Mwishoni mwa mwezi uliopita nilisafiri kwenda Dar kutembea. Nikiwa Dar nilipata nafasi ya kuongea na mmoja wa rafiki zangu. sijui ilikuwaje lakini kwenye maongezi yetu kuna sehemu tulifika tukaanza kuongelea suala zima la ajira, na hapo ndipo akawa ananiambia kwamba yeye alihitimu mwaka 2006 na kupata ajira miezi mitatu baada ya kuhitimu.
Kwa maneno yake akawa ameianiambia, “siyo kama ninyi vijana wa siku hizi mnahitimu na kukaa mtaani miaka na miaka bila kupata ajira”. Aliendelea kuniambia na hiyo miezi mitatu aliyokaa bila kupata ajira ni sawa na alichelewa kupata ajira.
Siku hizi hali ni tofauti. Vijana wanaozidi kuhitimu kila mwaka ni wengi ila wanaoajiriwa ni wachache sana. Kilio kikubwa cha vijana sasa hivi ni ajira. Sasa nini kifanyike ili kuondokana na hali kama hii?
Sasa viafuatavyo ni vitu ambavyo kwa leo ningependa kushirikisha kuonesha ni kwa namna gani tunaweza kuondokana na tatizo la ajira
Moja. Kufanya kazi kwa bidii kunaweza kukukutanisha meza moja na wafalme
Ukisoma CV za vijana wengi wanajinadi kamawachapakazi na wanaofanya kazi kwa bidii. Na ambao wapo tayari kufanya kazi kwenye mazingira na hali yoyote. (nasema ukisoma CV za vijana wengi kwa sababu mimi mwenyewe hata CV ya kuombea kazi sina na sina mpango wa kutengeneza moja. nataka matendo yangu na kazi zangu tu ziongee mbele ya watu.
Lakini kitu cha kushangaza ni kwamba, vijana hawa hawa ambao wanajinadi kwamba wanaweza kufanya kazi kwa bidii wakiajiriwa hawafanyi kazi kwa bidii. Mwajiri asipokuwepo hawawezi kujisimamia na kuchapa kazi badala yake wanachapa soga.
Ongea na mwajiri yeyote, atakwambia asilimia kubwa ya tatizo analokumbana nalo kwa vijana wa siku hizi anaowaajiri ni uzembe. Mtu hataki kujituma na kufaya kazi kwa bidii.
Inaweza kushanganza ila ni kweli, kijana ameajiriwa anatumia muda mwingi facebook na instagram kwa siku kuliko anavyoutumia kweye kazi yake, asa unashangaa hivi huyu ameajiriwa na kampuni ya facebook au nini kinaendelea.
USHAURI WANGU: vijana wenzangu tupende kufanya kazi kwa bidii. Tukipewa kazi tuifanye kwelikweli kwa viwango vya juu. Kazi ni moja ya kitu ambacho kinaweza kukuinua juu, juu sana. nimekuwa nikiandika mara kwa mara humu kuwa kazi inaweza kukufanya ukutane meza moja na wafalme. Kazi inaweza kukuinua juu.
Ninachojua ni kwamba, unaweza ukawa hauna elimu kubwa, unaweza ukawa hauna ujuzi mkubwa, unaweza ukawa hauna konekisheni kubwa, ila kazi tu ikakuinua.
Sidhani kama kuna mwajiri anachukuia mtu anayefanya kazi kwa bidii. Mtu anayejituma na kufanya kazi kwa viwango vya juu. Hakuna mwajiri wa aina hii. kwa hiyo vijana tupende kazi.
SOMA ZAIDI: WANAOSHEREKEHEA KUHITIMU CHUO TUWAAMBIE UKWELI? AU TUWAACHE KWANZA WAFUMUE NYWELE ZAO ZA GRADUATION?
Mbili, tuwaambie vijana watembee na ujuzi mtaani na siyo Vyeti
Dunia ya sasa hivi imebadilika sana. Kuna kazi au ajira zilizokuwepo siku za nyuma, ila siku hizi hazipo au la zinaelekea kuisha. Siku hizi kuna hizi mashine ambazo zinaweza kufanya kazi ya watu wawili mpaka kumi au hata zaidi kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, mashine moja inakula ajira za watu kumi
Na sasa hivi kuna mshine zinatibu,
Mashine ambazo zinafanya kazi za kihasibu
Mashine ambazo zinafanya kazi za kilimo mpaka mapishi.
na mashine hizi haziitishi mgomo, mashine hizi haziombi kufanya kazi kwa saa chache zinafanya kazi saa 24 siku saba za wiki. Ebu chukulia mfano wa ATM benki. Hii mashine kila siku inafanya kazi, haina likizo na wala haitakuja kulilia likizo hata siku moja, haiwezi kugoma na wala haiwezi kudai ongezeko la mshahara. Gharama pekee inayotumika kwenye hii mashine ni gharama ya kuinunua na gharama za maintainace.
