Home


  • Namba Zetu Za Malipo

    Namba za malipo ya vitabu:

    Namba za lipa

    TIGO PESA: 19016638 Jina ni SONGAMBELE CONSULTANTS

    M-PESA: 5564517 jina ni GODIUS GORDIAN RWEYONGEZA

    Namba za kawaida

    AIRTEL MONEY: 0684408755
    TIGO PESA: 0655 848 392
    M-PESA: 0745 848 395

    Kote jina ni GODIUS RWEYONGEZA

    NB: Kama namba ya malipo anatumiwa mtu ambaye yuko nje ya nchi. Iandikwe Kwa kuanza na +255

    Kwa hiyo namba zinazotumwa nje ya nchi zitakuwa
    Airtel money: +255 684 408 755
    TIGO PESA: +255 655 848 392
    M-PESA: +255 745 848 395

    KOTE Jina ni GODIUS RWEYONGEZA

    Kama malipo yatakuwa yanafanyika kupitia benki.

    Yafanyie kupitia

    1. CRDB BANK: 0150770710200
    2. NMB BANK: 22110047274

    Kote jina ni GODIUS GORDIAN RWEYONGEZA

  • Wasiliana na Godius Rweyongeza Sasa

    Habari yafuatayo ni mawasiliano Unayoweza kutumia kumpata GODIUS RWEYONGEZA

    Simu: +255 (0) 684408755

    Whatsap: +255 (0) 755848391

    Email: songambele.smb@gmail.com

    Kupata vitabu vyake wasiliana Moja kwa Moja na +255 (0) 684408755 (more…)

  • Njia nzuri ya kuwaambia watu wakulipe katika kipindi hiki ambacho gharama za miamala zimeongezeka

    Nakumbuka mwaka juzi baada ya kuwewa kwa tozo za miamala kwa njia ya simu niliandika makala moja ndefu sana kuhusiana na namna ambavyo tungeweza kukabialiana na hiyo hali kwa ustadi zaidi.  Utakumbuka kwenye hiyo makala nilieleza wazi kuwa moja ya eneo ambalo tunapaswa kulitumia vizuri kwenye kuweka akiba katika kipindi hicho ambacho miamala ya simu ilikuwa imeongezewa tozo ilikuwa ni benki. Sasa hivi ninapoandika hapa, benki nako kuna makato, sasa swali ni je, wapi tena tuweke  fedha yetu. Malipo yetu yafanyikeje katika kipindi hiki.

    Kabla sijaandika sana kabisa, ningependa kusisitiza jambo moja tu. Ni ukweli kutuma au kupokea fedha kwa njia ya benki au simu hakutakwepeka kwa asilimia 100. Na njia ambayo ninakuelekeza leo, inafanya kazi sanasana  kama mtu anakutumia hela na wewe huna shida nayo ya haraka. Ila kama fedha hiyo unaihitji kuitumia leo au kesho, basi njia hii haitakufaa kiviile, katika mazingira kama hayo, benki au miamala ya simu ndiyo utalazimika kutumia. Ila siyo vibaya ukiifahamu hii njia, ninaamini muamala mmoja mmoja unaweza kuamua kuwa utumwe huku.

    Na njia hii ninayoiongelea ni mtu kukuwekea fedha zako kwenye akautni za uwekezaji za UTT

    Kwa yule ambaye hajui UTT AMIS ni taasisi ya kiserikali iliyo chini ya wizara ya fedha.Kazi kubwa ya taasisi hii ni kukusanya fedha za watu wenye mitaji midogo na mikubwa, kisha kuwekeza fedha hizi kwa niaba ya hao watu.

    Faida yote inayopatikana kwenye uwekezaji huu, inakuwa ni faida ya wawekezaji husika.

    Katika hali ya tozo ambayo tunapitia kwa sasa, tumefikia hatua ambapo mtu utahitaji kuwekeka fedha zako huku. Kwa nini

    Kwanza kama mtu anakuwekea fedha huku makato ni madogo wakati anakuwekea, makato ni ya mtandao wa simu husika na wala hata hakuna tozo za serikali.

    Pili ni kuwa fedha yako ikikaa huku inapata ongezeko la thamani. Ikumbukwe kuwa fedha yako unayopaswa kuiweka huku ni ile fedha ambayo huihitaji kwa haraka. Kwa hiyo, kama ambavyo huwa tunawaambia watu watuwekee fedha benki, tunaweza kuwaambia pia watu watuwekee fedha kwenye akaunti zetu za  UTT na fedha zetu zikakaa huko.

    Lakini pia ni sehemu salama. Kama nilivyokudokeza hapo mwanzo UTTAMIS ni ni taasisi ya kiserikali iliyochini ya wizara ya fedha. Hivyo, usalama wa fedha yako ni mkubwa sana

    Ni sehemu ambayo inakuwezesha kuweka kiwago cha chini kuanzia elfu tano. Hii inategemea na aina ya mfuko ambao unakuwa umechagua, ila kwa aina nyingi ya mifuko ya UTT unaweza kuweka akiba kwa kiwango cha chini cha elfu tano tu

    Ni akaunti pekee ambayo ukitaka kuangalia salio haukatwi. Utt wana mfumo wao wa kukusaidia wewe kuangalia salio ambapo ukitaka kuangalia salio unatuma ujumbe kwenda uwekezaji@utt.co.tz bila gharama yoyote ile na unaambiwa taarifa zako za uwekezaji bila kukatwa gharama yoyote ile

    Kwa hiyo rafiki yangu, kama kuna malipo ambayo unapaswa kulipwa ila fedha yake huihitaji kwa haraka, basi waambie watu wakulipe kupitia UTT.

    @songambele

  • Sehemu sahihi ya kuweka akiba yako

    Jana kwa nyakati tofauti watu watatu walinipigia na kuniuliza swali ambalo kwangu lilikuwa ni kama swali moja tu. japo kila mtu alikuwa na namna yake ya kulitoa hilo swali, ila kilichonishangaza ni kuwa hilo swali lilikuwa  na vipande vitatu muhimu ambavyo vinafanana.

    • Kwanza kila mtu alitaka kuweka akiba sehemu nzuri
    • Sehemu ambayo haina makato
    • Sehemu ambapo ataweka kwa muda mrefu
    • Sehemu ambapo atapata fedha yake ikiwa imeongezeka zaidi ya alivyoiweka mwanzoni

    Sasa watu hawa watatu wamenifumbua macho na kunionesha kuwa pengine na wewe ungependa kuijua sehemu ya aina hii. Ndio maana siku ya leo nimeona, siyo vibaya, wacha nikuandalie makala ya kina inayoeleza hili suala ili na wewe uweze kuliewa.

    Kwanza unaweza kuwa unajiuliza, hivi kweli sehemu ya aina hiyo ipo kweli?

    Yaani, kwamba ipo sehemu ambapo unaweza unaweza ukaweka akiba yako kwa usalama, haina makato kwa kipindi chote ambacho umeweka akiba, na baadaye ukataka kuitoa, ukaitoa ikiwa imeongezeka zaidi ya vile ulivyokuwa umeiweka? Sehemu ya aina hii ipo kweli?

    Jibu ni ndio sehemu ya aina hii ipo ila haiwezi kuwa benki. Kwa sababu benki mara zote kwenye akaunti yako huwa kuna makato pale unapoweka fedha yako, benki huwa wanakukata kukutunzia fedha yako. Kwa hiyo sehemu ya aina hii haiwezi kuwa benki.

