Hatutoki Hapa Mpaka Tushinde


Kwenye makala ya jana, kama utakumbuka, niliekeza juu ya fikra ambavyo zinaweza kukupelekea wewe kupata au kutopata matokeo.

Lakini niligusia hadithi fupi ya wanajeshi walioenda kupigana na jeshi kubwa, kapteni wa jeshi hilo akawa anawaambia kuwa hatutoki hapa mpaka tushinde.

Leo hii nipo hapa Kwa mara nyingine KUELEZA zaidi juu ya hii dhana ya hatutoki hapa mpaka tushinde.

Kwa lugha nyingine naweza kuiita ung’ng’anizi.

Fikra ya aina hii unaihitaji sana hasa unapoendea MAFANIKIO MAKUBWA. Ni mara nyingi sana utahitaji kusema, sitoki hapa mpaka nitoboe.

Kuna wakati unahitaji kuonana na mkuu Fulani, halafu wasaidizi wake wanakuzia usionane naye, jiambie sitoki hapa mpaka nionane naye.

Nakumbuka siku kadhaa zilizopita nilitoka ofisini kwangu saa 11 hivi, kwenda kwenye duka la Airtel. Nilikuwa nahitaji router Kwa ajili ya ofisi yangu.

Tangu asubuhi, nilikuwa nimetingwa na majukumu, hivyo sikuweza Kutoka mapema, na hii jioni saa 11, ndiyo ulikuwa muda wangu pekee

Laiti ningesema kesho, nisingepata pia muda wa kufanya hivyo asubuhi, maana muda wangu hasa wa asubuhi Huwa nauheshimu sana.

Lakini isitoshe hiyo router ilitakiwa kuwepo ofisini KABLA ya saa Moja kesho yake, la sivyo kazi zisingefanyika Kwa ufanisi.

Kilichotokea, nilichukua boda chap Kwa haraka kuwahi kwenye ofisi za Airtel na pale nilikuta wamefunga.

Kitu cha kwanza kabisa, niligonga mlango.

Kwa bahati nzuri mlangoni walikuwa hawajatoa Ile alama ya PUSH. lakini wakati huohuo walikuwa wamewekwa alama ya CLOSED.

Nilichofanya niliPUSH mlango. Ila haukufungua maana ulishafungwa, ilibidi nitulie mlangoni.

Mdada mmoja wa ndani akaanza kunionesha kuwa pamefungwa, na Mimi nikawa namwonesha kuwa pameandikwa PUSH.

Mwisho alitoka jamaa mmoja (nadhani ndiye baunsa wao😁😁) akafungua mlango.

Alivyofungua mlango TU, nikamwambia nilichokuwa nataka, na nikamwambia naihitaji sasa hivi. Nikamalizia Kwa kusema, siondoki hapa mpaka nipate hii router.

Jamaa akasema, ebu ngoja niongee na wenzangu.

Wakati huohuo, bodaboda niliyekuwa nimekuja naye alikuwa hataki kuondoka (inaonekana naye alikuwa kinga’anganizi!). Alishaona FURSA, nadhani alikuwa anajisema kimoyomoyo,  huyu jamaa nimekuja naye bora nisiondoke haraka, maana asipohudumiwa nitakuwa boda wa kumrudisha, napiga Hela mara mbili😁.

Akawa akiniambia wamefunga tuondoke. Ilibidi nimpuuze tu.

Baada ya muda Sasa, ndipo yule bausa alirudi na kuniruhusu niingie ndani na huduma nikapata.
Sitoki hapa mpaka kieleweke.

Kwenye biashara na kwenye maisha, hasa unapokuwa unapambania ndoto zako kubwa, unahitaji kuamua nitapambania malengo na ndoto zangu kubwa bila ya kurudi nyuma, mpaka kieleweke. Ni au nifanikishe hizi ndoto zangu kubwa, au nife nikiwa nazipambania.
Sing’atuki hapa, mpaka kieleweke.

Wakati mwingine kwenye kung’angania hatupata kile tunachotaka siku hiyohiyo, itatuchukua muda kuweza kufanikisha hicho tunachotaka, ila ukweli ni kuwa, tukiwa ving’ngang’anizi ni wazi kuwa lazima tu tutatoboa.

Rafiki yangu, kwa leo nadhani inatosha, utakuwa umeweza kupata mengi kutoka kwenye somo la leo. Mimi nikutakie kila la kheri

Tukutane kesho kwenye somo jingine zuri kama hili, lakini kabla kabisa hujaondoka kabisa. Hakikisha umesoma makala hizi

  1. Kitu Kimoja kinachokwamisha mafanikio ya watu wengi
  2. Kama haupo tayari kupoteza, hautaokota


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X