Uchambuzi wa Kitabu: Atomic Habits; Tiny Changes, Remarkable Results


Mwandishi: James Clear

Mchambuzi: Hillary Mrosso

Simu: +255 683 862 481

UTANGULIZI

Tabia hujenga maisha tuliyonayo, tabia huamua mafanikio kwenye maisha yetu. Ubora wa maisha yetu ya sasa na ya baadaye yanategemea sana tabia tunazoziishi kila siku. Mara zote tumejikuta kwenye jamii ambayo inaishi na kuamini kwenye tabia fulani ambazo kwa kiasi kikubwa ndio tabia tunazoziishi na ndio zimetuletea maisha tuliyo nayo.

Mandishi James Clear kupitia kitabu chake cha ATOMIC HABITS, ametuonyesha namna inavyowezekana kujenga tena tabia tunazozipenda, pia ametuonyesha kupitia kitabu hiki namna ya kuvunja tabia tusizozipenda. Kupitia uchambuzi huu, nimekuandalia mambo 130, niliyojifunza ndani ya kitabu hiki bora kuhusu tabia. Naweza kuungana na watu wengine kusema hiki ndio kitabu bora sana kuhusu tabia. Karibu sana katika uchambuzi wa kitabu hiki.

1. Wote tunakutana na changamoto kwenye maisha lakini baada ya muda ubora wa maisha yetu huamuliwa na ubora wa tabia zetu. Kila tabia ina matokeo yake, ukiwa na tabia nzuri utaleta matokeo mazuri ukiwa na tabia mbaya utaleta matokeo mabaya.

2. Mjasiriamali na mwekezaji, Naval Ravikant aliwahi kusema, ili uandike kitabu bora, unahitaji kwanza kuwa kitabu. Maana yake kabla ya uandishi wa kitabu hiki kilichoandikwa na James Clear aliishi na kuyafanyia kazi mambo yote yanayohusu tabia aliyoyaandika katika kitabu hiki.

3. Hakuna njia moja nzuri ya kujenga tabia bora, lakini kupitia kitabu hiki mwandishi amejaribu kutumia njia za ufasaha na zilizohakikishwa katika utengenezaji wa tabia bora, haijalishi upo kona gani ya dunia, unaweza kutumia mafunzo ya kitabu hiki na ukajenga tabia bora sana kwenye maisha yako.

4. Kila ushindi kidogo unaoupata, au vikwazo vidogo unavyovipata vinaweza kuzalisha matokeo makubwa sana endapo vitaendelea kutokea bila kukoma. Maana yake ni kwamba hata kama unataka kuanzisha tabia unayoiona ni ndogo na inaweza kuwa haina sana mchango, ukweli ni kwamba mkusanyiko wa vitu vidogo vidogo huleta matokeo makubwa hapo baadaye.

5. Tabia ni mkusanyiko wa juhudi binafsi zinazochukuliwa kila siku ili kujiboresha. Kama vile fedha inavyoweza kuongezeka kwa njia ya riba kutokana na mkusanyiko wa siku nyingi hivyo ndivyo ilivyo kwa tabia pia.

6. Mafanikio yako kimaisha ni matokeo ya tabia ulizoziishi kwenye maisha yako, mafanikio yako kifedha ni matokeo ya tabia bora za kifedha unazoziishi, uzito na afya uliyonayo ni matokeo ya tabia za ulaji unazoziishi kwenye maisha yako, ufahamu na maarifa uliyonayo ni matokoe ya tabia za kujifunza unazoziishi kwenye maisha yako. Mara zote huwa tunapata kila tunachokifanya na kukirudia rudia kwenye maisha yetu.

7. Tabia ni kama upangwa wa pande mbili, unaweza kuutumia kukusaidia na pia unaweza ukatumika kukuharibu. Maana yake tabia zinaweza kukuletea mafanikio na pia tabia zinaweza kukukwamisha kufikia mafanikio yako. Tabia ni hatari sana, hivyo jua namna ya kuzitumia tabia zikusaidie kwenye maisha yako.

8. Mafanikio ni matokeo ya mkusanyiko wa juhudi na hatua ulizokuwa unachukua siku za nyuma bila kuacha, na ndio hujikusanya na kukufanya uonekane umefanikiwa sana ndani ya kipindi fulani. Maana yake hakuna kinachofanyika bila kuwa na mchakato wa muda mrefu, mfano ugonjwa wa kansa, unaweza kutumia zaidi ya 80% ndani ya mwili wako bila kugundulika, lakini siku ya kuja kuonekana ni majanga makubwa sana ndani ya mwezi mmoja.

9. Mara nyingi sana ni ngumu kutengeneza tabia bora zinazodumu, kwasababu hatua ndogo ndogo tunazochukua kila siku zinaweza zisiwe na matokeo ya haraka, na wakati mwingine matokeo yake hayaonekani na huchukua muda mefu kuonekena, jambo hili ndio husababisha wengi kuishia njiani na kukata tamaa, hivyo kushindwa kuunda tabia wanazozitaka.

10. Kama unajikuta unashindwa kujenga tabia nzuri kwenye maisha yako, au umeshindwa kuivunja tabia mbaya, sio kwasababu huna uwezo wa kuivunja tabia hiyo, bali ni kwasababu kuna ukanda umeshindwa kuuvuka.

11. Kazi ya kuondoa tabia mbaya kwenye maisha yetu ni kama kuungoa mti mkubwa wa mkuyu wenye mizizi mirefu na imara, lakini pia kazi ya kujenga tabia mpya na nzuri kwenye maisha yetu ni kama kupalilia na kutunza uwa zuri na laini ili lisivyauke kila siku.