    Lakini kabla hujazilaani benki, naomba unielewe kwa kitu kimoja kwanza na cha msingi sana. Mimi nina akaunti ya NMB, kama sijakosea akaunti hii inaitwa akaunti ya mwanachuo au akaunti ya mwanafunzi. Kwenye akaunti hii huwa hawakati fedha pale unapoweka fedha  yako huku. Fedha yako huwa inaendelea kubaki kama ilivyo hata kama ikikaa kwa muda mrefu, labda makato ni pale tu ambapo huwa natoa fedha. Labda kama sera za uendeshaji wa akaunti hii zimebadilika. Ila kama hazijabadilika, basi hii inaweza kuwa akaunti nzuri kwako. ubora ni kwamba NMB wanaruhusu ufungue akaunti hii hata kama wewe siyo mwanafunzi.

    Lengo lao ni kusaidia watu kujijengea utaratibu wa kujiwekea akiba. Na mimi nawaunga mkono. Kwa nini? kwa sababu tafiti nyingi zimeonesha kuwa watu wenye akaunti ya benki, walau huwa wanajiwekea akiba ukilinganisha na watu ambao hawana akaunti ya benki. Sasa kama wewe hauna akaunti ya benki, nadhani unaweza usiwe na akiba yoyote ile mfukoni, au uongo?

    Enewei, tuachane na hilo, maana tangu mwanzo niliahidi kukwambia eneo unapwoeza kuweka akiba na baadaye ukaitoa ikiwa imeongezeka ila siyo benki. Halafu eti bado naendelea kuongelea masuala ya benki…

    Sasa baada ya kusema hayo, naomba tuone eneo ambapo

    • unaweza kuweka fedha yako,
    • Sehemu ambapo hakuna makato
    • Sehemu ambapo utaweka kwa muda mrefu
    • Sehemu ambapo utapata fedha yake ikiwa imeongezeka zaidi ya ulivyoiweka mwanzoni

    Hiki ni kitabu kizuri sana ambacho unapaswa kusoma. Gharama yake ni elfu tano tu.

    Walau sehemu hii siyo benki.

    Sehemu yenyewe ni kwenye akaunti za uwekezaji wa pamoja za UTT

    UTT ni taasisi ya kiserikali iliyochini ya wizara ya fedha ambayo inawakutanisha wawekezaji wote wenye mitaji midogo na mikubwa na kuwasaidia kuikusanya hiyo mitaji, kisha kuiwekeza sehemu salama.

    UTT imekuwa inafanya kazi hapa nchini karibia mwaka 20 sasa, ila cha kushangaza watanzania wengi hawana uelewa juu ya UTT na hata wengine hawajawahi kusikia habari za UTT.

    Ukiweka fedha yako UTT inakuwa sehemu salama, maana fedha yako zinakuwa chini ya taasisi ya kiserikali, lakini sambamba na hilo fedha yako inakuwa chini ya watalaamu ambao wataiwekeza sehemu salama ambazo wao wanajua. Kitu hiki kinafanya uwekezaji wako unakuwa salama na hata baadaye uwekezaji unakuja ukiwa na mrejesho mzuri.

    UTT AMIS kama inavyofahamika, ina mifuko sita ya uwekezaji ndani yake. Mifuko hii imeanzishwa kwa dhana na malengo tofauti kulingana na aina ya mfuko.

    Mfano mfuko wa umoja ambao pia ni mfuko mkongwe kwenye mifuko yote ya UTT, Ebu angalia picha hiyo  hapo chini

    Mfuko mwingine ni mfuko wa ukwasi ambao maelezo yake ya mafupi haya hapa

    Kwa kuwa hii makala lengo lake siyo kueleza mifuko yote ya utt kwa undani, nimedokeza hiyo mifuko mwili tu kwa kuwa ndiyo nataka kuiongelea zaidi kwenye makala ya leo.

    Kwa hiyo, kama una fedha zako na ungependa kuiwekekeza basi nashauri uweze kuiweka kwenye mfuko mmojawapo hapoo juu. Aidha mfuko wa umoja au mfuko wa ukwasi.

    Ukiweka fedha yako kwenye mfuko mmojawapo hapo juu, ni uhakika kuwa baada ya muda fedha yako itakuwa imeongezeka, maana mifuko hii imekuwa na mrejesho mzuri kila mwaka. Ambapo kwa wastani tangu kila mfuko umeanzishwa umekuwa na mrejesho wa asilimia 13.5. Hii maana yake kwamba ukiweka fedha yako huku, kwa kila kiasi ambacho utaweka huku, unapata ongezeko la silimia 13.5.

    Ikumbukwe kwamba huo ni wastani. Hii ndio kusema kwamba kuna miaka ambapo uwekezaji huo unaweza kuwa juu kama ulivyoona hapo juu. Na kuna miaka ambapo mrejesho huu unaweza kuwa chini.

    Kwa hiyo rafiki yangu, kwa kuwa leo nilitaka kukwambia sehemu nzuri ya kuwekeza fedha yako, basi naona lengo lengu kama nimeweza kulifikia.

    Kazi yako ya fuanya siku ya leo.

    Nenda kafungue akaunti ya Utt, ubora ni kuwa unaweza kufungua akaunti hata kwa simu yako.

    Bonyeza *150*82# uanze kufanya hivyo.

    Au unaweza kufungua akaunti kupitia aplikesheni yao iliyo kwenye playstore. Inaitwa UTT AMIS

    Kwa maelezo zaidi ya ndani kabisa, nashauri uweze kupata ebook yangu inayoitwa MAAJABU YA KUWEKEZA KWENYE HISA, HATIFUNGANI NA VIPANDE pamoja na ebook nyingine inayoitwa MAAJABU YA KUWEKA AKIBA. Hizi ebooks hizi zitakufaa sana rafiki yangu.

    Kila ebook gharama yake ni 5,000/- tu. Ona huyu mwenzako aliyekisoma hapa anavyosema

  • Uchambuzi wako pendwa umesomwa kwa sauti (Kitabu cha how to stop worring and start living)

    Wiki hii kweney blogu ya songambele tumefanya uchambuzi wa kitabu c ha How to stop worrying and start living. ni uchambuzi ambao umesomwa na watu wengi na wengi wameupenda. kutokana na hilo tumeona ni vyema ukasomwa kwa sauti, na hiki kitu ndicho kimenisukuma niulete hapa siku ya leo.

    huu hapa chini ndio uchambuzi wa kitabu cha How to stop Worrying and start living

  • Mtazamo mzuri kuhusu intaneti

  • Vitu Vitano Vitakavyokuzuia wewe kufanikisha malengo yako

    Siku siyo nyingi nilipokea ujumbe kutoka kwa mmoja wa watu wanaofuatilia kazi zangu mtandaoni. Kitu kikubwa sana ambacho aliweza kuniambia ni kuwa anapata changamoto hasa anapoweka malengo, anashangaa siku zinaenda ila hayo malengo yake hayatimiii.

    Sasa siku ya leo kwa namna ya kipekee ningependa kumjibu huyu rafiki pamoja na watu wengine wengi ambao wanawakuwa na shida kama hii hapa ili sote kwa pamoja tukitoka hapa twenda kufanyia kazi malengo yetu kwa manufaa na kwa namna ambayo ni bora zaidi.

    Kabla sijaingia ndani zaidi, ningependa sana kukwambia kuwa karibia kila mwanzoni mwa mwaka watu wengi huwa wanaweka malengo makubwa ambayo watayafanyia kazi ndani ya mwaka huo, ila cha kushangaza ni kuwa mpaka kufikia tarehe 19 januari watu wengi huwa wamesahau malengo yao, na wachahe ambao huwa wanaendekea kukumbuka malengo ndio huweza kuendelea nayo mbele kidogo huku wachache zaidi wakiwa ndio wanafikia malengo yao. Sasa swali kubwa sana ambalo mtu unaweza kujiuliza ni kwa nini?