Sasa ili kijana uweze kuishi kwenye ulimwengu huu wa mashine unapaswa kujitofautisha.
Nakumbuka siku moja wenye mtandao wa Quora Kuna mtu aliuliza, nawezaje kuwa Kama Elon Musk, Jeff Bezos au Bill Gates? Justin Musk ambaye ni mke wa zamani wa Elon Musk, alijibu kwa kusema HUWEZI. Ila kama unataka kufikia kwenye viwango walivyofikia basi chagua kitu kimoja kisha bobea kwenye hicho kitu kiasi kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kubobea kwenye hicho kitu kama wewe. Kisha baada ya hapo bobea kwenye kitu kingine. Mfano, bobea kwanza kwenye uhasibu kisha bobea kwenye kompyuta. Baada ya hapo unganisha hivyo vitu viwili kutengeneza kitu kimoja.
Alimalizia kwa kusema, uliweza kufanya hivyo, nakuhakikishia hakuna mtu hata mmoja ambaye anaweza kukufikia kwenye kitu utakachofanya. Na wala hakuna mashine itaweza kuchukua kazi yako.
NDIYO MAANA vijana tunapaswa kutembea na ujuzi mtaani. Mwenye ujuzi halali njaa, mwenye cheti mhhh!
Sasa na wewe Unapaswa kubobea. Dunia ya leo bado inawapenda sana wabobevu na inawalipa vizuri ukilinganisha na watu wa kawaida. Sasa swali langu kwako, unaemda kubobea katika nini?
Kama ungependa kubobea kwenye uandishi hakikisha unajipatia nakala ya kitabu hiki Cha JINSI YA KUWA MWANDISHI MBOBEVU NDANI YA SIKU 30. Bonyeza hapa.
Tatu, vijana tuwe waaminifu
Kuna akili ambazo vijana wengine wanakuwa nazo, zinakuwa siyo nzuri. Mtu anawaza aajiriwe halafu aanze kupiga cha juu. Yaani, aanze kuiba. Uaminifu ni mtaji mkubwa. Watu wanapenda kufanya kazi na waaminifu. Uaminifu ni kitu muhimu bila kujali umeajiriwa au umeajiajiri
Siku za nyuma hapahapa kwenye hii blogu niliwa hia kuandika namna ambavyo kijana mmoja alikusanya vijana wengine na wakaunda kampuni huku wakimshirikisha mmwekezaji. Wazo lao lilikuwa ni kulima mboga mboga, kwa kuanzia na nyanya na mboga nyinginezo.
Walikubaliana na mwekezaji kuwa wao wangekuwa na asilimia sitini ya umiliki wa kampuni (walikuwa vijana watano) na mwekezaji angepata asilimia 40.
Wakati taratibu za kusajili kampuni zikiendelea, mwekezaji alimpa kiongozi wao milioni saba. Mradi ulikadiriwa kuwa wa milioni 30. Kijana alipopokea hela akatokomea kusikojulikana.
Kama vijana tunahitaji kuwa waaminifu kwenye kazi zetu.
waaminifu kwa wale tunaofanya nao kazi
Waaminifu kwa kwenye bidhaa zetu. Ukimuuzia mtu bidhaa, umuuzie bidhaa inayoendana na hela aliyotoa. Kiuhalisia bidhaa yako inapaswa kuwa na thamani zaidi hata fedha inayotoka. Hiki kitu ndicho tupambane nacho. Bila uaminifu, sahau kuhusu mafanikio yoyote yale maishani mwako.
SOMA ZAIDI: Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Mtaji Tanzania
Nne;KIJANA FANYA KITU
Huwa napenda kuwaambia vijana wenzangu kuwa haifai wewe kuendelea kulalamika tatizo la ajira huku ukiwa umekaa kwenye kochi. Ebu fanya kitu chochote kile ambacho ni halali na kinaweza kukuingizia kipato.
Usikae tu na kujiita msomi, huku ukiwa huna hata kitu chochote cha kukuingizia kipato.
Fanya chochote
Uza karanga
Uza madazi, vitumbua n.k.
Najua vitu kama hivi kwa wasomi wengi ni kichekesho, kwa sababu wengi wanapenda wakae kwenye ofisi yenye kiyoyozi. Yaani, mtu amehitimu halafu aanze kuuza mandazi. Inaonekana ajabu kweli.
Ila ushauri wangu kwako kijana mwenzangu ni huu: Fedha zako wanazo watu wengine.Hapo hapo ulipo kuna watu wana fedha zako, ila huwezi kuzichukua hizo fedha kwa nguvu, huo utakuwa ni wizi.