12. Muhimu kwenye maisha sio kuwa na malengo, bali ni kuwa na mfumo mzuri utakaokufanya uufuate mara zote ili ukuletee matokeo na kutimiza malengo yako.

13. Jenga mfumo mzuri na imara ambao hautakuwa mgumu kuufuata, jenga mfumo ambao utafanya iwe rahisi kutimiza malengo ya maisha yako.

14. Muhimu kwenye maisha sio kubadilisha matokeo, muhimu ni kubadilisha mfumo au system iliyoleta matokeo hayo.

15. Ili tupate suluhisho la kudumu ni muhimu kutatua matatizo yetu kwa ngazi ya kimfumo na sio ngazi ya kimatokeo.

16. Changamoto iliyopo kwa wanaoweka malengo ni kuahirisha furaha au baadhi ya mambo muhimu kwenye maisha, mfano kuna watu wanasema wakifanikiwa kutimiza malego fulani au wakifikia mafanikio fulani ndio watakuwa na furaha, watafanya jambo fulani nk.

17. Kama utaendesha maisha yako kwa misingi ya kimfumo hutakuwa na muda wa kusubiria matokeo ndio ufurahi au uwe na amani, utakuwa na amani na utafurahia mchakato utakao kupeleka kwenye matokeo, hutahitaji ruhusu au wakati fulani maalumu ili uwe na furaha.

18. Mafanikio makubwa kwenye maisha yanategemea kujitoa kwa kiwango kikubwa kubakia katika mchakato wa kufikia mafanikio yako, uwezo wako wa kubakia katika mchakato wa kufikia mafanikio yako unatakiwa kuwa mkubwa na wenye uvumilivu mkubwa.

19. Tabia mbaya unazotaka ziondoke kwenye maisha yako huwa zinatabia ya kujirudia rudia kila mara hata bila ya wewe kujua; hii ni kwasababu kuna mfumo wa maisha unaouishi unaifanya tabia hiyo mbaya kuwa na nguvu ya kuendelea kutokea kwenye maisha yako.

20. Jambo muhimu katika kubadili tabia mbaya uliyo nayo ni kubadili mfumo mbaya ulio nao. Ukiwa na mfumo mzuri utakuletea matokeo mazuri, na mfumo mbaya unaleta tabia mbaya.

21. Atomic habit ni vitabia vidogo kama atomi ambavyo vinakuwa sehemu ya mfumo sahaihi ambao unaleta matokeo makubwa, kama vile ilivyo kwa atomi ni chembe ndogo sana ambayo huungana na kutengeneza kitu kikubwa sana.

22. Mara nyingi ni ngumu kubadili tabia ambayo ni matokeo ya mapokeo na imani za tamaduni fulani, tabia ambazo zimetokana na mambo ya imani ni ngumu sana kuzibadili, maana ukitaka kuzibadili tabia hizi inabidi ubadili kwanza namna mtu anavyoamini kuhusu tabia hiyo.

23. Kama kuna ufahari unaupata kutokana na jinsi ulivyo, au jinsi watu wanavyokutambua, ndio inaongeza hamasa ya kuendelea kuidhihirisha tabia hiyo.

24. Tabia zinazobeba utambulisho wa mtu ni ngumu sana kuzivunja na pia ni rahisi kuunda tabia ambazo zinahusianisha utambulisho wa mtu.

25. Kama unaona fahari ya nyele za kichwa chako jinsi zilivyo, lazima utatengeneza aina ya tabia ambazo zitakuasidia katika utunzaji wa nywele zako ili ziendelee kuonekana vizuri kila siku.

26. Kama unaona ufahari juu ya mwili wako kuonekana imara na wenye afya, lazima utajenga tabia za kila siku za kuendelea kuutunza mwili wako na kufanya mazoezi ili uonekane kuwa imara mar azote.

27. Mwandishi wa kitabu hiki James Clear anasema, unaweza kujenga tabia kwasababu umepata hamasa ya kujenga tabia hiyo, lakini ili uendelee kuwa na tabia ulioijenga ni muhimu tabia hiyo ikahusisha utu wako au ikawa sehemu muhimu ya utambulisho wako.

28. Mfano, lengo lisiwe kusoma tu kitabu, lengo kubwa linatakiwa kuwa msomaji wa vitabu. Lengo lisiwe tu kukimbia, bali iwe kuwa mkimbiaji, lengo lisiwe kuwa mpiga vyomba bali liwe kuwa mwanamziki. Endapo utafikiri kwa namna hii katika kufanya mambo yako, utajenga tabia za kudumu ili uendelee kuwa msomaji, mkimbiaji na mwanamuziki mkubwa.

29. Ni rahisi kufanya kama mtu ambaye unatamani kuwa. Na ujenzi wa tabia unakua rahisi endapo tabia zitahusisha kuwa mtu bora unayemtamani kuwa.

30. Katika ujenzi wa tabia mpya, unaweza kuzalisha tabia bora na zikakusaidia kufikia ndoto zako, kwa upande mwingine unaweza kuzalisha tabia hatarishi ambazo zitakwamisha maisha yako. Chagua kwa usahihi ujenzi wa tabia muhimu kwenye maisha yako.

31. Utambulisho wako au utu wako unatokana na tabia zako; hukuzaliwa na mapokeo na imani ulizo nazo na unazozijua kuhusu wewe mwenyewe, kila unachokiamini ulijifunza au umekutana nacho kwenye mazingira uliyoyazoea.

