Uchambuzi Wa Kitabu Cha 5 Langues Of Love


Kitabu: The 5 Languages of Love
Mwandishi: Cary Chapman
Mchambuzi: Hillary Mrosso
Mawasiliano: +255 683 862 481

Ukiona hutaki kusikia chochote kuhusu upendo, mapenzi, mahusiano na maneno mengine ya kufanana. Basi ujue unahitaji sana kusoma kitabu hiki. Ndugu msomaji wa uchambuzi wa kitabu hiki, nakuahidi hiki ni kitabu bora sana kwako kukisoma. Mwandishi wa kitabu hiki amekiandika baada ya shuhuda nyingi za mafunzo aliyokuwa anayatoa sehemu mbali mbali duniani. Kitabu hiki kimekuwa msaada kwa watu wengi sana, kinaweza kuwa msaada kwako pia. Nimejitahidi kukisoma kitabu hiki kwa kina sana, nimekuandalia baadhi ya mambo muhimu niliyoyaandika kwa lugha nyepesi, nina uhakika lazima utapata vitu muhimu sana vya kukusaidia. Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu. The 5 Lnaguages of Love; The Secret to Love that Lasts.

 1. Upendo, mapenzi, mahusiano na ndoa ni mambo yanayojadiliwa na kuandikwa sana kwenye magazeti, vitabu, na kuongelewa sana katika vyombo vya habari kama vile redio televisheni na majukwaa mengine makubwa.
 2. Upendo una lugha zake kulingana na tafsiri ya kila mtu, hii ni kutokana na makuzi, malezi, na utamaduni tulio nao ndio hutoa tafsiri ya mtu kupenda au kupendwa.
 3. Tunahitaji uelewa sahihi wa lugha ya upendo ambayo itaeleweka kwa yule anayepokea upendo. Kwa sababu sio kila kitu unachomfanyia unayempenda atatafsiri ni upendo au anapendwa.
 4. Uelewa wa lugha sahihi kwa mwenza wako ndio itakayofikisha ujumbe wa upendo, bila kujua lugha sahihi mnaweza kupishana sana na kupelekea ndoa au mahusiano kuvunjika.
 5. Upendo una lugha zake kulingana na tamaduni, malezi na maeneo watu walipo ishi.
 6. Sio kila unachofikiri wewe ni upendo itakuwa ni upendo kwa mweza au yule unayemfanyia jambo hilo ambalo unafikiri ni upendo.
 7. Kwasababu tunatofautiana katika makuzi na malezi, tafsiri za kupendwa na upendo baina yetu zinaweza pia kuwa tofauti kabisa.
 8. Utofauti wa lugha tunazoongea ni asili ya mwanadamu, lakini kama tunataka kufikisha ujumbe wa upendo kwa wale tuwapendao tunatakiwa kujifunza lugha yao kwanza.
 9. Mfano, kama mweza wako anaelewa kiswhili na wewe unajaribu kumwambia lugha za upendo kwa lugha ya kichina, ni wazi kabisa hatakuelewa.
 10. Njia nzuri ya kufikisha ujumbe wa upendo kwa yule umpendae ni kujifunza tamaduni na lugha yake ya upendo, yaani kujifunza namna anavyotafsiri upendo au kupendwa.
 11. Unaweza ukawa na hisia zote za upendo lakini zikashindwa kueleweka kwa mwenza wako kutokana na mwenza wako kutoelewa lugha yako ya kwanza ya upendo au kupendwa ni ipi.
 12. Haijalishi utatumia nguvu kasi gani kuonyesha upendo kwa mwenza wako, kama mwenza wako anaelewa tofauti kamwe hamuwezi kupendana inavyotakiwa wala kuelewana.
 13. Kwa mfano, unaweza kudhani ukimwambia maneno mazuri mwenza wako inaweza kuwa ni upendo au anaweza kudhani unapenda, inaweza isiwe hivyo mara zote, maneno yanaweza yasiwe kiashiria cha kwanza cha upendo kwa mwenza wako, hvyo unatakiwa kujua ni kitu gani ni kiashiria cha upendo kwa mwenza wako.
 14. Kuna wengine upendo au kupendwa wanatafsiri katika kufanyiwa vitu fulani na wenza wao, labda kuosha vyombo, kupika, kutandika kitanda au kufanya usafi.
 15. Kuna wengine kutoa au kupokea zawadi ni kishiria namba moja cha upendo au kupendwa, lakini kwa wengine sio kiashiria namba moja cha upendo au kupendwa.