    Jibu ni kwamba ule mkumbo na motisha ya tarehe moja vinakuwa vimeisha. Mwanzoni unapokweka malengo unakuwa na motisha kubwa, ila kadiri siku zinavyokuwa zinazidi kwenda, ile motisha inapotea, sasa watu huwa wanaishia hapo. ila sasa wewe haupaswi kuishia hapo, baadala yake unapaswa kuendelea kujisukuma zaidi ili uweze kufika kule unapotaka kufika. Na utaweza hili kama utajiwekea utaratibu wa kuwa unajikumbusha malengo yako karibia kila siku. Kila siku hakikisha kwamba unaandika chini malengo yako ambayo unayafanyia kazi, ili usiyasahau.

    Pili, usisubiri mpaka uwe kila kitu ili ufanyie kazi malengo yako. Kuna watu wanaweka malengo mazuri tu, ila kinachowafanya washindwe kuweza kufanyia kazi malengo yao na kuyatimiza ni kwa sababu wanasubiri mpaka wawe na kila kitu ili waje kufanyia kazi malengo yao. Naomba unisikilize kwa kitu, huhitaji kuwa na kila kitu ili uwezer kufanyia kazi malengo yako. Anza na kile ulichonacho, fanya kile kinachowezekana, mwisho wa siku utajikuta kuwa umeweza kufanya yasiyowezekana.

    Tatu, usisubiri mpaka tarehe 31 disemba ili ufanyie kazi malengo yako. Wengine wanaweka malengo makubwa ila wanasubiri mwisho wa mwaka ili malengo yao hayo yaweze kutimia. Unachopaswa kufahamu ni kuwa malengo makubwa huwa hayatimii mwishoni mwa mwaka. Hivyo, badala ya wewe kusubiri mpaka mwisho wa mwaka ili uweze kutimiza malengo yako, anza kuyafanyia kazi siku ya leo hata kama ni kwa udogo.

    Nne,  watu waliokuzunguka. Moja kati ya usemi wenye ukweli mkubwa sana ndani yake ni usemi kuwa miaka mitano ijayo utakuwa jisnsi ulivyo isipokuwa kwa vitu viwili tu, watu waliokuzunguka na vitabu unavyosoma. Rafiki yangu, kama kuna kitu unahitaji sana ili kuweza kufikia malengo yako basi ni watu, hakikisha kwamba unazungukwa na watu ambao ni chanya na wale ambao wanaendana na malengo yako.

    Watu ambao ni hasi watakufanya ukwame na ushindwe kuweza kufkia malengo yako.

    Tano, kuweka malengo madogo sana. malengo madogo yanakunyima hamasa na yanakufanya ushidnwe kusonga mbele ila malengo makubwa yanakupa msukumo wa kufanya makubwa na kujisukuma zaidi. hivyo basi rafiki yangu nakushauri sana uweke malengo makubwa na kila mara uhakikishe  kwamba unajisikuma kwenye kuyafanyia kazi na kuyatimiza. Kamwe usirudi nyuma kwenye kufanyia kazi malengo yako.

    Kil la kheri

    Umakuwa nami rafiki yako wa ukweli

    Godius Rweyongeza

    0755848391

    Morogoro-Tz

  • Uchambuzi Wa Kitabu: How To Stop Worrying and Start Living

    NB: kusikiliza makala hii kwa njia ya sauti. Bonyeza hapa

    Kitabu: How To Stop Worrying and Start Living

    Mwandishi: Dale Carnegie

    Mchambuzi: Hillary Mrosso

    Simu: +255 683 862 481

    Utangulizi

    Jina la kitabu hiki lenye maana ya Namna ya kuachana na hofu na kuanza kuishi. Ni kitabu bora sana kinachoelezea namna ya kukabiliana na hofu kwenye maisha yetu ya kila siku. Hofu imewalaza wengi katika vitanda vya hosipitali, hofu imewanyang’anya wengi afya, furaha, amani, utajiri, na fedha nk. Mwandishi wa kitabu hiki ametumia muda mwigi sana kufanya utafiti wa kina kwenye maisha ya watu wengi waliopitia nyakati ngumu zilizotawaliwa na hofu na kupata maoni yao na ndio kwa kiasi kikubwa yametumika katika uandishi wa kitabu hiki. Hiki ni moja ya vitabu bora sana kwa binadamu yoyote, hupaswi kabisa kukosa kusoma kitabu hiki, ni kama dawa na kinga endapo utayatumia yaliyoandikwa humu kukutoa kwenye aina zote za hofu ulizo nazo. Karibu kwenye uchambuzi huu muhimu.

    1. Kitabu hiki kinawafaa zaidi wale ambao wapo tayari kutekeleza yaliyoandikwa katika kitabu hiki, hii ndio faida na lengo la uandishi wa kitabu hiki, sio kwa ajili ya kujifurahisha na kufurahia namna kilivyoandikwa, ni kitabu kinachodai zaidi utekelezaji.

    2. Mwandishi wa kitabu hiki anasema, soma kurasa 40 za mwanzo za kitabu hiki, na endapo hutapata chochote cha kukusaidia kukabiliana na hofu ulizo nazo, basi, unachotakiwa kufanya ni kukitupa au kukichoma kitabu hiki.

    3. Maisha yetu ya baadaye yatakuwa bora kwa kufanya yale yaliyopo kwenye siku yetu ya leo, usifanye mambo ya kesho leo wala usifanye mambo ya jana kesho, wekeza kwenye kufanya yaliyopo kwenye siku yako.

    4. Mwandishi Dale Carnegie anasema tukumbuke moja ya maombi ambayo Yesu Kristo aliwafundisha wanafunzi wake, aliwaambia waombe mkate wa siku, na sio mkate wa kesho au jana, au mwezi ujao.

    5. Mkate wa siku hiyo ndio wa muhimu zaidi, maana yake kila siku ina mambo yake, huenda kesho usihitaji mkate ukahitaji kitu kingine, Mungu anakupa kile unachokihitaji sasa, yaani leo na sio unachokihitaji kesho au jana.

    6. Katika moja ya mafunzo muhimu Yesu Kristo aliyowafundisha wanafunzi wake ni kuacha kujisumbua au kuhangaika kwa ajili ya mambo ya kesho, aliwaambia iacheni kesho ijisumbukie yenyewe.

    7. Usighairishe mambo ya leo kwa kuhofia utaishije kesho, kesho ina mambo mengi na kuna mengi hutaweza kuyathibiti hivyo wekeza nguvu zako kufanya yale yaliyomo mbele yako, mbele ya siku yako, hii ndio njia nzuri ya kuondoa hofu kwenye maisha yako.

    8. Kuwa na mawazo mazuri kuhusu siku yako, itakufanya uipangilie na kufanya yote kwa ufanisi, mawazo mabaya yanaleta hofu na msongo wa mawazo ambao hupelekea kuairisha mambo muhimu ka kuhofia mambo usiyoyajua na usiyo na ukakika nayo.

    9. Ili maisha yetu yawe bora, tunahitaji siku moja bora, ili tuweze kufanya yote yaliyo bora kwenye siku hiyo. Siku zote jifunze jambo hilo, unahitaji siku moja tu.

    10. Andika hii sentensi kwenye karatasi na uibandike ofisini kwako au nyumbani kuwa, unahitaji siku moja tu kufanya makubwa. Siku moja, ukiipata siku hii moja fanya makubwa na ya muhimu kwenye siku hiyo.

    11. Fanya jambo moja kwa wakati, hatua moja kwa wakati hii dhana itakusaidia sana kuwa mwenye ufanisi unapofanya mambo muhimu kwenye siku yako.