32. Mazoea na uzoefu yamechangia sana kukupa mitazamo na imani ulizo nazo, ndio maana tabia nyingi hujengwa na kusitawi kupitia mazingira yanayotuzunguka.

33. Jinsi unavyokoaa kwenye mazingira fulani kwa muda mrefu, mazingira hayo yanamchango mkubwa sana wa kukufanya uwe na tabia ambazo unazirudia rudia kila mara bila hata wewe kujua.

34. Tabia ndio zinakujengea utambulisho wako, mfano, kama una tabia ya kuandika kila siku, utaishia kuwa mwandishi, kama una tabia ya kuimba kila siku utaishia kuwa mwimbaji, kama una tabia ya kupika kila siku utaishia kuwa mpishi, kama una tabia za kufundisha kila siku utaishia kuwa mwalimu.

35. Kila hatua unazochukua kila siku ni kura yako unajipikia ili kufikia mtu unayetamani kuwa, hakuna ambalo unalifanya lisiwe na matokeo yake.

36. Kila siku chagua aina ya mtu unayetaka kuwa, kisha thibitisha hilo kwa kuchukua hatua ndogo ndogo zinazokupa ushindi. Wewe sio jiwe, tabia yako sio jiwe kwamba haibadiliki, kila kitu kinaweza kubadilika endapo kitaandaliwa mfumo sahihi wa kubadilika.

37. Mwandishi anasema, kuna aina 3 za mabadiliko, mabadiliko ya matokeo, mabadiliko ya mchakato na mabadiliko ya utu au utambulisho wako. Fikiria mtu bora unayetamani kuwa, kiasha jenga tabia za kufanya kila siku ili kufikia mtu huyo bora unayemtamani.

38. Mwandishi James anaeama, tabia ni njia fupi ulizojifunza na kuzitumia kipindi cha nyuma ili kutatua changamoto ulizokutana nazo.

39. Mazingira yale yale yakijirudia utatumia tabia ile ile kutatua changamoto ulizokutana nazo. Mazingira sahihi yanatukumbusha kuchukua hatua fulani zilizofanya kazi kipindi cha nyuma ili kutatua changamoto zinazotokea kwenye maisha.

40. Usipokuwa na udhibiti mzuri wa tabia zako, zinaweza kuwa kikwazo kikubwa sana kwako, zinaweza kukunyima uhuru mkubwa sana.

SOMA ZAIDI: Uchambuzi Wa Kitabu Cha The 5Am Club: (Mambo 304 niliyojifunza kutoka kwenye hiki kitabu)

41. Siku zote fahamu zetu zinaangalia mazingira yote ya ndani na nje ili kujua ni sehemu gani zawadi zilipo. Kunakuwaga na msukumo mkubwa sana wa kufanya jambo fulani endapo jambo hilo limeambatana na zawadi baada ya kulifanya.

42. Fahamu zetu zinaangalia sehemu ambazo tunaweza kupata matamanio yetu na ambapo tunaweza kupata utoshelevu na raha.

43. Hisia za raha na karaha ni sehemu ya mchakato wa mrejesho wa taarifa ambao husaidia ubongo wetu kutofautisha kati ya matendo ya muhimu na yale yasiyo ya muhimu.

44. Lengo la kila tabia ni kutatua changamoto zinazotokea kwenye maisha yetu kwa nguvu kidogo kwa kadri inavyowezekana. Mfano, kila siku unapovaa viatu au unapofunga kamba za viatu vyako, unatumia gharama na nguvu gani kufanhya hayo, ukiangalia utaona unatumia nguvu kidogo sana.

45. Kuna kanuni na sheria za kubadili tabia yoyote ile, sheria hizo ni fanya tabia hiyo kuwa wazi, pili ifanye tabia hiyo kuwa ya mvuto, tatu ni kuifanya tabia hiyo kuwa rahisi na nne ni kufanya tabia hiyo kuwa na utoshelevu.

46. Kuna vitu vinatokea kwenye maisha yetu bila hata sisi kufikiria vinatokeaje, mfano jinsi nywele zetu zinavyoota, jinsi mapigo ya moyo yanavyodunda, jinsi tunavyopumua, jinsi tumbo letu linavyomengenya chakula. Mambo haya yanafanyika katika miili yetu bila hata ya sisi kufikiri namna yanavyofanyika, sisi ni zaidi ya fahamu zetu.

47. Mwanasaikolojia maarufu Carl Jung aliwahi kusema, inabidi tuyadhanie yale tusiyoyadhaia, bila kufanya hiyo mambo hayo yanaweza yakayaendesha maisha yetu hadi tukaishia kuona ni kama sehemu ya hatima yetu.

48. Tunatakiwa kuzielewa kwa undani tabia zinazoendesha maisha yetu, ili ujue kama zinaweza kuleta majanga au hatari kwenye maisha, usipofanya tathimini ya tabia, unaweza kudhani baadhi ya tabia ulizo nazo ni haki yako na huwezi kuzibadili.

49. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, hakuna tabia nzuri wala tabia mbaya, tabia zote zina manufaa kwa namna moja au nyingine kwa mtu anayezitumia. Tabia zote huwa kuna tatizo zinatatua ndio maana watu wanaendelea nazo, tabia mbaya kuna namna zinawasaidia watu hata kama ni kwa muda mfupi.

50. Namna ya kujenga tabia mpya ni kuisema kuisema angalau kila siku kwa nguvu, hii itatasidia kufanya tabia hiyo kuwa wazi sana kwako, lakini pia itakupa ufahamu wa uwepo wa tabia hiyo.