 16. Mfano, mwengine atajihisi anapendwa endapo atapata muda wa kukaa na mweza wake na kujadili mambo yao pamoja, kwa hivyo kiashiria namba moja kwa baadhi ya watu ni muda anaopata wa kukaa na mwenza wake.
 17. Unaweza kufanya kila kitu unachojua ni upendo kwa mweza wako, kama humpi muda wa kukaa naye pamoja mtashangaa mnaanza kugombana na mmoja wenu anahisi hapendwi.
 18. Kitu muhimu ni kujua kwa mwenza wako ni jambo gani au kitu gani akifanyiwa na mwenza wake atatafsiri haraka kuwa anapendwa au ni upendo. Maana sio kila kitu utamfanyia mwenza wako atatafsiri ni upendo au kupendwa, hivyo ni muhimu tukajifunza ili kuboresha mahusiano yetu na ndoa zetu.
 19. Mwandishi wa kitabu hiki ameeleza kuwa kuna aina tano za lugha za upendo, lakini zinaweza kuwa katika lahaja mbali mbali, lakini kuu ni tano.
 20. Muhimu wa kitabu hiki ni kutusaidia kujua aina hizi tano za lugha za upendo, na kung’amua ni ipi ndio lugha sahihi kwa mwenza wako na kuifanyia kazi.
 21. Kila mtoto amelelewa kwenye makuzi ya kipekee yanaweza yasiwe sawa na watoto wengine, hivyo hata namna yake ya kupokea upendo ni tofauti na watoto wengine.
 22. Hisia za upendo kwa watoto hazifanani, kuna wengine walionyeshwa na kupewa upendo na wazazi wao, kuna wengine hawakupata hio nafasi ya kuonyeshwa upendo na wazazi au walezi wao, hii inaweza kuleta tafsiri tofauti sana kwenye ndoa, maana mara nyingi tunawafanyia na kuwaonyesha wenza wetu yale tuliojifunza au kuyaona kwa wazazi wetu.
 23. Watoto waliolelewa katika upendo kutoka kwa wazazi wao watakuwa watu wa kujiamini na kujikubali, hivyo inamfanya mtoto kufanya mambo makubwa na kutimiza majukumu muhimu kwenye maisha yake.
 24. Watu wengi sasa wanatafuta hisia za upendo na kupendwa kutoka kwa wenza wao, bahati mbaya au nzuri unaweza kukuta mwenza wako hajali kabisa hisia zako, na hapo ndipo kunakuwa na vita ndani ya ndoa.
 25. Hali ya kutojiamini iliyopo kwa watu inaweza kuwa ilichangiwa na kukosekana kwa upendo au kutoonyeshwa upendo na wazazi au walezi waliotulea kipindi wakiwa watoto.
 26. Hisia za upendo ni muhimu sana kwa watoto wetu, na pia zinatakiwa kuonyeshwa wazi baina ya wanandoa. Hii itamsaidia mtoto kuona namna ya kumpenda na kumjali mwenza wake.
 27. Vijana wengi wameingia kwenye tabia hatarishi na msongo wa mawazo kwa sababu ndani ya mioyo yao ambako kulitakiwa kukaa upendo, na kukubaliwa na wazazi au walezi wao ipo wazi au imejazwa na mambo hasi yanayoleta majuto na hisia hasi.
 28. Kama wazazi watajali makuzi ya watoto wao, basi watazingatia baadhi ya viashiria kutoka kwa watoto wao ambavyo ukiwafanyia watoto wanaona na kutafsiri kama upendo kutoka kwa wazazi.
 29. Mfano, mtoto anaweza kutaka kucheza na mzazi wake, mweingine atapenda kubebwa na kushikwa na mzazi wake, mwingine atapenda kupewa zawadi na wazazi wake, mwingine atapenda kwenda matembezi au kutembea na wazazi wake, hayo yote ni mahitaji yanayotafsiriwa kama upendo endapo mtoto husika atafanyiwa.
 30. Tunatakiwa kuwa waangalifu namna tunavyowalea watoto wetu, sio wote wataona tunaowanyesha upendo kwa kuwaletea zawadi, au kutembea pamoja, elewa lugha sahihi ya mtoto wako ndio umfanyie anachotamani kufanyiwa.
 31. Namna sahihi ya kuwasilisha upendo wako ni kujua hasa kitu gani anachohitaji mwenza wako ambacho kwake akifanyiwa ndio atajua anapendwa na kuthaminiwa.