    12. Epuka kuwa na mrundikano wa mawazo, au majukumu mengi ndani ya siku yako, maana hayo yatakufanya ushindwe kuianza siku yako kwa ushindi na pia yanaweza kukukatisha tamaa na utaishia kuchanganyikiwa na kukosa cha kufanya hii itapelekea uanze kuwa na hofu.

    13. Ukweli ni kwamba nusu ya vitanda vya hosipitalini vimetengwa kwa ajili ya wagonjwa hofu, ambao neva za miili yao zimeharibika kwa hofu waliyoitengeneza kwenye maisha yao kwa kuhofia mambo ya jana na kuwa na mashaka na kesho wasiyoijua.

    14. Panga kuishi maisha yako kikamilifu ndani ya siku moja, achana na usiyoyajua kuhusu kesho, achana na kujibebesha mizigo ya mambo yaliyokwisha kupita.

    15. Jifanyie wepesi kwenye maisha yako, amua kuishi maisha marefu kwa kuondoa hofu kwenye maisha yako, hofu inafupisha sana siku zako za kuishi, inakufanya uonekane mnyonge muda wote hofu ni mbaya jamani.

    16. Hadi unapofikia wakati wa kulala usibebe mzingo wowote wa madeni, hofu, chuki, uchungu, hasira kwnda nao kitandani, achilia, samehe, na ingia kitandani ukiwa mwepesi na ukilala usingizi wako utakuwa kama wa mtoto mchanga.

    17. Jikumbushe kila siku unapoianza siku yako, jiambie maneno haya, “wacha niishi siku hii moja tu vizuri”, jiambie hivyo kila siku. Kwa kufanya hivyo utawekeza nguvu zako zote kwenye kuifanya siku yako kuwa bora sana, na hatimaye maisha yako ya sasa na ya baadaye yatakuwa bora.

    18. Moja ya asili ya binadamu ni kughairisha kuishi, na kuanza kufikiria vitu ambavyo hata havipo kabisa, wengi wanaghairisha furaha, amani, upendo au mambo muhimu yaliyopo mbele yao na kuanza kufikiria vitu ambavyo hata havipo.

    19. Maisha ni yako, shughulika na yako, acha kutoroka maisha yako, maisha yako ni jukumu lako, yafanye maisha yako kuwa yenye furaha, amani na upendo wakati wote, uwezo huo unao.

    20. Mambo ya leo ndio muhimu, usiache kuishi sasa na kuanza kutatua matatizo ya kesho ambayo hujui itakujaje.

    21. Ifurahie siku yako, na panga kufanya makubwa uwezavyo ndani ya siku hiyo, Carpe diem. “Enjoy the day.” 

    22. Fanya kama mtunga zaburi aliyosema, Hii ndio siku aliyoifanya Bwana, tutaifurahia na kuishangilia. Hakusema hizi ndizo siku, au hii ndio kesho au jana aliyoifanya Bwana, alisema hii ndio SIKU aliyoifanya Bwana.

    23. Unapoamua kukabiliana na hofu zilizoko kwenye maisha yako, jiambie bila kuogopa, na agalia hali zote unazoweza kukabiliana na hofu hizo bila kujali. Unaweza kujiambia endapo nitafanya jambo hili ninalolihofia nitaenda jela? Au nitakufa?

    24. Pambanua kwa undani bila mashaka yoyote endapo utafanya unachohofia, ni kitu gani kibaya sana kitatokea kwenye maisha yako, ni kifo, au utaenda jela au ni nini kitatokea, ukiona hakuna kibaya basi acha kuogopa na ufanye jambo hilo.

    25. Unapodhamiria kufanya jambo muhimu kwenye maisha yako usiache hofu zikakuzuia kufanya, jifanyie tathimini fupi ya faida na hasara kisha chukua hatua sahihi.

    26. Mara kwa mara jiulize swali, kuna faida gani kwenye haya ninayoyaogopa? Hii hofu inanisaidia nini? Fikiria na chukua hatua mara moja uachane na hofu zinazokusumbua.

    27. Hofu inadumaza na kutufanya tushindwe kuchukua hatua kwenye maisha yetu, hofu zinaturudisha sana nyuma, amua kuondoka kwenye hofu uishi maisha yenye furaha na afya tele.

    28. Hofu nyingi tulizonazo zitapungua endapo tutajua uhalisia wa jambo na kukubaliana na matokeo yake. Wengi wamelimbikiza hofu zinazowaua taratibu kwa kushindwa kukubaliana na uhalisia wa mambo.

    29. Usipokuwa tayari kukubaliana na uhalisia ulivyo, siku zote utaishi kwenye hofu, mashaka, hasira, chuki na magojwa yatakuandama.

    30. Wachina wana msemo wao wa ajabu sana, wanasema amani ya moyo unaipata pale unapokubaliana na yaliyokwisha kutokea. Kama mambo yameshatokea huna unachoweza kufanya tena zaidi ya kukubaliana na matokeo yake.

    31. Wengi wameingia kwenye hofu kwasababu wameshindwa kukubali matokeo, na wanatumia muda mwingi, nguvu, na hisia zao kufikiria mambo yaliyopita. Hii ikiendelea ilaleta hofu, uchungu na hasira.

    32. Kubaliana na mabaya yaliyokwishatokea au ambayo hayajatokea, hii inatakufanya uishi kwa amani, tegemea mabaya yanaweza kutokea kwako au kwa mtu mwingine, hivyo usiogope maana kwa kuogopa au kuwa na hofu hutabadili chochote.

    33. Namna nzuri ya kukabiliana na kupanda au kushuka kwa sukari mwilini mwako ni kuwa tayari kuyapokea yote yatakayokuja kwenye maisha yako, haijalishi ni mazuri au ni mabaya, yapokee kama yalivyo, kwa kufanya hivyo utalinda afya yako na mwili wako.

    34. Kama wewe ni mfanyabiashara na hujui kupambana na hofu, unaweza kufa mapema. Kwenye biashara kuna mengi yasiyotarajiwa, hata ujiandae vipi, lazima kuna mengine yatakuja tu kukushangaza, hivyo kama wewe ni mtu wa hofu unaweza usifanikiwe na ukafa mapema.

    35. Mwandishi Dale anasema, asilimia 70 ya wagonjwa wanaoenda kumuona daktari wanaweza kupona maradhi na magonjwa yao endapo watakaa mbali na hofu na mashaka.

    36. Hofu na mashaka zinafanya mfumo wa neva za miili yetu kushindwa kufanya kazi vizuri, hivyo kupelekea madhara kwenye mfumo wa umeng’enyaji wa chakula na kusababisha neva za tumbo kupeleka taarifa za uzalishaji mwingi wa acidi ambazo huleta madhara kama vidonda ya tumbo.

    37. Mwandishi anasema, taarifa za kitabibu zinaonyesha wengi wenye vidonda vya tumbo ni kwasababu ya hofu na mashaka waliyo nayo kwenye maisha yao. Hivyo wengi wanaweza kupona au kutoingia kwenye madhara ya kupata magonjwa hayo kwa kuziepuka hofu.

    38. Hofu pia zinazalisha msongo wa mawazo ambao pia una madhara kwenye mwili wa binadamu kama vile kusababisha vidonda vya tumbo.

    39. Daktari Joseph Montague anasema, hatupati vidonda vya tumbo kwa vyakula tunavyokula, tunapata vidonda vya tumbo kwa vile vinavyotula. Anamaanisha sio aina ya vyakula ndio huleta vidonda vya tumbo, bali vidonda vya tumbo vinatokana na vile vinavyotula.

    40. Utafiti wa gazeti la Life magazine nchini Marekani unaonyesha kuwa, hofu, mashaka, uchoyo uliopitiliza, chuki na kushindwa kukubaliana na uhalisia wa mambo vimekuwa ndio chanzo kikuu cha vidonda vya tumbo, na vidonda vya tumbo vinaripotiwa kuwa moja ya janga kubwa linaliua watu watu duniani.