51. Mfano, kama unataka kuacha tabia ya kula vyakula vyenye sukari, unapaswa kusema kwanguvu leo nataka kula chipsi mayai na soda, lakini nikila chipsi mayai sio nzuri kwa afya yangu maana zitaniongezea uzito na kisukari kwenye mwili.

52. Unapoamua kujijengea tabia mpya kwenye maisha yako, itakuwa ngumu katika siku za mwanzo, lakini ukiendelea kuifanyia kazi kila siku, itafikia hatua itajiendesha yenyewe bila wewe hata kutumia nguvu. Na hapo inahitaji muda na uvumilivu mwingi.

53. Kabla ya kuibadili tabia yoyote kwenye maisha yako, unahitaji kuifahamu vizuri tabia hiyo, ielewe tabia hiyo illivyo na namna inavyokufanya ukose furaha kila inapojitokeza.

54. Kama unaweza kuiona na kuitaja tabia unayotaka kuibadilisha inatakufanya upate nguvu ya kuchukua maamuzi ya kuibadili tabia hiyo, mwandishi anasema kuitaja na kuisema kwa sauti tabia unayotaka kuibadili unajipa nguvu zaidi na ushawishi mkubwa wa kuibadili.

55. Wengi wetu tunapenda kusema nitafanya hiki au nitafanya kile, au nitabadili hiki au kile, lakini hatusemi tutafanya lini, na wapi na kwa muda gani. Tunaishia kusema tu nitafanya nitafanya, lakini hatuweki maelezo ya kutosha kwenye ufanyaji wa jambo tunalotaka.

SOMA ZAIDI: Uchambuzi wa Kitabu: The Leader Who Had no Title (Kiongozi Asiye na Cheo); Mambo 200 Niliyojifunza katika kitabu hiki.

56. Ili kuongeza ushawishi wa kuchukua hatua kujenga tabia bora ni lazima tuweke bayana kabisa tabia ambayo utaifanya, muda ambao utaifanya, eneo ambalo utaifanya tabia hiyo. Mfano, saa tano asubuhi nitaenda ofisini kwa ajili ya kuandika makala kwa muda wa saa moja. Hapo umeiweka kabisa wazi hivyo inakupa nguvu ya kuchukua hatua na kufanya.

57. Kuna watu wanakaa wakisubiri maisha yako yote ili muda uwe upande wao ndio waanze kufanyia kazi malengo na ndoto zao. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, huna muda wa kusubiria kama unavyofikiri, chukua hatua mara moja.

58. Wengi tunafikiri tumekosa hamasa ya kufanya mambo, mwandishi James anasema, hatujakosa hamasa, tumekosa uwazi, au ubayana kwenye yale tunayoyafanya. Mfano hutuweki bayana ni lini, na wapi, utafanya jambo lako, hivyo kusema tu utafanya haikupi ushawishi wa kutosha kuchukua hatua.

59. Tunatakiwa kuwa na nia ya utekelezaji ambayo tumeiweka bayana kabisa, ili ikifikia wakati uliopanga kufanya jambo fulani kila kitu kiwe tayari, isiwe umefika wakati wa kufanya jambo lako unaanza kuwaza waza, na kuangalia mambo mengine, ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kukutoa kwenye malengo na mipango yako uliyoipanga.

60. Weka mazingira yote yawe bora kabisa kiasi cha kukuvutia uendelee kutekeleza tabia mpya, ainisha na weka bayana kabisa unachotaka ili ukipate. Usikubali mambo mengi yakufanye ushindwa kujenga tabia bora unayoitamani kwenye maisha yako.

61. Mwandishi James Clear anasema, muda mzuri wa kuanza tabia mpya ni siku ya kwanza ya wiki, mfano siku ya jumatatu, mwandishi anasema, siku hii unakuwa na nguvu na hamasa na matumaini makubwa sana, hivyo ni rahisi kuanza jambo lolote siku ya jumatatu.

62. Sehemu yenye matumaini inakupa sababu ya kuendelea kuchukua hatua, chagua kuwa na nyakati nyingi nzuri na zilizojaa matumaini ili upate sababu nyingi za kuendelea kufanyia kazi mabadiliko unayoyataka kwenye maisha yako.

63. Ipe tabia yako mpya muda na nafasi ya kutokea na kuchanua hapa duniani, kila tabia bora unayotamani kuwa nayo kwenye maisha yako inawezekana kuitengeneza na kuipa mazingira yote wezeshi ili ichanue na kukuletea kila ulichokitamani na kukufanya kuwa mtu uliyemtamani.

64. Jitamanishe tabia mpya unayoijenga kwenye maisha yako, jione ukiwa bora kwa kuiishi tabia hiyo, jenga shauku itakayokusukumba kuishi tabia hiyo kila siku mpaka iwe sehemu muhimu ya maisha yako ya kila siku.

65. Hakuna tabia inayojijenga katika upweke, kuna uhusiano mkubwa sana endapo utajenga tabia mpya na nzuri, utaendelea kujenga tabia nyingine nyingi mpya na nzuri zinazoendana na tabia mpya uliyoijenga. Kanuni ya uhusiano huu inaitwa Diderot effect.

66. Kanuni ya Diderot inasema unaponunua kitu kimoja inachochea kununua kingingine kinachoendana na hicho. Mfano, ukinunua nguo, utatamani ununue na viatu vinavyoendana na hiyo nguo, saa inayoendana na hiyo nguo nk. Kanuni hii inaweza kutumika vizuri kwenye uanzishwaji wa tabia mpya ambao utakufanya uanzishe tabia nyingine nzuri zinazoendana na tabia uliyoanzisha.