Njia nzuri ya wewe kupata fedha ni kuwapa kitu wanachotaka. Na moja ya kitu ambacho wanataka ni chakula. Kwa hiyo unaweza kuwapa hicho ili wakupe fedha. Ndiyo maana hapo juu nikasema kwamba unaweza hata kuuza mandazi au vitumbua.
Najua wazi kuwa una malengo ya kuwa kwenye ofisi kubwa yenye kiyoyozi, ila hilo kwa saas awacha tuliweke pembeni. Pambana kwanza upate hela.
Najua siyo kitu cha viwango vyako ila kwa kuwa ni halali kinaweza kukufikisha mbali.
Ngoja sasa nikwambie siri ambayo hakuna mtu alikuwa amefikiria kukwambia. SIri yenyewe ni hii. vitu vidogo vina hela aisee! Shhhh! Usimwambie mtu.
Mtu akiwa akiwa ananunua kitu cha shilingi mia moja kama kitumbua. Hajiulizi mara mbilimbili. Anatoa mia au mia mbili na wewe unampa kitumbua chako, na kuendelea mbele.
Lakini ukiwa unauza kitu cha elfu kumi. Aisee, mtu atajihoji sana sana kabla ya kutoa hela yake. Ndiyo maana unaona hata matajiri wakubwa bado wanatengeneza vitu vya hela ndogo kama pipi na kiberiti.
SOMA ZAIDI: Kama Unataka Mali: Maeneo Matano Unapoweza Kupata Mali Halali…
Tuseme kwa mfano umeamua kuuza vitumbua vyako, unaweza kuungana na mwezako. Mkatengeneza ofisi yenu ya uongo na ukweli.
Au kama huoni mwenzako wa kuungana naye, basi unaweza kuajiri kijana mmoja.
Akawa anatengeneza vitumbua halafu wewe unasambaza. Tafuta basikeli hata ya kuazima. Zunguka mitaani, na kwa siku mnajiwekea lengo la kuuza vitumbua 300 mpaka 500. Hiyo ni sawa na elfu 30 mpaka 50 kila siku. Ukitoa gharama uliyoweka kwenye hivyo vitumbua hukosi cha kwako kila siku. Rafiki yangu, miaka mitano mpaka kumi ijayo, tutakuwa hatuongelei kijana wewe ambaye hukuwa na ajira, bali kijana wewe uliyetengeneza ajira za watu. hivi ndivyo watu waliofanya makubwa walivyoanza.
Hivi kweli hata mtaji wa kuanzisha biashara ya karanga kweli utakosa?
Hivi hata mtaji wa vitumbua utakosa kweli rafiki yangu? kweli..
Kama hauna huo mtaji ila una simu kubwa ambayo unaitumia kusoma hii makala. Uza hata hiyo simu kwanza upate mtaji, kisha chapa kazi. siku za mbeleni utanunua simu nyingine.
Nimeeleza zaidi kuhusiana na suala zima la mtaji kwenye kitabu changu cha NGUVU YA VITU VIDOGO KUELEKEA MAFANIKIO MAKUBWA. Kiufupi hiki kitabu unapaswa ukipate na ukifanye kuwa mwongozo kwako, kwa sababu kimeeleza ni kwa namna gani unaweza kutumia nguvu ya vitu vidogo kwenye kila eneo la maisha yako. Na vile unaanzia chini kabisa, basi unahitaji hiki kitabu kama mwongozo wako wa kukusaidia kufanyia mpango kazi wako mpaka ukufikishe kileleni.
Tano: Geuza kitu ulichosomea kuwa ajira
Hivi kwa nini tunasoma? Hizi shahada za awali hizi ni za nini? Haoa naweza kuwa mtazamo tofauti na walio wengi. ila huu ndiyo mtazamo wangu na hiki kitu ndiyo mimi nasimamia. Mimi naamini kwamba, tunasoma ili tuje kutatua matatizo yaliyo kwenye jamii zetu. Tunasoma ili kuja kutengeneza ajira.
Kwa hiyo kwa kitu ambacho umesoma, angalia ni kwa namna gani unaweza kukitumia hicho kitu kwenye jamii yako kusaidia watu.
Umesomea sheria, je, hiyo inawasaidiaje watu waliokuzunguka.
Wewe ni mtalaamu wa kilimo, watu waliokuzunguka wananufaika na utalaamu wako?
Ni mtaalamu sijui wa IT, huo utalaamu wako unauletaje kwenye mazingira yetu ya huku mtaani. Kuna vitu unajua na unaweza kuwa unavichukulia poa, ila watu huku mtaani wanavihitaji sana.