    41. Madakari bingwa kutoka katika kitengo cha hosipitali ya Mayo nchini Marekani wanasema nusu ya vitanda vya hosipitali vimejaa wagonjwa ambao wana matatizo ya neva. Matatizo ya neva huathiri utendaji kazi wa sehemu kubwa ya mwili, na kwa kiasi kikubwa husababishwa na hofu.

    42. Matatizo hayo ya neva sio kwamba yanasababishwa na neva kuharibika kutokana na michubuko ya nje, bali ni kutokana na hisia za kuchanganyikiwa, hofu, huzuni, hasira, kushindwa na kukata tamaa.

    43. Mwanafalsafa maarufu sana duniani Plato aliwahi kusema, madaktari wanakosea sana pale wanapojaribu kutibu mwili bila kutibu nafsi, ambayo imebeba hisia zote za mtu kama vile hisia za chuki, furaha, hasira, hofu nk. Huweze kutengenisha kutibu mwili pekee bila kutibu na eneo lake muhimu la hisiaa.

    44. Ni ukweli sayani ya utabibu imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutibu na kuondoa kabisa magonjwa mabaya kwa binadamu kama vile, surua, pepopunda, kipindupindu, ugonjwa wa manjano, malaria nk. Ambayo yalipeleka watu wengi kaburini.

    45. Hata hivyo, sayansi ya udakatri bado inakabiliwa na changamoto sana katika kutatua changamoto za magojwa ya kiakili, hisia, hofu, chuki, na msongo wa mawazo ambayo kwa kiasi kikubwa yanawasumbua sana watu wengi.

    46. Taarifa za kitabibu kutoka nchini Marekeni zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya watu 20 anatatizo la kiakili, ambalo limechangiwa na msongo wa mawazo na hofu.

    47. Tafiti nyingine kuhusu afya ya akili zinaonyesha mtu mmoja kati ya sita walioitwa kwa ajili ya kushiriki kwenye vita ya pili ya dunia alikataliwa kutokana na matatizo ya kiakili. Matatizo haya ya kiakili kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na hisia za hofu na mashaka

    48. Kama unakabiliwa na nyakati ngumu kwenye maisha yako, ushauri ni kwamba usichukue nyakati ngumu ukazipeleka kwenye mfumo wako wa upumuaji au hisia, ukifanya hivyo utafupisha maisha yako.

    49. Utafiti wa Dkt. Wiliamu McGonigle kutoka taasisi ya meno nchini Marekani unaonyesha kuwa hofu na mashaka yanasababisha meno kuoza, hii ni kutokana na hisia mbaya za hofu na mashaka zina haribu uwiano wa mfumo wa madini ya Calciam mwilini na hivyo kusababisha meno kuoza.

    50. Hofu inaharibu hata mwonekano wako wa nje, hofu inaweza kukujengea muonekano usiovutia kabisa, ukaonekana wa ajabu, ukaonekana mzee kumbe ni kijana.

    51. Hakuna kitu kinaharibu mwonekano wako wa nje haraka kama hofu, mwonekano wako wa nje una maana sana kwenye maisha yako, hivyo usikubali uharibiwe kwa hofu.

    52. Hofu inakufanya ujioni mkosaji, hufai, hustahili na inakufanya ujione unaonewa, hofu inakujengea picha na taswira ambazo hazina uhalisia wowote.

    53. Ukiruhusu tu hofu kwenye maisha yako, ujue umeruhusu pia majirani zake wa karibu ambao ni vidonda vya tumbo na matatizo ya moyo kama shinikizo la damu nk.

    54. Hofu inaharibu nywele zako, zinaweza kupoteza rangi yake ya asili, hofu inaweza kufanya hata nywele zako za kichwani kupotea au kushindwa kuota.

    55. Hofu inaweza kukuletea magonjwa ya ngozi, inaweza kubadili hata rangi ya ngozi ya mwili wako, inafanya ngozi kusinyaa na kusababisha vipele majipu na muwasho.

    56. Unapokuwa na hofu huwezi kuzalisha chochote, zaidi sana utajiletea madhara makubwa yatakayokugharimu uhai, kama vile magonjwa ya moyo na vidonda vya tumbo.

    57. Hofu ni kama dripu za maji ya matone, ukiiruhusu inakutafuna hadi unaishia kujiua au kukufanya kuwa kichaa. Usiruhusu hofu kwenye maisha yako.

    58. Changamka na uwe mtu wa furaha, hii itaongeza kinga za mwili wako na kuimarisha afya ya mifupa yako, kumbuka mifupa yako inaweza kuharibika kwasababu ya hofu, hivyo ukaishia kupata kansa.

    59. Mwandishi Dale Carnegie anasema nusu ya majanga ya hofu yanayowapata watu ni kwasababu wanafanya maamuzi bila kuwa na taarifa za kutosha kuhusu jambo fulani.

    60. Tafuta taarifa za kweli kuhusu kinachokutia hofu, kwa kufanya hivyo utakuwa umetatua sehemu kubwa ya tatizo linalokusibu.

    61. Kuwa na utaratibu wako wa kuandika kila changamoto unayoipitia, pia ainisha njia utakazotumia kukabiliana na hiyo changamoto, fikiria unachoweza kufanya kuitatua changamoto hiyo na kisha chukua hatua mara moja.

    62. Jinsi unavyojikita kwenye kufanya majukumu yako kila siku ndivyo unavyoachana na hofu. Hofu inatabia ya kumtawala na kumtesa mtu ambaye hana cha kufanya kutwa nzima amekaa tu au amelala tu bila kufanya jambo lolote.

    63. Mfano, kama unasumbuliwa na hofu sana, nenda shambani, tengeneza bustani, nenda kwenye mazoezi, au nenda ukacheze mziki hii itakufanya uache kuwaza kuhusu hofu, (occupational therapy).

    64. Tafuta wastani wa jambo unaloliogopa kwamba litatokea kwenye maisha yako, mfano kama unaogopa kusafiri kwasababu kuna ajali, basi tafuta wastani wa magari yote yanayosafiri kisha angalia yanayopata ajali ni mangapi angalia wastani, ukiona ni mdogo, usiogope kuchukua hatua.

    65. Changaoto hazitufanyi kuwa na furaha au kutokuwa na furaha, ni jinsi tunavyozichukulia ndio huamua hisia zetu kwenye hizo changamoto.

    66. Bwana Yesu aliwahi kusema, Ufalme wa Mungu upo ndani yetu, hivyo ufalme wa shetani unaweza kuwa ndani yetu pia. Maana yake kama wema unakaa ndani yetu hata ubaya unaweza kukaa ndani yetu, hivyo wema na ubaya kukaa ndani yetu ni kutegemeana na maamuzi tunayoamua.

    67. Binadamu ni viumbe wa ajabu sana, wanaweza kubeba majanga, kushindwa na hata mambo machungu sana, hivyo pia anaweza kubeba ushindi furaha, amani na mafanikio. Tumeumbwa na uwezo mkubwa sana wa kuweza kupitia kila hali kwenye maisha haya, tuna uwezo kuliko tunavyodhani.

    68. Henry Ford aliwahi kusema kauli moja nzuri sana kuhusu mambo yanayotushinda maishani, alisema kama huwezi kukabiliana na jambo fulani ana achana nalo. Maana yake kama kuna jambo huwezi kulibeba kwenye maisha yako liache lijibebe lenyewe.

    69. Kuna mambo yapo kabisa nje ya uwezo wetu kama binadamu na hatuwezi kuyaathiri kwa namna yoyote ile, tutayaacha tu yatokee kama yaliyo. Ukitambua hilo hutakuwa na hofu na mashaka kwenye baadhi ya mambo, utakuwa na amani na utulivu.

