Jinsi Ya Kupata Ushawishi Mkubwa Miongoni Mwa Watu


Rafiki yangu mpendwa salaam,

Umeshawahi kuona hili, unakutana na mtu, anakwambia au unamwambia kwamba nakukumbuka sura yako, ila sikumbuki jina lako. Sijawahi kukutana na mtu ambaye anakumbuka jina la mtu ila amesahau sura yake. Kwenye makala ya leo tunaenda kuangazia sula zima la MAJINA YA WATU. Tutaona njia rahisi utakayoitumia kupata majina ya watu, kukumbuka majina ya watu.

Hivi umeshawahi kujiuliza ni kitu gani ukikifanya, kwa watu watu watapenda sana kuendelea kuwa karibu na wewe na watavutiwa kuonana na wewe mara kwa mara. Naam, kitu cha aina hiyo kipo.

Kitu hiki ni kukumbuka majina ya watu. Hakuna mtu hata mmoja ambaye huwa anachukia kuitwa jina lake. Kila mmoja huwa anapenda sana kusikia akiitwa kwa jina lake.

Hivyo kama kuna kitu cha maana sana ambacho unaweza kufanya, basi kitu hicho ni kuhakikisha kwamba mara zote unakumbuka majina ya watu. Majina ya watu ni silaha kubwa sana ambayo unapaswa kuitumia kwenye maisha yako.

Nadhani imewahi kukutokea ukawa kwenye kusanyiko la watu na kukawa na mzungumzo ambayo yanaendelea. Mara ghafla ukasikia kwamba kuna kikundi cha watu wanataja jina lako. Linaweza kuwa ni eneo lenye kelele nyingi sana, ila kile kitendo cha wewe kusikia jina lako likitajwa na wale watu, kinakufanya  wewe uanze kufuatilia yale mazungumzo yao hata kama wale watu mwanzoni ulikuwa hufuatilii mazungumzo yao.

Hiki ni kiashiria tosha kuonesha ni kwa namna gani huwa tunaweka nguvu kubwa kwenye kufuatilia majina yetu na kutaka kujau ni kwa na mna gani watu wanaongea juu yetu.

Hivyo, basi kuanzia leo hii nakupa jukumu moja tu. Jukumu la kuhakikisha kwambna kila mtu ambaye wewe unakutana naye unakumbuka jina lake. na hili litawezekana kama utafuata mambo yafuatayo.

Kwanza, kama utahakikisha kwamba kila mtu ambaye unakutana naye unamsikiliza vizuri pale anapokutajia jina lake. MARA NYINGI WATU huwa wanasahau majina ya watu, ila kitu kikubwa sana ambacho uwa kinawafanya hao watu wasahau majina ya watu ni kwa sababu huwa hawako makini kwenye kusikiliza hayo majina mara ya kwanza kabisa. unakuta kwamba mtu anataja jina lake lakini anayetajiwa jina hilo, hayuko makini kusikiliza.

Sasa kama wewe unataka kuhakikish kwamba unakumbuka jina la kila metu  ambaye unakutana naye, kitu cha kwanza kabisa, ni kuhakikisha kwamba unamsikiliza kwa umakini mtu huyo anapokuwa anakutajia jina lake.

Lakini siyo tu kumskiliza kwa umakini, baada ya huyo mtu kukutajia jina lake hakikisha kwamba unatumia jina la huyo mtu kwenye mazungumzo. Litumie mara kwa mara kwenye mazungumzo na kwenye maeneo ambapo unaona kwamba linafaa kutumiwa. Mtu asiishie tu kujitambulisha kwako, halafu wewe ukawa hujatumia jina lake kwenye maongezi naye.

Pili, kama mtu amekutajia jina lake na wewe hujalisikia. Basi hakikisha kwamba unamwuliza vizuri ili arudie kukutajia jina lake kwa usahihi. Usiishie tu kusema kwamba ahaa, ok sawasawa.

Tatu, mara zote hakikisha kwamba unajua namna jina la mtu linavyotamkwa na linavyoandikwa. Kuna mtu anaweza kukutajia jina lake ukawa unajiuliza hivi hili jina linaandikwaje, au linatamkwaje, kuwa makini kwenye hilo. Mara zote hakikisha kwamba unajua jina la mtu linavyoandikwa na linavyotamkwa pia.

Lakini pia katika ulimwngu wa leo, unaweza kupata jina la mtu kupitia intaneti, bado ukiongea na huyo mtu utapaswa kumwuliza namna sahihi ya kutamka hilo jina ili huyo mtu aweze kujitambulisha kwako kwa usahihi na wewe uweze kutambua jina lake.

Nne, kama mtu huyo anatambulishwa kwako na mtu mwingine, hakikisha aliyemtambulisha kwako amelitamka vizuri jina la mhusika na wewe umelisikia. Kama hilo jina hujalisikia vizuri, usikubali yapite. Maana mara nyingi watu huwa wanaona kama hawatakuja kuonana na mhusika ambaye wameongea naye, ila ukweli ni kuwa unapaswa kulikumbuka vizuri jina la mtu, hata kama unahisi huyo mtu hutaonana naye tena maishani mwako.