Umesomea masuala ya biashara, wasaidie watu kukuza biashara zao. Zile mbinu ulizojifunza chuoni onogea na watu wenye biashara ndogo huku mtaani ili wazitumie. Hawajui hata namna hata namna ya kutunza hesabu zao za kibiashara, kila siku wanasema kuna chuma ulete anachukua fedha zao. Wasaidie kwenye hilo.
Wasaidie kuwafikia wateja. Wakiona mbinu zako hizo zinawasaidia baadaye ukisema kwamba wakulipe ili mfanye kazi zaidi, watakuwa tayari. Maana watajua unaenda kuwasaidia zaidi.
Kijana msomi, ebu badilisha elimu yako kuwa ajira yako basi. Ebu wasidie watu waliokuzunguka kwanza, watu hao hao watakuwa tayari kukulipa, maana wewe ukiwapa mbinu za kuwainua hawawezi kukuacha.
SOMA ZAIDI: Cha kufanya pale wenzako wanapokuzidi elimu, kipaji, ujuzi konekisheni n.k.
Sita, Vijana tujitangaze
Kama una ujuzi au una kitu chochote ambacho unajua kinaweza kusaidia watu , kitangaze watu wakijue. Kuwa na bidhaa nzuri bila kuitangaza kwa watu ni sawa na kujinongongeza mwenyewe kwa kumwambia binti kuwa nakupenda kwenye giza.
Ukiwa na bidhaa,
Saba; Vijana tushikane mkono
Njia pekee ambayo tunaweza kusaidia vijana kuondokana na hili tatizo la ajir ni kuwashika mkono au kwa lugha ya mtaani kuwaungisha pale wanapokuwa na bidhaa au wnapoonesha juhudi za kufanya kitu fulani. Tusapoti juhudi za vijana wenzetu.
Ni kweli mtu anaweza kuwa ameanza kwa kufanya kitu kwa udogo, ila tukizidi kumsapoti kitakua.
Hapa naongea na ninyi nyote wenye tabia za kupenda vitu vya nje ya kudharau vitu vya ndani. Utasikia mtu anasema, aah, kitu chenyewe kimetengenezwa na mtanzania. Wabongo hakuna kitu chochote.
Tukisapotiana sisi vijana tutafika mbali.
Moja ya ndoto yangu kubwa ni kuona watu wakiacha kwenda China kutafuta bidhaa. Badala yake vitu hivyo wavipate hapa nchini. Mfano, badala ya mtu kwenda china kununua nguo, kwa nini vijana wa kitanzania tusitengeneze nguo na kuziuza hapa kwa bei sawa na ile ya china.
Kuna vijana wengi wanashona nguo. Ila je, tunawasapoti.
Tunataka wainuke.
Jamani, tuwasapoti watu wanaofanya vitu.
Mtu akianzisha mgahawa kanunue chakula kwake
Mtu akilima mboga, nunua kwake.
Mtu akiinua kipaji chake, kisapoti
Tatizo la watu ni kwamba unaweza kuwa unapambana na bado wanataka wakija kwenye biashara yako uwape vitu bure. Mtu umepambana na kupata mtaji wako na sasa umefungua duka,, wanataka wakija kwako uwape vitu bure tu. Wengine wanakopa na kulipa hawalipi. Hivi kweli, tutafika kwa namna hii?
Vijana tusapotiane.
Tena inabidi tuanze kusapotiana kwa vitendo kuanzia sasa hivi. Ebu shirikisha hii makala kwenye makundi mengine ya whatsap ili vijana wengi wasome ujumbe huu. hakikisha kwamba hakuna kijana unayemjua ambaye hajasoma huu ujumbe.
Subscribe kwenye channel yangu ya youtube pia. Enhee, hapo naona sasa umeanza kunielewa kwenye dhana nzima ya kusapotiana.
Nakaukaribisha pia upate vitabu vyangu vya NGUVU YA VITU VIDOGO KUELEKEA MAFANIKIO MAKUBWA na JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO kila kitabu ni elfu ishirini (20,000). Ukituma 40,000/- tu unapata vitabu vyote viwili na nikakusafirishia bure.
Karibu sana
umekuwa nami Godius Rweyongeza
Kupata makala zaidi kutoka kwangu weka mawasiliano yako hapa chini ili uendelee kujifunza zaidi kutoka kwangu kila siku. Jaza taarifa zako hapa
Kwa mawasiliano na mimi tafadhali usisite kutuma ujumbe kwa Email: songambele.smb@gmail.com
Whatsap +255755848391
For Booking: songambele.smb@gmail.com
One response to “Namna ya kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana. Njia Saba Zilizothibitishwa (Njia Namba 2, 4 na 7 ni muhimu sana)”
I need to change my life and to give out positive perception to my community