 32. Kushindwa kuwasilisha tafsiri sahihi ya upendo kwa mwenza wako haimaanishi kuwa wewe ni mshindwa au haupendi, kila kitu kinawezekana endapo tutakuwa tayari kujifunza namna bora na sahihi ya kuwasilisha upendo au hisia za upendo kwa wenza wetu.
 33. Hata watoto waliokuwa bila hisia za upendo au kupendwa wanaweza kufanyia kazi hisia zao za upendo na wakaanza kupenda na kupendwa. Kwasababu wameshakuwa watu wazima na wamejifunza jambo hili.
 34. Kama unahisi haupendwi na mwenza wako ujue mnatofautiana kwenye tafsiri sahihi ya upendo baina yenu. Inawezekana mnaongea lugha za kigeni hivyo hakuna maelewano kwenye mahusiano yenu.
 35. Mara nyingi tunajitahidi kuonyesha upendo lakini unakuta ujumbe wetu wa upendo haufiki au haupokelewi kwasababu tumepishana lugha za upendo na kupendwa.
 36. Endapo tutagundua na kuanza kuongea lugha sahihi ya upendo kwa mwenza wetu, itasaidia sana kuboresha na kudumisha hisia za mapenzi na upendo na ndoa zitadumu kwa muda mrefu.
 37. Hisia za upendo na kupendwa hazitakiwi kuishia kwenye hanimuni (fungate), zinaweza kuendelea kudumu endapo utangundua na kujifunza lugha nyingine sahihi za upendo.
 38. Ni vizuri tukaacha kungangania lugha zetu za asili za upendo endapo wenza wetu hawatafaidika nazo, tunapaswa kujifunza namna nzuri ya kuwasilisha hisia zetu za upendo kwa lugha anayoielewa mwenza wako.
 39. Wanasaikolojia wanasema matamanio makubwa ya watu ni kujisikia wanapendwa, mtu akipenda au akipendwa anaweza kufanya mambo makubwa sana. Kwa sababu upendo una nguvu sana, upendo unafanya watu wapandishe milima, wavuke mito, mabonde, baharini na wavuke majangwa.
 40. Upendo umefanya watu wavumilie yasiyovumilika na wafanye mambo yasiyoelezeka kirahisi, upendo umewafanya wengi kuwa hai, na wengine kufariki, upendo umewagharimu wengine maisha lakini pia umewapa wengine maisha.
 41. Hata Mtume Paulo aliwahi kuandika kuwa mafanikio yote hata kama ni makubwa kiasi gani kama hayajatokana na ushawishi wa upendo ni bure.
 42. Unaweza kuwa na Imani kubwa au matumaini makubwa, lakini tunaambiwa haya yote ni bure kama hatuna upendo, upendo unashinda yote.
 43. Watu wanadiriki kufanya mambo ya kutisha na ya kuhuzunisha kwasababu wanaamini ndio upendo.
 44. Wakati mwingine watu wanaweza hata kubadili tabia zao kwasababu ya kuonyesha upendo.
 45. Kwa kila mtoto kuna tanki la hisia ambalo lipo wazi linahitaji kujazwa hisia za upendo na kupendwa. Kwa bahati mbaya mtoto anaweza kuwa hata mtu mzima bila tanki la hisia za upendo kujazwa, hivyo anakuwa hasi na kushindwa kuwasaidia wengine.
 46. Tabia mbaya tunazoziona kwa watoto wetu zinachangiwa na kukosa hisia za upendo na kupendwa na wazazi wake. Yaani kuna uwazi upo ndani ya moyo wake ambao ili maisha yake yaje kuwa mazuri anahitajika kujaza hisia za kupendwa na upendo.
 47. Ndani ya moyo wa mwanadamu kuna njaa na kiu ya kutamani kupendwa na kukubalika na mwanadamu mwenzake.
 48. Ili ndoa iende vizuri inahitajika uwazi uliopo ndani ya moyo ujazwe hisia za mapenzi, upendo na kupendwa ili kuifanya ndoa kudumu.
 49. Kama gari ambalo linahitaji mafuta ili liweze kwendelea na safari, ndivyo ilivyo kwenye ndoa, hisia za kupenda na kupendwa ni muhimu sana ili wanandoa waendelee kufurahia ndoa yao na mahusiano yao.
 50. Wakati mwingine ukiwa umezama kwenye lindi la mahaba na mapenzi hasa kipindi cha uchumba, unaweza kuona kila kitu kipo sawa na kitakuwa sawa tu na wala hakuna changamoto inayoweza kutokea. Ukweli ni kwamba ndoto hizi huwa hazidumu baada ya kuingia kwenye ndoa.