Njia nzuri ya kupata majina ya watu

Njia nzuri ya kupata majina ya watu ni wewe kujitambilisha kwa hao watu na kuwaambia kwamba wewe unaitwa…. Na kuwauliza wao wanaitwa akina nani? Hakikisha kwamba unajitambulisha kwa watu unaokutana nao punde baada ya kuwa umekutana nao.

Ukiacha kujitambulisha kwa hao watu na ukaacha muda ukapita, nakuhakikishaia kwamba, baada ya muda  wa kukaa na huyo mtu, utajikuta kwamba umezoea kukaa naye ila humjuui jina lake, na itakuwa ni vigumu kwako kuweza kumuuliza tena, maana utaogopa kuonekana kama mtu ambaye hajali muda wote huo hujauliza jina lake na sasa hivi ndio unataka kuuliza jina lake.

Kwa hiyo, unapouktana na mtu, jitambulishe, na muulize yeye jina lake.

Kisha litumie hilo jina kwenye mazungumzo yako na yeye bila kurudi nyuma.

Kwa mfano, mimi naitwa Godius Rweyongeza, na wewe ni……(EBU JAZA JINA LAKO KAMILI, BARUA PEPE NA NAMBA YAKO YA SIMU HAPO CHINI). Nitakupigia simu kukupongeza kwa kusoma makala hii.

Sasa ukijua majina itakusaidia nini

Kwanza itakusaidia kuteka umakini wa mtu. Ngoja nikupe mbinu ambayo utaitumia siku ya leo. Unapotaka hapa fanya kitu kimoja tu, nenda uulize jina la mtu ambaye hujawahi kukutana naye na wala hajui jina lako. Ukishajua jina lake, nenda uonane naye. Kisha ukionana na huyo mtu, mchangamkie. Mtaje jina lake kisha msalimie. Kwa kufanya kitu hicho kidogo tu, utaona ni kwa namna gani huyo mtu ataanza kukuuliza hivi jina langu umelifahamuje. Na utaona namna ambavyo huyu mtu atakuwa tayari kukusikiliza kwa umakini zaidi kwenye kile unachoongea.

Ukijilijua jina la mtu na ukalitumia jina hilo kwenye mazungumzo, basi nakuhakikishia kuwa  huyo mtu utamvuta umakini wake. na hata kama huyo mtu alikuwa na mambo mengi ambayo anayafanyia kazi, nakuhakikishia kuwa huyo mtu ataacha kila kitu na kukusikiliza wewe kwanguvu zako zote.

Pili, majina utayatumia kwenye mahusiano ya kawaida ya kila siku. Pata picha leo hii mtu amejitambulisha kwako, halafu kesho, ukakutana tena na huyo mtu. Ukamwita jina lake na ukaendelea kuongea naye kwa ustadi wa hali ya juu kuhusuaiana na kitu fulani. Ni wazi kuwa huyo mtu atapenda sana, kuwa karibu na wewe na hivyo, itakusaidia wewe kujenga mahusiano makubwa zaidi pamoja na yeye.

Tatu, Kwenye biashara. Kama mfanyabiashara, unakutana na watu wengi, na kama mfanyabiashara unafanya kazi na watu wengi, ambao wanaweza kuwa ni wafanyakazi, wahisani, wapambe, wawekezaji, washirika n.k.. Rafiki yangu, unahitaji kuhakikisha kwamba unakumbuka majina yao.

Tatu kwenye mauzo, utatumia majina ya watu kwenye mazungumzo na watu ili kuweza kuwauzia. Mara zote. unapokuwa unafanya mazungumzo ya mauzo hakikisha kwamba unatumia majina ya watu kwenye mazungumzo nao.

Nne, kwenye kampeni. Kama wewe ni mwanasiasa na unataka kupata ushawishi mkubwa wa watu, basi kumbuka majina ya hao watu.

Kwenye matangazo, ulimwengu wa sasa hivi umerahisha sana. Unaweza kufanya matangazo kwa njia mbalimbali, na kwa kutumia hizi njia unaweza kutumia majina ya watu na kuyataja. Mfano, utangazaji wa kutumia baruapepe…au kwa kutumia njia ya simu. Bado unaweza kutaja jina la mhusika na hivyo kuendelea kuvuta umakini wake kwenye kukusikiliza.

Endapo utatumia vizuri hizi mbinu ambazo nimezianinisha hapa, ni wazi kuwa baada ya muda utakuwa superstar kwenye kukumbuka majina ya watu. Utaachana na dhana ya kwamba nakukumbuka  sura ila sikumbuki jina lako.

Jina la mtu ni muhimu sana, ndio maana leo nimezama ndani zaidi kueleza hiki kitu.

Unaweza kuwashirikisha wengine makala hii pia kwenye mitandao ya kijamii

Makala hii imeandikwa na Godius Rweyongeza.

Baadhi ya makala za Godius Rweyongeza zimechapwa kwenye magazeti makubwa nchini Tanzania likiwemo gazeti la MWANANCHI.

Kupata vitabu vya Godius Rweyongeza unaweza kwa kuwasiliana na 0755848391/ +255755848391 kwa simu au whatsap.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X