WANAOSHEREKEHEA KUHITIMU CHUO TUWAAMBIE UKWELI? AU TUWAACHE KWANZA WAFUMUE NYWELE ZAO ZA GRADUATION?


Siku zinaenda kweli. Mwaka jana kipindi kama hiki hapa kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na picha fulani iliyokuwa inasambaa sana. Picha hii ilikuwa na maneno yafuatayo. Wanaosherehekea kuhitimu chuo tuwaambie ukweli, au tuwaache kwanza wafumue nywele zao za graduation? Kisha lilikuwa linafuata cheko ka mtu anayeonekana kuujua ukweli wanaoenda kukutana nao wahitimu kwenye mtaa.

Mwanzoni nilipoiona picha hiyo sikuipa uzito sana, ila sasa nilikuja kushangaa profesa wa chuo kimoja hapa Tanzania ameiweka kwenye mtandao wake wake wa kijamii.

Hapo ndipo nilipojouliza, hivi huyu profesa anayefundisha wanafunzi  wanahitimu chuo miaka mitatu, minne mpaka mitano. Kuna kitu gani ambacho hakuwahi kuwaambia wanafunzi wake darasani siku zote hizo mpaka anasubiri wanafunzi wafumue nywele zao za sherehe?

Ilibidi nifuatilie kwa umakini sana. Ndipo niligundua kwamba kuna vitu saba ambavyo shuleni huwezi kuambiwa ila mara tu baada ya kuingia mtaani. Vitu hivi utakutana navyo ana kwa ana. Sasa na mimi leo hii napenda niwaulize ndugu wasomaji. Wanaosherehekea kuhitimu chuo tuwaambie ukweli? Au tusubiri wafumue nywele zao za graduation?

Binafsi nasukumwa kuusema ukweli mapema ili kila mtu apate kuujua kabla mambo hayajawa mabaya. Hivyo naomba mnipe nafasi nijimwage na kuusema ukweli kabla mambo hayajawaendea vibaya wasomi wetu. Kitu kimoja ni kwamba ukweli huu sio kwa wasomi wa kike tu ambao wanasuka bali ni kwa wote. 

UKWELI WA KWANZA: MUDA MZURI WA KUANZA MAISHA ILIKUWA KIPINDI UPO CHUO ILA MUDA MZURI ZAIDI WA KUANZA MAISHA NI SASA
Chuo ndio muda mzuri wa kuanza maisha. Huu ndio ulikuwa muda mzuri wa kuziona fursa na kuanza kuzichangamkia. Huu ndio ulikuwa muda wa kutengeneza mzunguko wa watu sahihi. Huu ndio ulikuwa wa kuanza kukutana na watu ambao ungekuja kuingia nao kwenye biashara, watu ambao wangekusaidia kutimiza vipaji vyako na ndoto zako. Huu ulikuwa ni muda mzuri wa wewe kutengeneza marafiki wa kudumu.

Ila sasa kama umechelewa. Basi amua kwamba hiki kitu unaenda kujifanyia kazi sasa hivi. Muda wa kuwa chuo ulikuwa ni wakati mzuri wa wewe kuiangalia dunia inavyokwenda na kuangalia namna ambavyo ungeweza kutafuta au kupata wazo la biashara ambayo sasa hivi ungekuwa unaanza. Sasa kama hukufanya hivyo amua kufanya hivyo kuanzia sasa.
Tafuta fursa ambazo unaweza kuchangamkia mara moja. Wasiliana na watu ambao unaona unaweza kujifunza kwao. Muda ndio huu.

UKWELI WA PILI:  KUHITIMU CHUO SIO MWISHO WA KUJIFUNZA BALI MWANZO WA KUJIFUNZA.
Mtu mmoja amewahi kunukuliwa akisema kwamba mjinga wa karne ya 21 sio yule ambaye hajui kusoma na kuandika. Mjinga wa karne ya 21 Ni yule ambaye anajua kusoma na kuandika ila hasomi wala kujifunza.
Ndugu mhitimu shuleni unafundishwa kusoma na kuandika ila huku mtaani unapaswa kusoma na kujifunza bila kuchoka. Nipende tu kukwambia kwamba dunia ya sasa hivi inabadilika sana. Kompyuta aliyokuwa anaitumia baba na mama miaka ya 90 sio ile ambayo mimi ninaitumia sasa hivi. Redio zenyewe zimebadilika sana tu. Simu zinabadilika kwa kasi, sekta ya afya inazidi kukua na usimamizi wa biashara kwenye zama hizi unabadilika kila kukicha. Ndugu mhitimu, ili uweze kuendana na kasi hii ya mabadiliko yanayoendelea kutokea kila siku basi utapaswa kukaa chini na kusoma vitabu na kujifunza. Sasa hivi husomi kwa ajili ya mtihani wala husomi ile usije ukaachishwa chuo (discontinuation). Sasa hivi unasoma ili kukabiliana na uhalisia.