 51. Kuna wakati hisia za mapenzi na upendo zinaweza kukoma, na hapo ndipo wana ndoa wanarudi kwenye maisha yao halisi, kwenye rangi zao halisi hapo ndipo inahitajika kujifunza kupenda upya kwa namna ambayo wote mtafurahia mahusiano yenu.
 52. Ukiwa kwenye hisia kali za mapenzi na kupenda ni ngumu kukubali ushauri na utaona mmekamilika wewe na mwenza wako, unaweza usione kasoro hadi pale mambo yatakapo badilika.
 53. Utafiti unaonyesha kuwa mahusiano ya kimapenzi na mahaba hudumu kwa miaka 2 kama yapo wazi lakini inaweza kwenda zaidi ya miaka miwili kama mapenzi ni ya sirini.
 54. Uzoefu unaonyesha baada ya hisia za mapenzi, mahaba na upendo kukoma ndipo inapokuja watu kuanza kutoelewana, kushindana, hata ndoa kuvunjika na wengine kutoa au kudai talaka.
 55. Ikifikia hatua hii kupenda hakuwi tena kwenye hisia tu, bali ni uchaguzi, yaani unaamua tu kufanya uchaguzi wa kumpenda au kupenda. Ikifikia hatua hii ndio upendo wa kweli unapoonekana na kuhitajika.
 56. Unatakiwa kupendwa na mtu ambaye amechagua kukupenda na ambaye ameona kitu cha thamani ndani yako na kuamua kukupenda. Yani kuna kitu cha kupenda kwenye maisha yako.
 57. Kama kupenda ni uchaguzi basi unaweza kupenda tena hata baada ya hisia za mapenzi au upendo kuondoka au kuisha.
 58. Kama mtajazilizana upendo kwenye uwazi ulio ndani yenu, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia malengo yenu makubwa mliyojiwekea kwenye maisha.
 59. Kama wanandoa hawatafikia kupendana na kuona kama wanatumika tuu, hii italeta hisia mbaya na utaona dunia ni chungu, hakuna kitakachokupendeza.
 60. Njia moja wapo ya kuelezea upendo ni kutumia maneno yanayojenga kwa mwenza wako, mfano mfalme Suleiman alisema ulimi una nguvu ya uhai na nguvu ya kifo. Tumia nguvu ya ulimi wako kujenga.
 61. Dhana kuu ya upendo imejikita katika kufanya vitu ambavyo mwenza wako au rafiki yako atatafsiri kuwa anafanyiwa upendo na sio kuangalia mambo yako binafsi.
 62. Pale tunapopokea maneno mazuri ya upendo tunahamasika na kuwa na fikra chanya kwetu na kwa wengine pia.
 63. Kumtia mtu moyo na kumuonea huruma inahitaji kuona mambo kwa namna anayoyaona yeye. Hivyo ndiovyo inavyotakiwa kuwa katika ndoa na mahusiano.
 64. Wengi waliopo kwenye mahusiano yenye changamoto wamezoa kusikia na kuambiwa maneno hasi yanayopelekea kujihukumu, na kujisikia mwenye hatia, manaeno ambayo hayana hata tone la hisia za upendo.
 65. Maneno tunayowaambia wapenzi wetu yanatakiwa kuwa maneno chanya na yenye kujenga, maneno ya kuwatia moyo na kuwainua ili waendelee kujikubali na kufanya mambo yao kwa mtazamo wa upendo.
 66. Maneno kama najua, nipo pamoja na wewe, najali, naweza kukusaidia jambo, ni maneno ya kuinua na ya kumfanya mtu ajione wa thamani. Yatumie kandri uwezavyo kumsaidia mwenza wako.
 67. Wengi wetu tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa kuliko tuliyowahi kufanya, lakini kinachoturudisha nyuma ni kukosa ujasiri, ukiwa na mwenza au mpenzi anayekuamini na kukutia moyo inaweza kuwa ndio kichocheo cha wewe kuanza kuchukua hatua kubwa za maendeleo na mafanikio.
 68. Kama tumedhamiria kuishi katika mahusiano ya kimapenzi tunatakiwa kufahamu upande wa mwenza wako, ni kitu gani anajali, anapenda na anachotafsiri kama upendo endapo atafanyiwa.
 69. Tunapofanya maamuzi ya kutembea pamoja kama wapenzi tunatakiwa kufahamu kuna mambo ya nyuma ambayo tunatakiwa kuachana nayo, pia tunatakiwa kusamehe maeneo ambayo tuliumizwa na kuwaumiza wegine. Haya yatawezekana endapo tutaamua kusamehe.