67. Mwandishi James anasema njia nyingine ya kujenga tabia mpya ni kuijua tabia unayoiishi kila siku na kisha kuipachika tabia yako mpya juu ya tabia ya zamani. Mfano, kufanya tahajudi kwa dakika moja baada ya kuweka kahawa kwenye kikombe changu wakati wa asuhuhi.

68. Pia unaweza kuongeza tabia ya kushukuru kila baada ya kukaa mezani wakati wa kula chakula cha jioni na familia yako; unaweza kufanya mazoezi kila utakapofika nyumbani na kubadili nguo za kazi na kuvaa za mazoezi wakati wa jioni ukitoka kazini.

69. Hata kama wewe ni wa kipekee kiasi gani? Kuna tabia zinaweza kuibuka kwenye maisha yako kutegemea na mazingira yalivyo. Mazingira yana mchango mkubwa sana wa kujenga tabia na kuzikuza baadhi ya tabia nyingine. Kwenye kila mazingira utakayoishi au kukutana nayo, yatumie mazingira hayo kwa faida yako ili yawe sehemu ya kuimarasha tabia zako bora na kujenga nyingine bora zaidi.

70. Mazingira yanaweza kukufanya ukaamua vingine kabisa na ulivyopanga au ulivyotarajia. Mfano, ukienda kwenye maduka ya nguo au bidhaa za fasheni utaona zile nguo au bidhaa zinye gharama na faida kubwa zinawekwa mbele kabisa ili zionekane vizuri na kila mtu, lakini zile bidhaa dhaifu na zisizo na faida kubwa zinawekwa mbali kwenye kona za maduka. Hapo ujue wanakulenga wewe ili ujichanganye ununue zenye faida kubwa kwao.

71. Watafiti wanaonyesha kuwa, tunategemea sana vitu tunavyoviona kuliko hata milango mingine ya fahamu. Vitu tunavyoviona vina nguvu sana ya kugeuza mitazamo na misimamo yetu. Vingi tunavyoviona ndio vinatufanya kuamua mambo mengi kwenye maisha yetu. Ndio maana ukitaka kufanya biashara yenye mafanikio makubwa lazima uzingatie bidhaa zenye mvuto zaidi mbele ya macho.

72. Kwenye kutengeneza tabia mpya, lazima uzingatie mazingira yenye mvuto, ifanye tabia mpya unayoipenda kuwa ya mvuto na inayokuvutia sana, kiasi kwamba utapenda kuifanya kila mara, hii inaenda sambamba na mazingra yenye mvuto sana katika kuikuza tabia hiyo.

73. Wengi tunaishi kwenye dunia iliyoandaliwa na watu wengine, tunaishi kwenye mazingira yaliyoandaliwa na watu wengine kwasababu ya matamanio yao. Kama tunataka kuwa na ufanisi kwenye mambo tunayoyafanya inatakiwa kujitengenezea dunia na mazingira yetu wenyewe ambayo yatakuwa ndio mazingira bora sana kutimiza na kutekeleza jambo lolote kwa ufanisi wa hali ya juu sana.

74. Mwandishi James Clear anasema, kuwa muundaji na mtengenezaji wa dunia yako, jitengenezee Edeni yako, ambayo kwa kukaa humo utaishi maisha bora, utafanya kazi zako kwa ufanisi na utakuwa mtu wa furaha, na utaifurahia dunia yako mwenyewe.

75. Siku zote ni rahisi kusimamia na kuongoza kitu ambacho umekiunda na kukianzisha mwenyewe. Unakuwa na uongozi na umiliki wote na yote yaliyomo ndani ya mazingira uliyoyatengeneza.

76. Tengeneza uhusiano mzuri na mazingira yako ya kazi, uhusiano ambao utakufanya kuchukua hatua zaidi na kufanya makubwa zaidi. Mfano, unaweza kutengeneza mahusiano mazuri na ofisi yako au sehemu unapokaa na kufanya kazi zako, ili ukifika tu eneo hilo hamu na shauku ya kufanya kazi iwe kubwa.

77. Uwezo wa kufanya kila mazingira yawe yanaleta ufanisi kwako zaidi ni muhimu sana katika ujenzi wa tabia. Mfano, mwingine kochi ni kwa ajili ya kukaa na kuangalia TV, mwingine kochii ni sehemu yake bora ya kukaa na kusoma kwa muda mrefu. Hii ndio namna ya kushirikiana na mazingira yako kwa manufaa makubwa ili kujenga tabia mpya.

78. Unaweza kubadili mazingira na kwenda sehemu nyingine tofauti ili ujitengenezee mazingira bora kwa ajili ya kupalilia tabia yako mpya. Mfano, unaweza kwenda hotelini, ukachagua kochi au kiti na meza unayoipenda kisha ukaamua kupafanya pakawa ndio sehemu yako bora ambayo ukikaa hapo unaweza kufanya kazi zako kwa ufanisi mkubwa.

79. James Clear anasema kila tabia inatakiwa kuwa na nyumbani kwake. Usiache tabia ikatanga tanga mitaani bila kuwa na sehemu ambayo itapata utulivu, chakula na kukua ili iwe sehemu ya mafanikio yako kwenye maisha. Tabia zinatakiwa kutusaidia kufanikiwa na sio kutuangusha.

80. Tengeneza mazingira yanayotabirika, mfano ukifika kitandani ni kulala na sio kufanya mambo mengine kama kuchati, ukifika mezani ni kula, ukifika ofisini ni kufanya kazi na sio jambo jingine. Tabia ili zikue zinahitaji mazingira yanayotabirika.