Sasa hivi hutasoma ili upate maksi za juu . Maana maksi za mtaani hazipimwi kwa viwango vya A,  B+ na B. Maksi za mtaani zinapimwa kwa kiwango cha pesa unachoingiza au kupoteza. Nimeona nikudokeze hili kabla hujafumua nywele zako za graduation.

UKWELI WA TATU: MSIWAPE KAZI NZITO NDUGU NA JAMAA.
Inafahamika kwamba wanachuo wengi wanapohitimu chuo ndio unakuwa muda wao wa kuanza kuzurura kwa ndugu na jamaa. Wanaenda kwa mjomba na kukaa mwezi huku wakiwa wanakula na kunywa kwa kisingizio cha kwamba wanatafuta ajira. Baada ya hapo wanaenda kwa shangazi wanakaa mwezi. Kisha wanahamia kwa bibi wanakaa miezi miwili. Kote huko wanakula na kunywa bila kufanya kazi yoyote kwa kisingizio cha kutafuta ajira. Na kwa kuwa jamii zetu ziathamini sana wasomi basi wanapokelewa kwa mikono miwili. Ila sasa sisi tunaoujua ukweli tunaona wazi kwamba hapa hawa wanachuo wanakosea kula jasho la wengine huku wakiwa hawafanyi kazi yoyote ya maana.

Ndugu mhitimu, Kuhitimu kwako kusiwe chanzo cha wewe kuwabebesha ndugu zako mzigo. Ninachoweza kukwambia ni kwamba chapa kazi. Huku mtaani ni kazi tu. Na wala sio tamthiliya tu. Wala sio facebook tu. Narudia tena huku mtaani ni kazi tu.

Mambo uliyokuwa unayafanya ukiwa chuoni unakaa mtandaoni siku nzima, Sasa yaweke pembeni. Masuala ya kuomba vocha achana nayo. Wewe sasa umekua na hakuna mtu mwingine ambaye unapaswa kumwomba vocha. Nimeona nikwambie ukweli huu mapema kabla hujafumua nywele zako za graduation.

UKWELI WA NNE: AJIRA HAZIPO ILA HAUTAKUFA NJAA.
Nimejaribu kutafuta namna ya kuusema ukweli huu ila nimekosa. Hivyo nausema kama ulivyo. Ajira hamna. Ila ukweli mwingine ni kwamba hutakufa njaa.  Inawezekana wakati unaanza chuo walikuambia kwamba kasome kozi fulani maana ina ajira sana. Lakini sasa uhalisia unaokutana nao baada ya chuo ni tofauti.

Ndugu mhitimu, chuo kimekuandaa na sasa kimekutunuku shahada, stashahada au astashahada. Hii ni hazina. Ukijua kuitumia vizuri hii inawezekana kabisa usikimbilie kutafuta ajira nyingine tena.
Tafuta tatizo ambalo unaona watu wanalo kwenye jamii kutokana na kile ambacho wewe umesomea chuo. Kuanzia hapo anza kuwasaidia watu kutatua tatizo lao.

Inasikitisha kukuta mtu kasoma kilimo miaka mitatu ila anahangaika kutafuta ajira. Sasa unabaki kujiuliza huyu mtu alikuwa anasoma nini darasani. Kama alichosoma hakiwezi kumsaidia yeye kwanza? Na hali kama hii wanayo wahitimu kutoka sekta zote.

Ebu tafuta namna ya kuanza kuitumia taaluma yako kuisaidia jamii. Ukiweza kufanya hivyo jamii nayo pia itakulipa.

UKWELI WA TANO: USIOGOPE KUCHAFUKA
Sasa hapa ndipo kazi ilipo. Wahitimu wengi hawapendi kufanya kazi za viwango vya chini. Kila mtu anahitaji akae ofisini kwenye kiti kinachonesa na kiyoyozi.

Ndugu mhitimu, najua wazi kwamba wewe ni msomi. Ila usomi bila pesa hauna maana. Hi hivyo  mimi nakwambia hivi, usiogope kuchafuka.

Kama kuna kazi ya chini ambayo unaona unaweza kuifanya ifanye badala ya kukaa ukisubiri ajira ya kuweka sahihi tu kwenye kiti kinachonesa. Anzia popote ilimradi panaweza kuanza kukuingia kipato mfukoni mwako.

Ndugu mhitimu, najua wazi kwamba hupendi kilimo na wala hupendi kushikwa na matope. Ukianza kufikiria juu ya wanja yako ya gharama, unaona sio vizuri  kuipeleka kwenye kilimo.

Naheshimu hili sana ila sasa kama  hauna pesa, hiyo wanja yenyewe siitaisha? Bora ukachafuke kwa kulima mchicha ila uwe unaingiza fedha mfukoni kuliko kukaa unazurura mtaani bila mwelekeo.