 70. Tujifunze kuacha mabaya ya nyuma yapite, hata kama uliumizwa namna gani, bado unaweza kuamua kuishi maisha yako yaliyosalia kwa furaha na kuacha kurudia yaliyosababisha ukaumia.
 71. Wakati mwingine maneno ya kutia moyo yakiandikwa na kusomwa kwa kujirudia rudia yana nguvu sana ya kubadilisha mwenendo wetu wa maisha. Hivyo jifunze kuandika maneeno mazuri ili urudie kuyasoma mara kwa mara kwa faida yako na ya mpenzi wako.
 72. Kuonyesha upendo na kusifia mwenza wako mbele ya rafiki zako au wazazi wake inaweza kukuongezea kitu cha tofauti kwenye mahusiano yenu. Jifunze kufanya hivyo inapobidi ili kuboresha mahusiano yako.
 73. Wazazi wa mweza wako watajiona wenye bahati kwa kupata mtu sahihi anayempenda mtoto wao, hivyo na wao watakupenda na kukuheshimu, maana umeonyesha wazi wazi umempenda mtoto wao mbele yao.
 74. Angalia ni maeneo gani mwenza wako au mpenzi wako anafanya vizuri na umpongeze kwa jitihada zake, hii itamfanya ajitahidi kuboresha maeneo ambayo hafanyi vizuri.
 75. Waambie na watoto wako ni jinsi gani baba yao au mama yao anafanya mambo yake vizuri. Fanya hivyo wakati mzazi huyo yupo na wakati hayupo. Hii itaongeza upendo na mshikamano kwenye familia na ndoa.
 76. Andika mashairi mazuri ya kumsifia mpenzi au mwenza wako, kama huwezi kutunga mashairi tafuta kadi zenye ujumbe mzuri kisha mpe mwenza wako. Angalia kila neno lenye thamani na kama unaweza kuongezea mengine fanya hivyo kuelezea ni jinsi gani unampenda na kumjali mweza wako.
 77. Jifunze kuelezea ni jinsi gani mpenzi wako au mwenza wako ana thamani kubwa kwako, tumia maneno, msikilize na yote yafanyike kwa hisia za upendo.
 78. Kama mwenza wako anajali sana muda wa kuwa naye (quality time), fanya hivyo kwa kumaanisha kabisa, mpe muda mwenza wako na usijihusishe na kitu kingine mnapokuwa pamoja, achana na simu, TV, magazeti au mambo mengine yanayoweza kuwaondolea utulivu.
 79. Unapokuwa na mwenza wako, muwe kama ndio mnachumbiana na sio kama watu waliokaa kwenye ndoa muda mrefu na kuchokana, yani kila mtu anaaangalia upande wake badala ya kuangaliana uso kwa uso.
 80. Kuwa pamoja au kuwa na umoja usiogawanyika yaaani focused attention, inahitajika sana kwenye mahusiano na ndoa.
 81. Kuwa pamoja na mwenza wako inaweza kuwa pia ni kuwa na jambo la kufanya kwa pamoja, maongezi ya maisha yenu ya baadaye, na kupanga mipango yenu yote pamoja; jambo hili linapofanyika linaongeza hisia za upendo na kupendana.
 82. Wengi wetu tumejifunza tunapokuwa na changamoto tunaichambua na kutoa majibu wenyewe bila kushirikisha mwenza wako. Kwenye ndoa au mahusiano mambo hayaendi hivyo, kila kitu kinatakiwa kiende kama mahusiano yanavyoenda na sio kama miradi itayotakiwa kukamilika.
 83. Mahusiano yanahitaji kuhusisha na kushusiana, kuelewa na kusikilizana, kupokea mitazamo, hisia, matamanio na mawazo ya mwenza wako. Mambo ambayo yanahitaji kufanyika kwa upendo na uvumilivu.
 84. Unapoongea na mwenza wako au mpenzi wako jifunzeni kuangaliana usoni, na uzuie akili na mawazo yako yasiwe yanazurura sehemu nyingine tofauti na hapo, mpe full attention.
 85. Epuka kumsikiliza mwenza wako na huku unafanya vitu vingine tofauti, mpe muda wako usiogawanyika, epuka kuzururisha macho, akili na mawazo yako unapokuwa unamsikiliza mpenzi wako.
