kumshangaza mwandishi ni kuona jinsi wakristo walivyokuwa hawatumii uwezo wao ipasavyo, walivyokuwa wanalaani utajiri na kuishi maisha ya kawaida.

Hivyo mwinjilisti Joseph C. Musharika akaamua kuwa ataishi maisha ya tofauti, atajenga utajiri na kutumia uwezo wake kadiri awezavyo.

Baada ya miaka mingi ya kufanya hivyo mwandishi akaona siyo vibaya nikiandika kitabu ili Waafrika wenzangu waweze kunufaika, maana imeandikwa kwamba watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.

Kitabu chake cha From Victim To Victor amekigawa kwenye sehemu kuu mbili.

Sehemu ya kwanza ya kwanza ameiita KWA SURA NA MFANO WAKE na sehemu ya pili ndiyo KUTOKA UHANGA MPAKA USHINDI (From victim to Victor).

SEHEMU YA KWANZA YA KITABU: KWA SURA NA MFANO WAKE

Mwandishi kaanza sehemu hii  kwa kueleza jinsi ambavyo tumeumbwa kwa sura na mfano wa mwenyezi Mungu na tuna uwezo mkubwa kuliko vile tunavyoweza kufikiri.

Kitu kimoja kilichonishangaza kutoka kwa mwandishi ni namna anavyotafsiri ile stori mnara wa babeli. Kabla yake na baada yake sijaona mtu ambaye anaitafsiri kwa kina na kwa namna ya upekee hivyo. Na kwa kuwa somo la leo nataka tuuone jinsi ya kuamsha uungu ulio ndani yako basi nitaenda na hiki kipengele cha mnara wa Babeli.

Kama wewe siyo mkristo utanisamehe, ila andiko la leo lina mazuri ya wewe kujifunza pia. Mpaka hapo naomba uniruhusu kwanza niweke stori ya mnara wa babeli, kama ilivyoelezwa kwenye kitabu cha MWANZO 11:1-9, kisha niendelee;

Kwanza, watu wote duniani walikuwa na lugha moja na walitumia maneno yaleyale. Basi, ikawa watu waliposafirisafiri kutoka mashariki, walifika katika nchi tambarare huko Shinari, wakakaa. Kisha wakaambiana, “Haya! Na tufyatue matofali, tuyachome moto vizuri.” Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, “Na tujijengee mji na mnara ambao kilele chake kitafika mbinguni ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.” Ndipo Mwenyezi-Mungu akashuka chini kuuona mji huo na mnara walioujenga binadamu.

Mwenyezi-Mungu akasema, “Tazama, watu hawa ni taifa moja na wote wana lugha moja; huu ni mwanzo tu wa yale watakayoyafanya. Lolote wanalokusudia kulifanya watafanikiwa.

Haya, na tushuke chini na kuivuruga lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.” Hivyo, Mwenyezi-Mungu akawatawanya mahali pote duniani, nao wakaacha kuujenga ule mji. Mji huo ukaitwa Babeli, kwa sababu huko ndiko Mwenyezi-Mungu alikoivuruga lugha ya dunia yote, na kutoka huko akawatawanya watu kila mahali duniani.

Swali la kwanza mwandishi analouliza Ni je, wangeweza kujenga mnara unaofika mbinguni? Mimi nakumbuka nilisema wasingeweza, hii ni kutokana na uelewa niliokuwa nao tangu mwanzo. Lakini mwandishi katika hali ya kushangaza alisema wangeweza na hiki Kitu ndicho kinatuleta kwenye point yetu ya kwanza kwa siku ya leo itakayokusaidia wewe kuamsha uungu ulio ndani yako.

 

#1. UMOJA

 

Mwandishi anasabhawa jamaa wangeweza kwa sababu walikuwa na umoja.

Rejea: Kwanza, watu wote duniani walikuwa na lugha moja na walitumia maneno yaleyale

Watu wote walikuwa na umoja na lugha waliyoitumia ni moja. Yaani, walikuwa wanaongea wanaelewana. Walikuwa wanapanga na kufikia muafaka. Hivyo, ndivyo walivyokuwa wanaishi.

Umoja haujawahi kufelisha watu hata siku moja, labda kama hao watu walikuwa na umoja feki. Ndio maana hata siku hizi tunasikia Kuna misemo kama umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, kwa pamoja tunaweza. Akina mama tushikamane n.k.

Hii yote ni kuonesha kwa namna ambavyo umoja unaweza kufanya makubwa. Ukitaka kuwagawa watu ondoa ule umoja uliokuwepo. Ukitaka kuijenga nchi, waunganishe watu, na ukitaka kuisambaratishe acha watu wapigane wenyewe.

