Leo Na Mimi Nataka Niseme Kitu Kuhusu Gari Ya Masoud Kipanya


Watu wenye kichaa cha kutosha kiasi cha kufikiri wanaweza kuibadili dunia, ndio ambao huibadili-Steve Jobs kwenye tangazo la THINK DIFFERENT la mwaka 1997-2002

Takribani siku mbili zilizopita Masoud kipanya alizindua gari ya umeme ya kampuni ya Kaypee Motors. Kitu ambacho ni cha kipekee sana hasa kwenye mazingira yetu. Asubuhi ya leo nilipotazama hotuba yake wakati anazindua gari yake,ilikuwa ni kama naangalia hotuba ya Steve Jobs akizindua iphone ya kwanza kabisa mwaka 2007. Ilikuwa inahamaisha lakini pia inakufanya wewe uweze kufikiri kwa ukubwa zaidi na wakati huohuo unaona kwamba yajayo yanafurahisha.

Sasa kwanza lazima tukubaliane kwamba gari ya Masoud na kitu alichofanya kiujumla ni kitu ambacho kinawasha moto miongoni mwa vijana wengi wa kitanzania wenye ndoto kubwa. kitu hiki kinastahili pongezi na ndio maana nimeandika makala hii…

Kwa kawaida vitu hivi huwa vinaonekana vigumu pale kunapokuwa hakuna mtu ambaye amewahi kuonekana akifanya vitu vya tofauti. Ila sasa anapotokea mtu katika jamii yenu akafanya kitu cha tofauti basi kinakuwa ni kiashiria kuwa wengine pia wanaweza na hivyo, watu wengine  watajitoa kuhakikisha kwamba wanafanyia kazi ndoto zao.

Jamii nyingi za kitanzania na za kiafirika kiujumla zimeaminishwa kwamba kuna vitu ambavyo huwezi kufanya kwenye maisha yako bila ya kuwa msaada wa mtu yeyote nyuma yako. Na kiufupi inaaminika kwamba vitu vingine wanaweza kufanya wazungu tu na siyo waafrika au watanzania.

Ndio maana ukizunguka mtaani utasikia watu wanasema maneno kama kazi ya mzungu, utasikia wengine wakisema kwamba mzungu noma.

Nimekuwa nikisisitiza kwa watu kupitia makala zangu mbalimbali kuwa kila mtu ana uwezo mkubwa uliolala ndani yake ambao anaweza kuutumia kufanya makubwa. Ila watu wengi wamekuwa hawatumii uwezo huu na hii inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo jamii zetu ambazo haziamini katika ndoto na vitu vikubwa,. Na hata mfumo wa shule.

Lakini tafiti zimeonesha kuwa hata wale ambao wanaonekana wamefanya makubwa hapa duniani, siyo kwamba wanakuwa wametumia uwezo wao wote, bali wanakuwa wametumia chini ya asilimia kumi tu ya uwezo wao.  Sasa sijui wewe unatumia asilimia ngapi ya uwezo wako. Ila kikubwa ni kwamba ukikazana tu hata kutumia asilimia kumi ya uwezo wako, utaweza kufanya makubwa sana.

Na unachopaswa kufahamu ni kwamba uwezo wako hauwezi kuutumia ukaisha. Kadiri unavyoutumia ndivyo unavyozidi kubarikiwa zaidi. Labda swali la uchokozi tu, umeshawahi kusikia kwamba Masoud ameacha kuchora kwa sababu kaishiwa na mawazo (ideas) za kuchora! Au kwamba hajaweza kuchora kwa sababu ametumia uwezo wake wote umeisha? Umewahi kusikia hilo..

Unachopaswa kufahamu ni kwamba kadiri unavyotumia uwezo wako, ndivyo uwezo wako unavyozidi kuongezeka zaidi… hata kama ungekuwa unaishi miaka buku, bado tu uwezo wako ungekuwa unazidi kumeremeta! Ndio maana hautakaa usikie kwamba Masoud ameshindwa kuchora kwa sababu kaishiwa…

Labda aamue tu.

Sasa na wewe ungeweza kuutumia uwezo huu wala si ungefika mbali?

Kwa maoni yangu kitu alichofanya Masoud ni mapinduzi makubwa na moto ambao ameuwasha kwa vijana wengi wa kitanzania. Siku siyo nyingi vijana wengine zaidi watakuwa wakizipambania ndoto zao siyo tu kwa kuanzisha vitu na kuishia njiani, bali kwa kuhakikisha kwamba wanazifanyia kazi ndoto zao mpaka zinatimia.

Na kwa leo nimeona niandae mambo sita makubwa ya kujifunza kutoka MASOUD KIPANDA NA NDOTO YAKE YA GARI LA UMEME.

KWANZA; KABISA NI KUWA NDOTO KUBWA.

PILI; ANZA KUFANYIA KAZI NDOTO ZAKO

Uwepo wa mitandao ya kijamii umekuwa ni baraka na wakati huohuo umekuwa kama karaha vile. Mtu akifikiri kufanya kitu hata kama hajakiweka kwenye vitendo anaingia mtandaoni na kuanza kujitangaza.

Ndio maana ukiingia kwenye mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na instagram utakutana na vitu vya ajabu  kweli.

Kuna watu ambao wanajiita wajasiriamali wakiwa hawajawahi kufanya biashara yoyote ile maishani mwao. Ila ukiangalia profie zao wanajiita maCEO wa kampuni.