 86. Unapompa umakini wako wote mpenzi wako (angalia lugha ya mwili wake), mwangalia machoni, angalia mwili wake, mikono yake, miguu na namna anavyoongea mawazo yake, kwa kufanya hivyo utajua ni hisia gani anapitia na anachosema kina uzito kiasi gani.
 87. Kuna utafiti unaonyesha watu wa kawaida wanaweza kuweka umakini wao wote kwenye jambo kwa sekunde 7 tu kabla ya kuingiliwa na mambo mengine yanayowatoa kwenye umakini na utulivu. Jifunza kwa nguvu zako zote namna ya kuongeza umakini wako katika mambo yako muhimu kama kumsikiliza mpezi wako akiwa anaongea.
 88. Lengo la kumpa umakini mpenzi wako lisiwe ni kwa ajili ya kutaka kujitetea au kutaka kuonekana upo sahihi la hasha, bali iwe ni kwasababu unataka kumuelewa ni nini anachotaka na anachomaanisha.
 89. Unapompa umakini na nafasi ya kuongea ni rahisi kujua upendo au kupendwa ina maana gani kwake. Usikimbilie kuhitimisha tu kwamba kupenda au kupendwa ni kujamiiana, kununuliana zawadi na kutimiza mahitaji ya nyumbani kama chakula nk. Unaweza kufanya hayo yote na mweza wako asione upendo au aone kama hapendwi, mpe nafasi ya kumsikiliza utagundua upendo uliko jificha.
 90. Kuna watu wengine wamelelewa na wazazi ambao walikuwa hawapendi kuwasikiliza wanapotaka kuelezea hisia zao za upendo, kazi na hata hasira. Hivyo wamekuwa wakiamini kuelezeana hisia zake kwa mtu mwingine ni jambo lisilofaa.
 91. Kuna baadhi ya wanandoa wana miaka mingi kwenye ndoa zao, lakini ni ngumu kukuta anaelezea hisia zake kwa mwenza wake, au unakuta mwenza wake hampi umakini na muda wa kuelezea hisia zake hii inasababisha kukosa majibu ya baadhi ya mambo magumu anayopitia, kwasababu hajaeleza hisia zake kwa mwenza wake ambaye angaweza kumsaidia.
 92. Kama tunataka kupunguza migongano na changamoto kwenye mahusiano na ndoa zetu, jambo mojawapo muhimu kufanya ni kujifunza kuelezea hisia zetu kwa wapenzi wetu, eleza tu hisia zozote ulizo nazo, hata kama ni hasira, chuki, upendo au mapenzi. Pia mpenzi wako anatakiwa kukupa umakini wote unapoeleza hisia zako kwake ili ajue unapitia mambo gani akusaidie au msaidiane kuvuka hizo changamoto.
 93. Tunatakiwa kujali sana hisia zetu na tujue sehemu sahihi ya kuziwasilisha ili tuwe na uhuru na amani. Usizipotezee hisia zako, tafuta mahali sahihi pa kuziweka na tafuta mtu sahihi atakayezielewa na ili akusaidie.
 94. Sisi binadamu ni viumbe wa hisia, na hisia zina mchango mkubwa kwenye maendeleo yetu kimaisha, mahusiano, na kiuchumi. Hivyo elewa kuwa mwenza wako ana hisia na anaweza kupitia vitu vigumu, hivyo mpe muda wa kueleza hisaia zake.
 95. Kumbuka siku zote hisia zenyewe kama zilivyo sio mbaya wala sio nzuri. Ni vile vitendo tunavyoamua kuvifanya baada ya kupata hisia ndio vinatoa tafsiri ya hisia hiyo.
 96. Kama wapenzi au wanandoa inatakiwa ifike sehemu uwe huru kuzungumza hisia zako kwa mwenza wako na kwa familia yako. Bila kufikia hapo tutishia kuteseka ndani kwa ndani bila majibu.
 97. Namna nzuri ya kufanyia kazi eneo hili la hisia ni kuwa na ratiba ya siku kushirikishana angalau mambo matatu yaliyotekea ndani ya siku husika na namna unavyojisikia kuhusu mambo hayo.
 98. Kuwa na jambo mbalo mnalifanya pamoja kama wanandoa au wapenzi inasaidia sana na inaweza kuwa ni hitaji kuu la upendo kwa mwenza wako. Angalieni ni jambo gani muhimu mnawza kulifanya kwa pamoja na mkafurahia.