    70. Mwanafalsafa mashughuri wa Roma, Epictatus aliwahi kusema, njia moja ya kuwa na furaha ni kuacha kuhofu na kuogopa vitu ambavyo vipo nje ya uwezo, au nguvu zetu kuvikabili.

    71. Kuna nguvu kubwa tunaipata pale tunakubali kuwa kwenye maisha kuna vitu vipo nje ya uwezo wetu kuvikabili, kuna vitu hatuna nguvu ya kuvifanyia chochote au kuviamulia, vipo nje ya uwezo wetu.

    72. Tunatakiwa kujua wakati wa kuwa chini na kuinama kuruhusu mengine yapite, hatuna nguvu za kukabiliana na kila kinachokuja mbele yetu, tukiwa wakaidi tunavujika, tujifunze kwa minazi na miti mingine.

    73. Mfano, miti na misitu minene iliyositawi inajua kanuni hii ya maisha, inajua lazima upepo uje na haiwezi kushindana na upepo maana vinaweza kuvunjika, hivyo hukunja matawi yake, huinama na kusujudu ili upepo upite zake.

    74. Tukubali kuomba Mungu atujalie neema ya kukubali vitu ambavyo hatuwezi kuvibadili, na kibali cha kubalidi yale tunayoweza kuyabadili. Na hekima ya kutambua tofauti.

    75. Tusiwe wakaidi, tunatakiwa kujifunza kushirikiana na yale yasiyoepukika kwenye maisha yetu, hii ndio siri ya furaha na kuishi maisha marefu.

    76. Usilazimishe mamba ambayo yalishatokea, usijaribu kuzoa maji yaliyokwisha mwagika. Imetokea imetokea basi, tafuta namna nyingine ya kuishi.

    77. Wacha yaliyopita yajizike yenyewe, huna cha kufanya zaidi, na endapo utayafuatilia basi ujue utapata ulichokitafuta ambacho ni hofu, sura mbaya na vidonda vya tumbo.

    78. Kumbuka, unapowachukia maadui zako maana yake unawapa nguvu juu ya amani yako, afya yako, usingizi wako, moyo wako nk.

    79. Waliokuudhi wanaweza waziwaze kabisa kuhusu wewe, wanaweza kuwa wapo sehemu wanafurahia maisha na kucheza muziki, wewe unaendelea kuumia na kutoa lawama kwao, kumbuka unajiumiza mwenyewe.

    80. Na aliyekuudhi atafurahia sana endapo atajua unaumia, unamuwaza au unamhofia kila mara. Jifunze kusamehe kwa ajili ya afya yako, nafsi yako, moyo wako, amani yako na furaha yako.

    81. Ndio maana unaona Yesu katika mafundisho yake alisema, “wapendeni adui zenu” akaendelea kusema semehe mara saba sabini, Yesu alijua njia nzuri ya kuwa na afya, furaha na amani muda wote ni kuishi kwa upendo na kusamehe.

    82. Kama utaishi na chuki, utashindwa kusamehe, basi jua hautakiwa mbali na shinikizo la damu, mashambulizi ya moyo, vidonda vya tumbo na magonjwa mengine. Jipende, samehe, achilia ishi kwa amani ukiwa na afya tele.

    83. Unajua hofu, uchungu, chuki vinatufanya tushindwe hata kufurahia chakula tunachokula, na hapo ndipo afya zetu zinapodorora.

    84. Hofu itakufanya uchoke hata kabla ya kuchoka, itakuondolea kila kitu kizuri kwenye maisha yako. Mwandishi wa kitabu hiki anasema hata kama tumeshindwa kuwapenda adui zetu, basi tujiepende wenyewe.

    85. Dale Carnegie anashauri, kabla hujalala usiku, samehe kila kitu na kila mtu, fanya hivyo maisha yako yote. Ili ulinde afya yako, amani na furaha yako.

    86. Maneno ya watu wanaokusema hayatakuvunja mifupa, jifunze kuyapuuza uendelee na maisha yako, kuna mambo mengi ya msingi unatakiwa kuyafanya kwenye maisha yako, usiwekeze kwenye maoni ya watu kuhusu wewe.

    87. Usijaribu kuwa sawa na adui yako, maana yake usiwe mtu wa visasi au ubaya, yashinde mabaya kwa mema. Usiache mabaya yakutawale ukaishia kuamua vibaya na kutengeneza hofu.

    88. Haitoshi kujisifia kuwa wewe ni mzalendo wa kweli, mzalendo wa kweli hana uchungu, visasi, chuki na wala hasira kwa mtu yeyote yule.

    89. Usiweke mategemeo kwamba kwasababu ulimsaidia mtu sana kwenye maisha yake basi atakuja kukushukuru au kukusaidia na wewe, ukiwa na mategemeo hayo unaweza kuwa mtu wa malalamiko na asiye na furaha.

    90. Ondoa mategemeo ya kusaidiwa, kusifiwa, au kupendwa ishi vizuri maisha yako bila kutegemea hayo mambo. Endapo utakuja kusaidiwa, kupendwa au kushukuriwa itakuwa ni jambo la ziada kwako, isiwe uhitaji maana ukitegemea ukikosa utaanza kutengeneza malalamiko na uchungu.

    91. Usitegemee watu watakuwa wema kwako, au watakutendea mema, wape watu nafasi kubwa ya kukosea na kukukosea hii itakufanya uwe na uwezo wa kukabiliana na kila hali kwenye maisha yako.

    92. Mwanafalsafa mahiri aliyewahi kuitawala Roma kwa mafanikio makubwa, Marcus Aurelius, aliwahi kusema, katika moja ya maandishi yake kuwa kila siku anapoamka asubuhi kwenda kazini anajiandaa kwenda kukutana na watu wachoyo, wabinafsi, wasio na shukrani, wakaidi, wenye kiburi na wakorofi. Alikuwa hashangazwi kabisa kukutana na watu hao maana bila wao hajui dunia ingekuwaje.

    93. Ndugu msomaji wa uchambuzi wa kitabu hiki, kumbuka siku zote watu wanaweza kukusahau hata kama uliokoa maisha yao kutoka kwenye kifo, wengine wanaweza wasikushukuru hata kama umewafanyia jambo zuri kiasi gani, ni asili ya binadamu, hivyo yakitokea hayo kwenye maisha yako yasikuumize kichwa kabisa.

    94. Mfano mzuri upo kwenye Biblia, Yesu aliponya vipofu 10, lakini ni mmoja tu ndio alirudi kushukuru. Jambo hili lilimfanya Yesu kuuliza nimeponya watu 10, amekuja mmoja kushukuru wengine 9 wameenda wapi? Ni asili ya binadamu kutoshukuru, ilitokea kwa Yesu, inaweza kutokea kwako pia, usishangae.

    95. Furaha na amani yako inatakiwa kutokana na wewe kuwafanyia wengine wema, na isiwe kinyume chake. Aristoto, moja ya wanafalsafa maarufu sana alinukuliwa akisema, mtu bora zaidi ni yule ambaye furaha yake ipo katika kutoa na kuwasaidia wengine na sio katika kupokea au kusaidiwa na wengine.

    96. Kama tunatafuta furaha kwenye maisha yetu tunatakiwa kujua, furha ya kweli ipo katika utoaji na sio upokeaje, hivyo tuache kabisa kutegemea shukrani au mema kutoka kwa wengine.

    97. Kuna wazazi wanapata shida sana, presha zao ziko juu, vichwa vinawauma kwa sababu walizaa watoto na kuwafanyia makubwa kwa mategemeo kuwa watoto hao watakuja kurudisha fadhila kwa wazazi wao au walezi wao. Kumbuka mfano wa Yesu Inaweza isiwe hivyo mara zote.