UKWELI WA SITA:USIPOKUWA MWAMINIFU BASI MAISHA YAKO YATAKUWA MAGUMU SANA

Kuna hiki kijitabia ambacho watanzania wengi wamekibeba. Mtu akipata kazi sehemu basi anaanza kufikiria namna ya kukwepesha baadhi ya vitu kutoka kwenye hiyo kazi yake. Kama ni kijana kapewa duka basi anatafuta kila namna aibe kitu kutoka humo dukani. Kama ni mwajiriwa kaajiriwa sehemu basi anatafuta fursa ili abebe vitu vya huko. Jamani hii hali itaendelea mpaka lini?

Ndugu mhitimu. Uaminifu ni hazina kubwa  sana ambayo unaweza kujenga kwenye maisha yako. Hivyo basi popote pale utakapokuwa anza kwa kujenga msingi wa uaminifu.

Hata kama utaajiriwa sehemu na ukawa unalipwa mshahara kidogo. Usikimbikie kuiba eti kwa sababu hulipwi vizuri. Na wala usikwepeshe kitu Cha kazini au ofisini.

Kama mtu akikuamini kufanya kazi yake, kiukweli ifanye kwa moyo wako wote, nguvu zako zote na pia khwa mwaminifu.

Ndugu mhitimu. Uaminifu unalipa zaidi ya kitu kingine ambacho unaweza kufikiria.

UKWELI WA SABA: ZAMA ZIMEBADILIKA
Kazi ambayo zamani ilikuwa inafanywa na watu 40. Sasa hivi inafanywa na mashine moja tu.

Hali hii imesababisha watu ambao wao hawajiongezei maarifa kutoweka kwenye soko la ajira. 

Ndugu mhitimu, bado kuna mabadiliko makubwa sana yanazidi kutokea. Inawezekana sasa hivi ukapata kazi ila kesho hiyo kazi ikasitishwa baada ya kuletwa mashine moja tu.  Ninachojua mimi kuhusu wewe ni kwamba, unapaswa kujiweka katika namna ambapo kazi unayofanya wewe. Hakuna mashine yoyote duniani yenye uwezo wa kufanya hiyo kazi. Nakuhakikishia ukiweza hicho kitu. Hutakosa kazi ya kufanya na wala hautakosa pesa za kukufanya uishi na utengeneze utajiri.

Na ili uweze kufikia kwenye viwango ambavyo wewe utakuwa na ujuzi ambao hakuna mashine yenye uwezo wa kufanya kazi yako basi utapaswa kufanya kitu kimoja muhimu. Utapaswa kuunganisha ujuzi au taaluma yako ya sasa na kitu kingine cha ziada. Kwa mfano ukiunganisha uhandisi na ubunifu.  Sheria na uandishi. Kilimo na utafiti. Kwa jinsi hiyo hakuna hata siku moja itakuja kupatikana mashine yenye uwezo na ujuzi wa kufanya kazi ambayo wewe unaifanya.

Ndugu mhitimu, nimeona niseme ukweli huu mapema kabla hujafumua nywele zako za graduation. Ili  yakija kukupata ya kukupata. Usije kusema sikusema.

Nakutakia kila la kheri.

Godius Rweyongeza
0755848391
MOROGORO TZ

🔥🔥LEO NIMEONA NITOE ZAWADI YA VITABU VYANGU KWA WAHTIMU WOTE WA CHUO TANZANIA.
Nimeandika vitabu vitano. Na Gharama ya vitabu vyote kwa pamoja ni 37,000/- tu.

Sasa kwa mhitimu au mtu ambaye atapenda kumunulia vitabu hivi ndugu yake mhitimu siku ya leo. Basi atalipia 20,000/- tu ili avipate vitabu hivi vyote vitano.

Vitabu hivi ni pamoja na
1. Kutoka sifuri mpaka kileleni (10,000/-)

2. Tatizo si Rasilimali zilizopotea (10,000/-)

3. Nyuma ya ushindi (5,000/-)

4. Mambo 55 ya KUZINGATIA KABLA YA KUANZISHA BIASHARA (5,000/-)

5. JINSI YA KUIBUA UBUNIFU ULIO NDANI YAKO (7,000/-).

Ila kwa wahitimu na watu ambao watawanunulia ndugu zao wahitimu vitabu vyote kwa pamoja, gharama take itakuwa 20,000/- ni kwa leo tu.

Lipia kwa namba 0755848391 jina Godius Rweyongeza Kisha nitumie ujumbe mfupi wenye neno VITABU. Karibu sana


7 responses to “WANAOSHEREKEHEA KUHITIMU CHUO TUWAAMBIE UKWELI? AU TUWAACHE KWANZA WAFUMUE NYWELE ZAO ZA GRADUATION?”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X