 99. Jambo la pamoja kulifanya kama wapenzi inaweza kuwa kutengeneza bustani, kwenda sokoni au kwenye maonyesho pamoja, kusikiliza musiki pamoja, kwenda kutalii pamoja, kuwa na matembeza marefu pamoja, kuosha gari pamoja, kusali pamoja n.k
 100. Kama mwenza wako anapenda zawadi basi unatakiwa kuwa mtoaji, na hapa zawadi haitakiwi kuwa ya gharama, maana sio lazima iwe ya gharama.
 101. Kuna wengine hata kujinunulia vitu wao wenyewe ni mtihani, ndio maana inapokuja sua la kununulia mpenzi wako zawadi wanakuwa wagumu na wazito kweli.
 102. Watu wanatunza fedha kwasababu wanajali zaidi usalama wao wa baadaye, mwandishi anasema kama unajali usalama wako wa baadae maana yake ujajali zaidi hisia zako. Kwanini usiwekeze kwa mweza wako kwa kujali hisia zake pia?
 103. Wakati mwenza wako anapitia magumu au changamoto kwenye maisha yake kama vile misiba kutoka kwa familia yake ni wakati wa kuwa karibu naye na kumuonyesha upendp kama zawadi. Ukiwa pamoja na mweza wako wakati wa changamoto anazopitia inatafsiriwa ni zawdi kubwa sana.
 104. Sio kila tunachofanyiana wakati wa uchumba ndio kitakuwa kinafanyika hivyo hivyo wakati wa ndoa, vitu vinaweza kubadilika sana, na ukaona rangi halisi ya mwenza wako, na hapo ndipo unapohitaji kujifunza kupendana tena ili kudumisha ndoa.
 105. Zile hisia kali za mapenzi na kupendana tunazokuwa nazo wakati wa uchumba sio hisia hizo tutakazokuwa nazo kwenye maisha ya ndoa, kwenye ndoa tunaishi uhaliasia wetu.
 106. Kwa miaka 30 iliyopita hakuna tena kazi maalumu za wanaume na wanawake sehemu nyingi duniani, jambo hili linachangia sana changamoto kwenye ndoa za kisasa ambazo wanataka waishi kama ndoa za kizamani za miaka 30 iliyopita.
 107. Kuna wakati mpenzi wako atakuomba umfanyie jambo ambalo unaamini sio la mwanaume kulifa ya au mwanamke kulifanya, kama vile kuosha vyombo, kufyeka majani nk. Hii inaweza kuwa changamoto endapo utakataa kufanya jambo hilo kwasababu ya jinsia yako.
 108. Tukumbuke, hakuna zawadi wala faida tunayoipata kwa kuendeleza tamaduni za miaka 30 iliyopita, kwa maslahi mapana ya familia yako na ndoa yako na hisia za upendo kwa mwenza wako ni vizuri kufanya jambo hilo.
 109. Watoto ambao wanabebwa, kubusiwa na kukumbatiwa wanakuwa katika afya nzuri za kihisia kuliko watoto wanaotelekezwa au kuachwa bila kufanyiwa mambo hayo. Upendo unahusisha mguso au kugusana.
 110. Kuwabusu na kuwakubatia watoto sio mambo ya kisasa na utandawazi, ni mambo ambayo yapo kwa karne nyingi, hata Yesu Kristo aliwabeba na kuwakumbatia watoto, sembuse sisi. Tuwaonyeshe upendo watoto wetu kwa kuwapa mkono, kuwabusu, na kuwakumbatia.
 111. Kwa wengine, kushikwa na kukumbaltiwa ndio lugha rahisi na wanayoielewa ya upendo na kupendwa, tunatakiwa kutambua endapo mweza wako anajali sana kuguswa basi mfanyie hivyo maana ndio upendo na kupendwa kulingana na tafsiri yake ya upendo.
 112. Elewa maeneo sahihi ya mwili ya kumshika mwenza wako, inaweza isiwe ni sehemu yoyote ya mwili wake, ni vizuri kuuliza na kuyajua ili unapomshika apate raha na hisia nzuri na akupende zaidi.
 113. Sio kwasababu wewe ukishikwa au kuguswa unapata hisia nzuri na raha basi ufikiri na kwa mpenzi wako inaweza kuwa hivyo hivyo, inaweza kuwa tofauti kwa mwenza wako, jua anachotaka mwenza wako na mtimizie.
 114. Kujamiiana inaweza kuwa ndio anachopenda zaidi mwenza wako, ili lifanyike kwa utoshelevu wote ni vizuri mkawa na muda wa kuzungumzia mambo hayo na jinsi inavyoleta hisia nzuri za upendo kati yenu.
 115. Kama mwenza wako anapenda sana kushikwa (physical touch) namna nzuri ya kuanya hivyo ni wakati analia, hii inaleta hisia nzuri sana za upendo na mahaba.