    98. Hapa simaanishi hatutakiwi kuwa watu wa shukrani, la hasha! Tunatakiwa kuwa wakarimu na kuwaonyesha wazazi wetu upendo, shukrani na fadhila. Lakini vitu hivyo visipotokea isiwe ndio wapandwe na hasira na kuishia kuwa na chuki.

    99. Kama tunataka kuwa na watoto wenye shukrani, wakarimu, tunatakiwa kuwa hivyo sisi wenyewe kama wazazi.

    100. Njia nyingine ya kuiua tabia ya hofu na mashaka ni kuhesabu baraka zako, angalia uliyonayo na sio yale ambayo huna, angalia faida na sio hasara, angalia suluhu na sio matatizo.

    101. Hofu inaweza kufa kabisa kwenye maisha yako endapo utajenga uhusiano mzuri na Mungu, hapa inabidi uwe mtu wa imani, fanya sala, maombi na shukrani kwa Mungu wako.

    102. Mahatma Ghandh, moja ya mtu mashughuri sana na baba wa taifa la India, alipigana vita vyote vya rohoni na mwilini na alishinda vita vyote bila kumwaga damu, moja ya kitu ambacho hakikukosekana kwenye maisha yake ni ibada na maombi.

    103. Ghandh anakiri katika maisha yake ya kuleta mapinduzi kwa taifa la India, asingeweza kustahimili vitisho, hofu, mashaka mashutumu mengi yaliyokuja kwake kama asingekuwa mtu wa sala na maombi. Maombi na imani yake kwa Mungu yalimfanya apate nguvu za kustahimili kila upinzani kwenye maisha yake.

    104. Hofu haiwezi kukaa kwa mtu mwenye imani, mtu mwenye uhusiano imara na Mungu, hofu na mashaka haziwezi kukaa pamoja na imani kwa Mungu. Imeandikwa kuwa, hatukupewa roho ya hofu na mashaka, bali roho ya nguvu.

    105. Mwandishi wa kitabu hiki anashauri tusome Zaburi ya 23. Hii itasaidia sana namna ya kukuza imani yetu kwa Mungu na itatuondolea hofu na mashaka.

    106. Usije ukakosa usingizi kwa sababu ya maneno ya watu juu yako. fanya mambo yako kwa uwezo wako wote, kwa ubora wa viwango vya juu sana, kisha waachie waendelee na kelele zao.

    107. Kama unajihisi uchovu na kuchoka, jipe muda wa kupumzika, relax na tafakari mazuri na namna ya kuboresha kazi zako.

    108. Usiogope kufanyia kazi malengo yako, hata kama itakugharimu kukosa usingizi, mwandishi anasema hakuna aliyewahi kufa kwa kukosa usingizi.

    109. Tafuta vitabu bora vya kusoma ili uboreshe imani yako, hata mahusiano yako na watu wako wa karibu, hii itaongeza kujiamini na kujiona mwenye mchango kwenye jamii.

    110. Hamasika kufanya mambo yako, tengeneza mazingira yote yawe mazuri na yatakayokufanya uhamasike kufanyia kazi ndoto zako, mfano kama ni ofisi hakikisha ipo katika mpangilio mzuri, taa, meza, kalamu nk.

    111. Fanya mambo yako kwa vipaumbele, zinagatia vipaumbele kwenye ufanyaji wa majukumu yako, la muhimu ndio lianze na lifuate jingine.

    112. Simamia masuala yako ya kifedha vizuri, pangilia bajeti yako na fanya manunuzi kulingana na bajeti yako, usitamani maisha ya mtu mwingine, boresha yako na yafanye unavyotamani yawe.

    113. Chukua tahadhari zote muhimu, kama vile kulinda afya yako, kazi zako, biashara yako na utajiri wako, unaweza kukata bima.

    114. Kuwa mwanamichezo, pasha misuli yako, furahi, cheka sana, usijichukulie serious saaana. Jicheke kwa uliyoyahofia ambayo hayakuwa halisi kama ulivyodhani.

    115. Kumbuka leo ni ile kesho uliyokuwa unaihofia jana, amua kuondoka kwenye hofu maana umeona hakuna uhalisia kwenye mambo mengi unayohofia.

    MWISHO:

    Kitabu hiki kina mbinu nyingi na mafunzo mengi yenye mifano halisi namna watu walivyotoka kwenye maisha ya hofu na kuanza kuishi maisha yao kwa furaha na kwa ujasiri. Napenda kila mtu akisome kitabu hiki kitatibu magonjwa mengi sana yanayoisumbua jamii yetu. haya ni machache kati ya mengi yaliyoandikwa kwenye kitabu hiki. Tafuta nakala yako ujisomee, utajishukuru siku zote.

    ©Hillary Mrosso 22.08.2022

  • Kiashiria Kuwa Unatakiwa Kuchapa Kazi Kubwa Zaidi Ya Unavyofanya Sasa

    Ukiona bado unatumia nguvu kubwa kujieleza kwa watu ili waweze kukufahamu wewe ni nani, basi fahamu kuwa bado unahitaji kuweka juhudi kubwa na kazi kubwa zaidi, ili kupata unachotaka.

    Chapa kazi kiasi kwamba ifikie hatua,  ukisema kwamba mimi ndiye John Makene, basi kila mtu ajue wazi kuwa ni wewe, siyo unaanza kujieleza sana ili ufahamike.

    SIku njema.

    rafiki yangu, twende zetu youtube leo ukatazame nilichokuandalia

  • Kitu Kimoja Muhimu Unachohitaji kufahamu Kuhusu Uwekezaji

    Rafiki yangu leo nataka nikwambie kitu kimoja na muhimu sana unachohitaji kufahamu kuhusu uwekezaji. Na kitu hiki siyo kingine bali ni kuwa usiwekeza kwenye kitu ambacho wewe mwenyewwe huelewi.

    Kamwe usikubali kuitoa fedha yako ambayo umeihangaikia kwa jasho kubwa kuiwekeza kwenye kitu ambacho wewe mwenywewe huelewi.

    Hakikisha kabla ya kuwekeza unajirisha kwa undani kuwa kitu unachoenda kuwekeza unakielewa vizuri na kwa undani.

    Kama kitu hukielewi, basi uweke fedha yako hapo.

  • Kitu Muhimu Kuhusu Fursa

    Habari ya upande wa huko rafiki yangu, bila shaka unaendelea vizuri kabisa.

    Mimi nakusalimia hapa kutoka mjini Morogoro.Leo nimeukumbuka ujumbe mmoja ambao niliwahi kuusoma siku za nyuma.

    Ujumbe huu sijauandika mimi, ila una funzo kubwa sana kuhusiana na fursa. Na ningependa na wewe uusome.Sina shaka utaniambia kitu kikubwa ulichojifunza baada ya kuwa umeusoma. Ujumbe mwenyewe huu hapa chini.

    Ukipata nafasi ya kufika kule Mbozi, Mbeya ukakutana na habari za watu wanaotajirika kutokana na kilimo cha kahawa, kwa kweli unaweza kuwehuka, na kujiona kama mtu uliyechelewa kweli kweli.

    Wakati unarudi, kama ukishuka Mafinga, Njombe na kufuatilia stori na kutazama mamilionea walioupata umilionea kutokana na biashara ya miti na mbao, unaweza kudhani kwamba hapa duniani fursa inayowatoa watu kiuharaka ni mbao pekee!

    Pitia maeneo ya Ruaha Mbuyuni, Iringa kutana na wakulima wa nyanya na vitunguu wakikuonesha coaster walizonunua kwa kilimo cha msimu mmoja pekee. Aisee kama una akiba utanunua shamba muda huo huo na kuachana na ajira kama ulikuwa mwajiriwa.