81. Wakati mwingine ni rahisi kutengeneza tabia mpya sehemu mpya, au kwenye mazingira mapya, kwa sababu upo kwenye mazingira mapya ambayo hayana upinzani katika kukuza tabia mpya.

82. Mwandishi anasema, uvumilivu, shauku, na matamanio makuwa ni mambo muhimu katika kufikia matokeo, lakini ili uwe na hayo yote unaweza kudhani unahitaji sana kuwa mtu wa nidhamu kubwa, nidhamu inatakiwa iwe kwenye mazingira ili yakufanya na wewe kuwa na nidhamu.

83. Njia nzuri ya kuondoa tabia mbaya kwenye maisha yako ni kuondoka na kuondoa mazingira yanayokufanya uifanye tabia hiyo kirahisi, au ondoka na ondoa mazingira yanayofanya tabia hiyo iwepo hapo. Mfano, kama unaona unashindwa kufanya kazi kwasababu upo na simu yako karibu, unatakiwa uiondoe simu sehemu unapofanyia kazi na uiweke chumba kingine ili ufanye kazi zako kwa ufanisi.

84. Kama kuna namna kwenye maisha yako unajiona hutoshi au hufai na umeachwa nyuma, mwandishi wa kitabu hiki anasema acha kabisa kufuatilia mitandao ya kijamii ambayo inakufanya ujione hutoshi, pia inakufanya uone wivu na ujione hufai.

85. Kama unapoteza muda mwingi kuangalia TV kwasababu ipo tu sebuleni na unaikuta inawaka na ina vipindi vinavyokuvutia, mwandishi anasema, iondoe hiyo TV na uiweke kwenye chumba kingine ambacho huingii mara kwa mara.

86. Kwenye ulimwengu tulionao sasa umetengeneza mazingira ya usumbufu mwingi sana, na usipojua unataka nini kwenye maisha yako, utajikuta unatumia muda wako mwingi kufuatilia maisha ya wengine, na kufuatilia vitu vya mitandaoni ambavyo havina tija kwenye maisha yako.

87. Weka mazingira yawe magumu sana kwenye ufanyaji wa tabia mbaya ambazo huzipendi kwenye maisha yako, na pia weka mazingira rahisi, yenye mvuto kwa utendaji wa tabia nzuri unayotaka kuijenga kwenye maisha yako.

88. Kama kitu kimekuvutia sana, kama kuna fursa imekuvutia sana, ni rahisi kuunda tabia kwenye vitu unavyovipenda maana vitakupa sababu na hamasa za kuifanya kila mara.

SOMA ZAIDI: Uchambuzi Wa Kitabu: 25 Hours a Day; Going One More to Get What You Want

89. Kama tabia unayoijenga inaendana na utamaduni wa jamii yako, mara nyingi inakuwa rahisi na kuvutia unapoifanya maana hutakutana na upinzani mkubwa kwenye utekelezaji wake.

90. Mara zote huwa tunafuata tabia za tamaduni zetu hata bila kufikiri, wakati mwingine hata bila kuuliza, au bila hata kukumbuka. Hii ni kwasababu kila mtu anaiona ni sawa na kila mtu anaifanya na umezaliwa umekuta watu wanazifanya hiyo wewe kuzifanya haiwi jambo gumu.

91. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, tabia ni rahisi kuzitekeleza kama zinatufanya tuonekane ni sehemu muhimu ya jamii au kundi pale tunapoifanya. Kumbuka mara zote huwa tunaiga au kufuata tabia za makundi 3 muhimu sana kwenye jamii zetu, makundi hayo ni; watu wetu wa karibu sana, wingi wa watu, na wenye nguvu au ushawishi.

92. Kama unataka kujenga tabia mpya na unayoipenda tafuta watu wanaoishi kwa tabia unayoitamani. Tafuta watu au kundi au jamii ambayo wanaishi tabia unayoitaka kisha jiunge nao, kwa kufanya hivyo utakuwa kwenye mazingira mazuri na rahisi kwa tabia yako kusitawi.

93. Mfano, ukienda kwenye jamii au kundi la watu ambao kila siku asubuhi wanafanya mazoezi ya kujenga mwili, itakuwa rahisi kwako kujenga tabia ya mazoezi ya mwili kwasababu kuna mazingira mazuri ya kuifanya tabia hiyo ya mazoezi bila upinzani mkubwa.

94. Mwandishi James anasema ili iwe rahisi kwako kujenga na kukuza tabia unazozipenda, ni vizuri ukazungukwa na watu au mazingira yatakayokufanya uijenge tabia yako kwa urahisi. Kama wewe unapenda muziki wa dansi, zungukwa na watu wanaoimba na kupenda mziki wa dansi.

95. Makundi, watu wa karibu, na watu wenye nguvu ya kiuchumi huwa wana ushawishi sana, hivyo ukikaa miongoni mwa kundi moja wapo hapo, ni rahisi kujikuta ukifanya kama wao; kama wanapenda kusoma vitabu utajikuta na wewe ukitamani kusoma vitabu, kama wanafanya biashara na kuzungumza biashara, basi itakuwa ni rahisi sana kwako kunzisha biashara maana upo kwenye mazingira sahihi.

96. Mara nyingi tuona ni bora kukosea tukiwa kwenye kundi kuliko kuwa sahihi sisi wenyewe. Maana yake makundi yana nguvu na ushawishi sana, hata kama kitu sio sashihi, wengi wakikipenda au kukifanya kinaonekana sahihi.