 116. Wakati mpenzi wako analia unatakiwa kumshika kwa hisia za upendo na mahaba, na hutakiwi kuwa na maneno mengi kipindi hiki, manano yako yanatakiwa kuwa machache sana na yenye hisia nyingi za upendo.
 117. Mwezi wako hawezi kusahau namna ulivyomshika kwa upendo kipindi analia na kupitia wakati mgumu, itampa kumbu kumbu nzuri za upendo wako. Na endapo utashindwa kufanya hivyo basi itakuwa kinyume chake.
 118. Changamoto nyingi kwenye ndoa ni kwasababu ya kushindwa kutimiziana mahitaji ya kihisia, na sio sio mambo mengine ya kawaida.
 119. Dhamiria kutimiza mahitaji ya kihisia ya mwenza wako, hii itasaidia sana kuokoa muda na kuweza kuelekeza nguvu zenu kwenye shughuli za maendeleo.
 120. Baadhi ya wanaume wana utupu ndani yao ambao unatakiwa kujazwa na hisia za upendo, na wanapokosa msaada huo ndani ya ndoa wanahangaika sana kutafuta sehemu nyingine.
 121. Kila kitu kinawezekana inawezekana unaitia changamoto nyingi sana kwenye ndoa au mahusiano yako, kumbuka kupenda ni uchaguzi unaweza kuufanya pale utakapoamua kumtimizia mwenza wako mahitaji yake ya kihisia ambayo anayatafsiri ndio upendo kwake.kwa kufanya hivyo nay eye atafanya kila ambacho wewe utatafsiri ni upendo.
 122. Jifunze kupitia haya machache kutoka katika kitabu hiki na uinusuru ndoa au mahusiano yako. Unaweza tena kupenda na kuwa na hisia zote kali za mapenzi na mahaba kwa mwenza wako kama wakati manachumbiana.
 123. Kupendana inaweza isitokee kwa siku moja, maana yake sio mara zote mtapenda kwa wakati mmoja, inawezekana mwenzio akaja kupenda baada ya muda hivyo inahitaji uvumilivu na uelewa. Mfano wewe unaweza kuanza kumpenda leo, yeye akaja kuanza kukupenda wiki ijayo, mwenzi ujao n.k.
 124. Wakati mwingine ukiona kupenda hakuji moja kwa moja kwako, basi ujue hiyo ndio namna nzuri ya kuelezea upendo, maana utachakuga kupenda.
 125. Tunapokuwa na utupu ndani yetu kwa kukosa upendo tunaishia kufanya mambo chini ya viwango na tunaishi kwenye maumivu.
 126. Kama unaongelea upendo basi jua kuwa ni kitu unaweza kukifanya kwa wengine zaidi kuliko kwako. Ni hii ndio maana upo tayari kumfanyia mwenza wako jambo fulani.
 127. Ukipendwa au kuwa na hisia za kupendwa na mwenza wako inaongeza kujiamini, na huwa tunaweka sababu kwamba ikiwa kuna mtu ananipenda maana yake mimi ni wa muhimu.
 128. Bila upendo tunaweza kutumia muda mwingi kutafuta kukubalika, kujiamini, na kujiona wa thamani. Upendo unatibu mambo hayo yote.
 129. Ndoa ilitakiwa iwe ndio sehemu ya kutengeneza kujiamini na kuwa mtu wa thamani, na sio kama ilivyo kwenye ndoa nyingi zimekuwa uwanja wa vita na sio sehemu ya usalama.
 130. Upendo sio jibu la kila kitu, lakini upendo unaweza kutengeneza mazingira ya amani na usalama wa kutafuta majibu ya kila kitu.

LOVE REALLY DOES “MAKE THE WORLD GO ROUND.

kupata chambuzi nyingine za vitabu kama hizi, weka jina lako na email yako hapa chini

SOMA ZAIDI: Uchambuzi Wa Kitabu Cha UNFAIR ADVANTAGE


One response to “Uchambuzi Wa Kitabu Cha 5 Langues Of Love”

 1. Hiki kitabu cha 5,love languages ni muhimu sana kwa mtu ambaye yupo au hayupo pia kwenye mahusiano kukisoma kwa sababu kitamsaidia kuweza kujua namna nzuri ya kumuendea mwenzie,pia hata kwenye kazi na biashara inaweza saidia kwa sababu ukijua partner wako anakuwa anahamasika vipi inakuwa vizuri sana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X