Kuna watu wanajiita waandishi wakiwa hawajawahi kuandika hata sentensi moja.

Kuna watu wanajiita wachoraji wakiwa hawajawahi kuchora hata mchoro kimoja. Unajua kwa nini?

Kwa sababu ni rahisi kuongea kuliko ilivyo rahisi kufanya.

Sasa ninachotaka wewe ufanye siyo tu uwe muongeaji, bali uwe mtu wa vitendo. Na hili unaweza kulifanya.

TATU IPE NDOTO YAKO MUDA

Kuna mtu anapenda akiwa na ndoto kubwa leo hii, kesho yake awe ameifanikisha. Siyo kweli. Ndoto kubwa inachukua muda na inahitaji muda kuweza kuifikia.

Kila mara nimekuwa nikiongea na vijana na kuwauliza una mipango gani miaka mitano au kumi ijayo. Ila cha kushanganza ni pale ambapo mtu anakushangaa. Utakuta mtu anasema yaani, wewe unaongelea mambo ya miaka 10 ijayo leo hii?

Mwingine atakwambia “mimi nahangaika na leo, kesho itajipa yenyewe”.

Ngoja nikwambie kitu.

Kama unataka kufanya makubwa na kama unataka kufika mbali, kuwa na ndoto kubwa ambayo unaifanyia kazi.

Inaweza kuchukua muda kufikiwa, ila ukweli ni kwamba inawezekana.

jinsi ya kufikia ndoto zako
Kupata kitabu hiki wasiliana nami kwa 0755848391

NNE; KUBALI KUANZIA CHINI

Ndio unapaswa kuwa na ndoto kubwa, ila unapaswa kuwa tayari kukaa chini na kuanza kuifanyia kazi ndoto yako hata kwa kuanzia chini.

Ndoto kubwa haifanyiwi kazi kwa siku moja na kukamilika. Unahitaji kuanzia chini, unapaswa kuanza na kile ulichonacho na kukifanyia kazi na kisha kuendelea kukuza kile kidogo ulichonacho.

Na sehemu nzuri ya wewe kuanzia ni kuanza kuitumia MITAJI 8 ILIYOKUZUNGUKA sasa hivi.

TANO;UKISIBURI MSAADA UFANYIE KAZI NDOTO YAKO, UTASUBIRI SANA

Yaani, sijui ni nini huyu alikuja na hili suala la misaada. Unakuta mtu anataka akaombe msaada wa kufanyia kazi kila kitu ambacho anakifirikia kwenye maisha yake.

Muda mwingine kuna vitu ambavyo unaweza kuanza kuvifanyia kazi bila hata ya kuhitaji msaada. Unaweza kudhani unahitaji msaada, kumbe huo msaada wenyewe utaishia tu kukuharibu na kukufanya ushindwe kufanikisha ndoto zako.

Ujue hili suala la misaada linafanya watu wasifikiri nje ya boksi. Unakuta mtu ana vitu vya kumsaidia kufanikisha ndoto yake ila tu kwa sababu akili yake ameiaminisha kuwa bila msaada haiwezi, utakuta kwamba anaendelea kusubiri msaada.

Nakumbuka niliwahi kukutana na kijana mmoja aliyekuwa na ndoto ya kufuga kuku. Nyumbani kwao kulikuwa na eneo kubwa tu la kumwezesha kufanya hivyo,ila unajua nini? Alikuwa amesubiri siku moja litokee zari la mentali ili aanze kufanyia kazi hiyo ndoto yake.

Naomba unisikilize wewe mwenye ndoto kubwa. ni kweli maishani kuna bahati, ila sasa bahati haimfuati mtu ambaye amelala kitandani na kuisburi. Bahati wanakutana nayo watembeaji…

Kama na wewe unataka bahati ya kukusaidia kufanikisha ndoto yako, basi utapaswa kuanza kufanyia kazi ndoto yako, ndipo utajiweka kwenye nafasi ya kukutana na bahati. Sijui unanielewa hapo, au niongeze sauti….

Basi bana, niache kwanza niendelee…

SITA; UNAWEZA KUTENGENEZA NJIA PASIPO NA NJIA

Njia pekee ya wewe kutengeneza njia pasipo na njia ni wewe kuhakikisha kwamba unapita eneo hilo kila siku bila kuacha. Siku ya kwanza hakuna kitu kitaonekana. Kadhalika siku ya pili mpaka hata ya 100 ila uhakika ni kwamba baada ya siku 365, eneo ambalo unapita kila siku. Kuna njia ambayo itakuwa imeshaanza kuonekana kuwa ipo.

Sasa hivyohivyo kwenye ndoto yako. Ukianza leo hii kuifanyia kazi ndoto yako, utaanza kuonekana kichaa kwa kufanyia kazi kitu ambacho hakiwezekani kabisa. ila ukweli ni kwamba kama hautakata tamaa, miaka kadhaa mbeleni, basi na wewe utakuwa na kitu ambacho unaweza kuongelea mbele ya watu na kuonesha kuwa kweli nimeweza kufanya kitu cha maana.

Nakuamini wewe

Naamini unaweza

Usiniangushe

Tukutane kwenye jukwaa la wanamafanikio

Ni mimi

Godius Rweyongeza

0755848391

Morogoro-Tz


One response to “Leo Na Mimi Nataka Niseme Kitu Kuhusu Gari Ya Masoud Kipanya”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X