97. Kuna watu wanavuta sigara wakidhani kuna watu wanawafurahia au kuwapenda kwa tabia hiyo. Mwandishi James anasema, huitaji tabia ya uvutaji wa sigara ili upendwe au uonekane kwenye jamii, kuna tabia nyingine nyingi nzuri na salama ambazo unaweza kuzitumia na zikakufanya kuwa maarufu na kupendwa.

98. Kama unasumbuliwa na tabia ya uvutaji wa sigara, unachotakiwa kufanya ni kuifanya tabia hiyo kuwa mbaya na isiyo kuvutia kabisa. Hivyo tengeneza mazingira yote yawe magumu kwa uvutaji wa sigara, lakini pia ukitamani kuvuta sigara fanya tabia nyingine bora kuliko hiyo.

99. Kuna muda mwingi sana tunatumia kupanga na kutamani vitu vifanyike kwa namna fulani, wakati mwingine tunasoma majarida au vitabu kupata taarifa ya kufanya jambo fulani tunalotamani; mwandishi anasema kuna upotevu mkubwa sana wa muda endapo hutachukua hatua haraka kutekeleza unayoyatamani.

100. James Clear anasema, hakikisha unachukua hatua kutekeleza unayoyatamani, haina maana kupanga mambo mengi halafu huchukui hatua.

101. Kama umeona tabia ya kufanya mazoezi ni muhimu kwa ajili ya afya yako usipoteze muda kuuliza uliza tena, unachotakiwa kufanya ni kutafuta vifaa vya kufanyia mazoezi na kuanza mazoezi mara moja.

102. Kuna wengine wanajiandaa sana kiasi kwamba hamu ya kufanya jambo husika inaisha na kupotea.

103. Kama umeona tabia ya kusoma vitabu ni muhimu sana kwenye maisha yako, usipoteze muda kujiandaa kwa hilo, ingia mara moja kwenye utekelezaji na uanze kusoma. Hii ni kwa wale wanaonunua vitabu vingi halafu hawavisomi.

104. Njia nzuri ya kujifunza chochote ni kuchukua hatua, au kufanya mazoezi. Mwandishi James anasema kuna wakati mwingine maandalizi ni kama aina nyingine ya kughairisha jambo. Kama una jambo unalipenda kwenye maisha yako, kikubwa unachoweza kufanya ni kuchukua hatua na kuanza utekelezaji mara moja.

105. Kama unataka kuchora hakikisha kila kitu unachohitaji kwa ajili ya uchoraji kipo mezani, kama vile penseli, karatasi, rangi, rula, ufutio nk. Vitu hivyo viwe karibu na ukifika mezani ni kuanza kuchora sio tena ukifika mezani unaanza kutafuta vitu vingine, weka mazingira yote yawe rahisi kwako ili uchore.

106. Kama unataka kuanza kujenga tabia ya kufanya mazoezi kwa ajili ya afya ya mwili wako, weka vifaa vyote vya mazeozi sehemu inayoonekana, usivifiche mbali, na pia hakikisha una vifaa vyote unavyohitaji kwa ajili ya mazoezi kama vile viatu, nguo nk.

107. Kama unataka kuboresha ulaji wako ili uwe ni wa afya, hakikisha vitu vyote unavyovihitaji kwa ajili ya mlo wako vipo, kama ni matunda, mboga mboga, maziwa, maji nk. Hakikisha vyote vinakuwepo. Pia usiweke karibu vyakula visivyojenga mwili kama vile soda, sukari, vilevi, chipsi nk vifanye vitu hivyo viwe vigumu kupatikana wala usivinunue na kuleta nyumbani kwako.

108. Ifanya ratiba yako ya siku iwe rahisi sana kwako kuitekeleza, pia panga mambo yote unayoyaona yana umuhimu mkubwa kwenye maisha yako yawe rahisi kwako kuyafanya, na pia yafanye mambo yasiyo na tija kwenye maisha yako yawe ndio mambo magumu sana kwako kuyafanya.

109. Kwa asili binadamu huwa tunapenda kufanya mambo rahisi yasiyotumia nguvu nyingi. Hivyo tengeneza mazingira ya kufanya mambo unayoyaona ni magumu lakini ni muhimu sana kwenye maisha yako yawe rahisi kwako kuyafanya.

110. Ujenzi wa tabia unahitaji mazingira rahisi na yenye mvuto, kama unatumia nguvu kubwa, na upinzani ni mkubwa sana kujenga tabia mpya ni wazi kuwa huwezi kufurahia tabia hiyo, na pia ni rahisi kukata tamaa na kuendelea na tabia zako za awali.

111. Unapojenga tabia mpya au kukuza tabia nzuri kwenye maisha yako, haitakiwi iwe kama ni changamoto. Ujenzi wa tabia unatakiwa kuwa wa mvuto mkubwa kwako, tabia zinatakiwa ziwe sehemu ya kukupa furaha na mafanikio. Hivyo fikiri tena kujenga tabia unayoipenda kwa kuweka mazingira rafiki kwa utekelezaji wa tabia hiyo.

112. Kuna kanuni inaitwa kanuni ya dakika mbili; kanuni hii inasema unapoanza tabia mpya utekelezaji wake usizidi dakika mbili. Maana yake kama unaaza kesho kuishi tabia mpya jisemee nitatumia dakika mbili tu kuishi tabia hii mpya.

113. Mwandishi James anasema, huwezi kuboresha kitu ambacho hujakianza, kama umeanza tabia mpya ni rahisi kuiboresha kadri siku zinavyokwenda ili iwe sehemu ya maisha yako.

114. Kama unataka kuvunja tabia usizozipenda kwenye maisha yako, unatakiwa kuweka upinzani mkubwa sana kwenye utekelezaji wa tabia hiyo. Ifanye tabia hiyo iwe ngumu na isiyovutia kabisa kuitekeleza.