Mwandishi amasema Mungu ni mmoja, ndio maana kwenye Biblia unakutana na maneno kama na tumuumbe mtu kwafano wetu. (Mwanzo 1:26)

Kwa hiyo basi kama unataka kuamsha uungu ulio ndani yako jenga umoja kwanza. Jenga umoja kati yako na familia yako, umoja Kati yako na wafanyakazi wako, au wenzako, na kikubwa zaidi umoja Kati yako mwenyewe.

Umoja haujawahi kufelisha mtu hata siku moja.

Labda unaweza kusema kwa nini sasa hawakuweza kufika huko mbinguni? Kwa Leo naomba niseme Kama mwandishi alivyosema: hakukuwa mpango wa Mungu wake pale, ila uwezo wa hao watu kufika mbinguni ulikuwepo ndio maana Mungu mwenyewe aliona afadhali achanganye lugha yao. 

Rejea: Tazama, watu hawa ni taifa moja na wote wana lugha moja; huu ni mwanzo tu wa yale watakayoyafanya. Lolote wanalokusudia kulifanya watafanikiwa

Hayo hapo juu ni maneno ya Mungu. Mungu anasema watu hawa ni taifa moja,  na wana lugha moja. Huu ni mwanzo tu wa Yale watakayoyafanya. Maana hapo badaye wangeweza kufanya makubwa zaidi ya hapo. Lakini Mungu anasema sentensi nyingine yenye uzito zaidi anaposema. Lolote wanalokusudia kukifanya wafafanikiwa.  Lolote wanalokusudia watafanyaje….?

Naomba nisisitize tena juu ya umoja. Kama unataka kufanya makubwa zaidi. Jenga umoja maana lolote utakaloamua kufanya, utafanikiwa?

 

#2. UBUNIFU

Hivi ni nani aliyewafundisha hawa jamaa kufyatua tofali, ni chuo gani hasa kiliwafundisha kujenga ghorofa? Hawa jamaa walikuwa wabunifu. Vitu ambavyo watu siku hizi wanakaa darasani kujifunza, hawa jamaa walikuwa wanavijua kwa kubuni.

kile mtu kapewa vinasaba vya ubunifu ndani yake. tatizo la watu wengi ni kwamba hawataki kuutumia huo ubunifu waliopewa. wewe pia umepewa huo ubunifu. ni jukumu lako wewe kuhakikisha kwamba unaeda mbali zaidi na kuutumia. u

 

#3. Kuwa na NDOTO kubwa

Hawa jamaa walikuwa na ndoto kubwa haswa. Ndoto ya kufika wapi? Mbinguni. Kwa sasa usiniulize mbingu iko wapi. Ila walau ninachotaka ufahamu ni kuwa walikuwa na ndoto kubwa. Na walikuwa hawapo tayari kurudi nyuma.

Wewe pia unapaswa kuwa na ndoto kubwa, kubwa sana unazozifanyia kazi.hapo ndio utaweza kuamsha uungu ulio ndani yako. Ndoto kubwa zitakusukuma wewe kufanya kazi zaidi na kutumia uwezo wako kwa viwango vikubwa.

Kwa ndoto kubwa tu walivyokuwa nayo hawa jamaa, Mungu alilazimika kushuka kutoka mbinguni ili aone kile walichokuwa wanataka kufanya. 

Rejea: Ndipo Mwenyezi-Mungu akashuka chini kuuona mji huo na mnara walioujenga binadamu

wewe umewahi kusikia au kuona wapi Mungu anashuka kutoka mbinguni ili kushuhudia ndoto kubwa waliyokuwa nayo watu? 

Sasa na wewe kuanzia sasa anza kuwa na ndoto kubwa ambazo utazifanyia kazi.  Sidhani kama Mungu atashuka kutoka mbinguni ili kushudia ndoto yako, ila nina uhakika kwamba uking’ang’ania kuifanyia kazi ndoto yako. Mungu atakuwa pamoja na wewe na utaweza kuifanikisha.

Kma na wewe una ndoto kubwa ya kufika mbali kwenye maisha yako, nashauri usome kitabu JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO. Utajifunza mengi ya kukusaidia wewe kuweza kuzifikia ndoto zako. kukipata wasiliana na: 0755848391 sasa hivi

Kwa leo niache niishie hapo. Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki jiunge na mafunzo yetu yanayotolewa kwa njia ya barua pepe.  Uchambuzi wote wa kitabu hiki utatolewa huko. BONYEZA HAPA kujiunga.

Umekuwa nami

Godius Rweyongeza

0755848391

Morogoro-Tz

 


5 responses to “AMSHA UUNGU ULIO NDANI YAKO: Sifa 3 Za Kimungu Unazopaswa Kuzitumia Kuanzia Leo”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X