Rafiki yangu, sina shaka unaendelea vizuri kabisa. hongera sana kwa siku hii ya kipekee sana. siku ya leo ningependa kuongea na wewe juu ya suala moja tu. Na suala hili ni namna ambavyo unaweza kuitumia nguvu ya mara kumi zaidi kufanikisha malengo yako, na kitu chochote kile ambacho umepanga. Kiufupi kwenye hii makala nataka nikuoneshe ni kwa namna gani ambavyo unaweza kuitumia nguvu ya mara kumi zaidi kuhakikisha kwamba unafanikisha makubwa sana.
Utakuwa unajiuliza hii nguvu ya mara kumi ndiyo nguvu gani na inafanyaje kazi?
Na mimi ningependa kuanzia hapo. Nguvu ya mara kumi kumi zaidi iko hivi, kwa chochote kile ambacho unapanga kupanga, unapaswa kukizidisha mara kumi zaidi. Kwa kuanzia tuanze na malengo yako. Kama una lengo lako lolote ambalo umeweka sasa hivi, zidisha mara kumi zaidi ya lengo ambalo umeweka sasa hivi.
Kwa mfano kama umeweka lengo la kuingiza kipato cha milioni moja kwa mwezi. Unapaswa kulizidisha hilo lengo lako mara kumi zaidi. yaani, badala ya kuwa na lengo la kuingiza milioni moja kwa mwezi, kuwa na lengo la kuingiza milioni kumi kwa mwezi.
Kama una lengo la kuingiza milioni kumi, zidisha mara kumi zaidi. Liwe ni milioni 100. Yaani, kitu chochote kile utakachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kwamba unakifanya kwa viwango vya mara kumi zaidi ya kawaida.
Mahusiano yako, yawekee lengo la kuyaboresha mara kumi zaidi.
Biashara yako, iwekee lengo la kuikuza mara kumi zaidi.
Wteja wako, weka lengo la kuwaongeza mara kumi zaidi.
Mtaji wako, weka lengo la kuukuza mara kumi zaidi
Oooh, kama nakuona vile unavyostuka na kuanza kuona kama vile lengo linakuwa ni kubwa sana. na ndio maana, kuna hii nguvu ya mara kumi zaidi.
Maana, uwezo wa hii nguvu siyo tu kwamba upange peke yake. Bali upange na kutekeleza kile ulichopanga. Kwa hiyo, maana yake mipango yako inapaswa kuwa ni mipango ya mara kumi zaidi, lakini sambamba na kuwa na mipango ya mara kumi zaidi, unapaswa kuwa na vitendo ambavyo ni mara kumi zaidi.
Yaani, baada ya kuwa umezidisha lengo lako na kulifanya kuwa lengo kubwa sana. sasa kinachofuata ni wewe kuzidisha kila kitu ambacho utafanya. Unapaswa kuzidisha hatua ambazo unachukua mara kumi zaidi.
Kwa lengo lako la kuingiza milioni moja, pengine ulikuwa umejiwekea kwamba ukiuza bidhaa kwa wateja 10 tu, utakuwa umeweza kulifikia. Ila kwa lengo lako jipya ambalo umeweka. Yaani, hili lengo la mara kumi zaidi. maana yake utahitaji kuhudumia wateja mara kumi zaidi ya wale ambao ulikuwa umepanga kuwahudumia.
Na ili uweze kuhudumia wateja mara kumi zaidi ya wale ambao unawahudumia, maana yake unapaswa kuchukua hatua za kutafuta wateja mara kumi zaidi. Kwa sababu ili uweze kuwa na wateja 100 wanaonunua kwa wiki au kwa mwezi. Lazima uwe na wateja zaidi ya hao. Maana yake kutakuwepo na wengine ambao hawatanunua, sasa baada ya kutoa 100 wanaonunua, ndipo na wewe unakuja kubaki na wale wachache ambao wananunua.
Kwa hiyo basi rafiki yangu, naomba kitu kimoja tu. kuanzia sasa hivi, anza kufikiri mara kumi zaidi ya sasa.
Kama ni pesa, fikiri mara kumi zaidi ya unavyofikiri sasa hivi. chukua hatua mara kumi zaidi ya unavyochukua sasa hivi.
Kutana na watu mara kumi zaidi ya unaokutana nao sasa hivi. piga simu kwa wateja mara kumi zaidi ya unavyopiga sasa hivi.
Fanya mazoezi mara kumi zaidi ya unavyofanya sasa hivi. Hii ndiyo tiketi ambayo inawatofautisha watu ambao wanafanya makubwa na wale ambao wanafanya vitu kwa namna ya ukawaida sana. Kama wewe hutaki kuwa mtu wa kawaida, basi unahitaji kuhakikisha kwamba unachukua hatua za tofauti ili uweze kufika kule unapotaka.
Makala hii imeandikwa na Godius Rweyongeza.
Godius Rweyongeza ni mwandishi wa vitabu zaidi zaidi ya 20. Na ni mwendeshaji wa mtandao wa Songambele. Amekuwa akiandika kwenye huu mtandao huu tangu mwaka 2016. Kitabu chake cha Kutoka Sifuri Mpaka Kileleni kimekuwa #1Best Seller kwa muda sasa kwenye mtandao wa GETVALUE
Baadhi ya makala za Godius Rweyongeza zimechapwa kwenye magazeti makubwa nchini Tanzania likiwemo gazeti la MWANANCHI.
Kupata vitabu vya Godius Rweyongeza unaweza kwa kuwasiliana na 0755848391/ +255755848391 kwa simu au whatsap.
Mtandaoni, vitabu vyake unaweza kuvipata kupitia mtandao wa GETVALUE kwa KUBONYEZA HAPA