115. Unaweza kutumia fursa za teknolojia zilizopo ili kuboresha tabia unayoipenda. Mfano kuna wengine wanapenda kufanya mazoezi ya mwili akiwa wanasikiliza musiki, au wengine wakivaa vifaa vya masikioni vinawafanya waongeze umakini kwenye majukumu yao.

116. Kama kuna namna unapata raha unapofanya tabia fulani, ubongo wetu huwa una tabia ya kutukumbusha mara kwa mara kuhusu raha zilizopo katika kufanya tabia fulani. Hivyo unaweza kuhusianisha ujenzi wa tabia mpya na raha ya kitu fulani ili ikusaidie kukuza tabia mpya.

117. Hisia chanya zinasaidia sana kukuza tabia mpya, lakini pia hisia hasi zinaua sana tabia mpya. Siku zote tunapenda kufanya na kurudia vitu ambavyo tunajua tukivifanya tutapewa au tutapata zawadi.

118. Unaweza kujenga mfumo wa ufuatiliaji wa tabia yako, hii itasaidia ili muda wote uwe kwenye ujenzi wa tabia yako. Unaweza kutengeneza form malumu ya kujaza tabia unazoziishi na kama unazitekeleza.

119. Sisi binadamu huwa tunajali sana maoni ya watu juu yetu, hivyo basi unaweza kumpa mtu jukumu la kukusimamia ili uweze kuishi tabia unazozipenda. Kwasababu hatupendi watu watuchukulie vibaya hii itatupa nguvu ya kuitekeleza tabia unayoipenda.

120. Unaweza kutengeneza mkataba wa tabia, mkataba uweke wazi kabisa aina ya tabia unazotaka kuzijenga kwenye maisha yako, utazitekeleza siku gani, kuanzia saa ngapi na kwa muda gani? Pia mkataba huo uweke wazi faini au adhabu ambazo utazipata endapo utakiuka masharti ulivyoonyesha kwenye mkataba, njia hii itakusaidia kujenga tabia na kuziishi kwa mafanikio.

121. Fanya kile unachokipenda kwenye maisha yako, soma kile unachokipenda, na jenga na ishi tabia unazozipenda. Usijenge wala kuishi tabia ambazo huzihitaji kwa kuogopa watu watakuonaje. Chagua tabia sahihi kwako zijenge na ziishi kila siku.

122. Njia nyingine bora ya kuwa na tabia nzuri ya kudumu muda mrefu ni kuchagua kujenga tabia ambazo zinaendana na ujuzi wako, haiba yako, utalaamu wako na jinsi ulivyo. Kwa kufanya hivyo itakusaidia kuwa na utekelezaji mwepesi wa tabia unazotaka kuzijenga.

123. Uchaguzi mbaya wa tabia unaleta utekelezaji mgumu, uchaguzi sahihi wa tabia unaleta utekelezaji rahisi. Chagua tabia kuendana na uwezo wako wa kipekee uliozaliwa nao. Chagua tabia zinazoendana na wewe. Mfano kama uwezo wako wa kipekee ni kuandika, unaweza kujenga tabia za kuandika kila siku na ikawa rahisi kwako kutekeleza.

124. Cheza mchezo unaoendana na uwezo wako. Kama hakuna mchezo sahihi unaondana na uwezo wako, tengeneza mchezo wako mwenyewe kwa kujenga tabia mpya itakayokufanya ucheze mchezo huo.

125. Chagua tabia ambayo utaifanya kila siku, usichague tabia za msimu, tabia za mafanikio zafaa sana kuwa tabia za maisha. Tabia ambazo utazifanya bila kujali unajisikiaje au upo kwenye hali gani, tabia za muda wote na sio za misimu fulani fulani tu.

126. Hata kama zitatokea nyakati utakuwa chini na upo boadi sana, mwandishi anasema ifike mahali upende tu hali za kuboreka, maana hazikwepeki, zipende na zitumie kufanya makubwa. Tuwe na uwezo wa kufaidika na nyakati zote zinazokuja kwenye maisha yetu, hata kama ni ngumu kiasi gani.

127. Kila mtu anaweza kufanya kazi kwa bidii kunapokuwa na hamasa na mazingira ni mazuri. Mwandishi anasema, mafanikio kwenye maisha yanadai matumizi ya nyakati ambazo hatuna hamasa kabisa ya kufanya chohote. Mafanikio na ukuaji mkubwa umefichwa kwenye nyakati ngumu, nyakati za giza, nyakati ambazo hatutamani tena kufanya chochote.

128. Mafanikio sio lengo unalohitaji kufikia au msitari wa mwisho unaotakiwa kuuvuka, bali ni mfumo unaohitajika kuboreshwa na ni mchakato unaotakiwa kuimarishwa kila mara.

129. Kama unapata tabu sana kubadili tabia zako, tatizo sio wewe, tatizo ni mfumo wako wa maisha, mfumo unafanya tabia uliyonayo ijiendeshe yenyewe hata bila wewe kujua. Ukibadili mfumo wako wa maisha ni rahisi kwa tabia kubadilika pia.

130. Until you work as hard as those you admire, don’t explain away their success as luck.

Mwisho; Kitabu hiki ni chepesi sana kusoma, na kina mambo mengi sana mazuri kuhusu kujenga tabia, kuvunja tabia usizozipenda na kujenga nyingine bora kabisa. Nashauri kila mtu akisome kitabu hiki.

@Hillary Mrosso_13.11.2022

/


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X