    Ukitoka pale ukaenda mpaka Mang’ula na Ifakara Morogoro, ukakutana na habari za watu wanavyopiga hela kwenye mpunga, kichwa chako kinaweza kuwaka moto. Unaweza kujizaba vibao na kujimaindi, afu utajiuliza, “Nilikua wapi siku, zote hizi?”

    Ukitoka kule jisogeze mdogo mdogo hadi Kariakoo, Dsm kisha kutana na wafanyabiashara wa maduka pale ambao wana gepu la kufuata bidhaa kule China, Uingereza na Dubai. Utapigwa na butwaa utakapoona watu wakiongelea milioni mia tatu, milioni mia saba, bilioni mbili kama vile wanaongelea elfu kumi kumi.
    Usipokua na utulivu unaweza kuamini kwamba biashara zinazolipa ni maduka na unaweza kuanza kufight kupata fremu pale!Usiende kwanza Zanzibar, bali chukua hata bus au Fastjet uende chapchap kule Arusha. Hapo kutana na stori za mabilionea wa madini wanaotikisa jiji.


    Ukisimuliwa ABC za madini na namna ya kucheza nayo, unaweza kuacha kila kitu na kuanza kuhangaika na biashara ya madini. Hapo sijakutajia jeuri utakayoiona kwa watu wanaofanya biashara ya utalii. Nakwambia hela ulizozisikia Kariakoo utaziona ni cha mtoto sana!

    Unapoendelea kutafakari, rudi mtandaoni. Kama ukibahatika kukutana na watu wanaoitwa Network Marketing utakoma kuchagua. Wakikuelezea stori zao, wakikusimulia walivyonunua mavouge yao, wakikuonesha picha zao walizokua wanakula bata Dubai, Paris, Madagascar na Uamerikani, nakwambia korosho utaziona takataka.Mbao utazihesabu kama biashara ya utumwa, maduka ya Kariakoo utayaona kama michosho na mipunga ya Ifakara utaiona kama madudu flani ya walugaluga waliochelewa! Sasa mara kumi hata ya Network Marketing wa bidhaa, usiombe ukutane na fursa ya digital currency, hakika nakwambia utatembea kifua mbele ukiamini kutajirika ni ishu ya kufumba na kufumbua.

    Hapo sijaamua kusafiri na wewe kwenda kwa wale tunaokinadi kilimo kama dhahabu inayoelea. Ukisikiliza wafuasi wa kilimo, ukasikiliza hesabu wanazokupatia unaweza kusema wanaohangaika na madini wanapoteza muda!

    Ngoja niuchune kukupeleka kwenye fursa ya samaki kuzitoa Mwanza kupeleka Congo, ngoja nisikurushe roho na habari ya korosho, ngoja nikaushie habari ya ufuta!


    KUNA MAMBO MATANO YA KUFAHAMU:-*1. Usipokua na utulivu wa fikra, hizi habari za fursa za biashara na ujasiriamali zinaweza kugeuka kuwa kama miluzi mingi, na itakupoteza.

    2. Mtu yeyote asikudanganye ya kwamba kuna biashara bora kuliko nyingine. Kila biashara, fursa unayoiona huku duniani inao uwezo wa kutengeneza matajiri.

    Kuna matajiri kutokana na kumiliki shule, wengine kwa kumiliki mabasi, wengine kwa kuwa na vituo vya mafuta, wengine kwa kilimo, wengine kwa udalali n.k.

    Usisahau kuwa biashara inayomtajirisha mmoja, mwingine akiingia ndio inaweza kumfilisi na kumpoteza kabisa! Kawaulize waliolizwa kwenye kilimo, watakusimulia.

    3. Mtu yeyote asikuchanganye na miluzi yake hata ukaamini kwamba kuna fursa inayoweza kumfaa kila mtu. Sio kila fursa inayompa faida John inaweza kukupa faida wewe Ashura.

    Ukifuatilia kwa umakini utabaini kwamba mafanikio hayakai katika uzuri wa fursa, bali yanatokana na mchukua fursa.

    Mwingine anaweza kujifunza na kumudu kuifanya network marketing, lakini mwingine nature ya network marketing haimfai, isipokua akienda kule Mafinga akazamia kwenye mbao, mwaka mmoja mbali unaona ana Semitrela zake mbili na mambo yanaenda.

    Kuna watu wanapotea kiuchumi kwa kung’ang’ana na fursa kwa kukariri. Kisa kuna mtu alinunua Range Rover katika network marketing na wewe unaendelea kukomaa, mwaka wa tano sasa hata bodaboda huna,

    kumbe ungeenda zako Mbozi kwenye Kahawa sasa hivi usikute na nyumba ungekua umejenga.

    Kisa wanaoenda China wanatoka na wewe unahangaika na biashara za maduka, mwaka wa ishirini bado hakujasomeka na kumbe ungeenda zako kwenye madini huko Mererani muda huu ungekua umeshanunua helkopta yako!

    4. Ni kweli kwamba inatakiwa tujifunze fursa mbalimbali, lakini ifike sehemu mtu uchague kukomaa na fursa fulani pasipo kurukaruka.

    Utajiri hauji kwa mtu kuwa bize na kila fursa inayoingia, bali unakuja kwa kujifunza fursa nyingi na ku-stick na eneo moja, ama maeneo machache ambayo, utajitambulisha nayo na watu watakutambua.

    Na ukishakua katika kukomaa na maeneo yako (fursa ulizoamua kukomaa nazo), usianze tena kuyumbayumba na kutamani ya wengine.5. Lazima ifike mahali utambue kwamba kila mtu anahitaji fedha za kutosha lakini hatuhitaji kiwango sawa cha fedha kwa sababu makusudi na malengo yetu hayafanani.

    Nikisema hivi, sikushauri uhangaike na fursa kwa motive ya hela pekee, bali ufanye vitu kama sehemu ya kuufurahia mchakato wa kazi, na fedha ziwe ni matokeo na sio lengo namba moja

    Fursa zipo nyingi kuwa makini katika maamuzi.Wewe umejifunza nini kutokana na ujumbe huu.
    Ebu weka maoni yako hapa chini

  • Tegemea hiki endapo utasoma kitabu Cha Godius Rweyongeza

    Ni kitabu kipi Cha Godius Rweyongeza umewahi kusoma?  Kama hujawahi kusoma kitabu chake chochote Basi huu unaweza kuwa Ni wakati wako muafaka wa kuhakikisha kuwa unasoma kitabu chake hata kimoja.

    Kitu kikubwa unachopaswa kutegemea kutoka kwenye vitabu vyake ni kuwa  kitabu chake chochote utakachosoma utapata  thamani zaidi ya vile ulivyolipia.

    Ukinunua kitabu Cha elfu tano, Basi ujue ulipaswa kulipia elfu kumi au zaidi. Kitabu unachostahili kulipia elfu hamsini unakipata kwa elfu ishirini au chini ya hapo.

    Unaweza kudhani nakudanganya. Ebu msikilize huyu hapa

    Au huyu

    Bado huamini tu, ebu muone na huyu

    Zaidi zaidi, pata nakala ya kitabu na wewe uvune makubwa yaliyo vitabuni mwake.

    Ni kitabu kipi ungependa kusoma Kati ya Hivi

    1. KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI
    2. JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO
    3. NGUVU YA VITU VIDOGO KUELEKEA MAFANIKIO MAKUBWA
    4. MAISHA NI FURSA: ZITUMIE ZIKUBEBE
    5. JINSI YA KUWEKA AKIBA
    6. JINSI YA KUWA MWANDISHI MBOBEVU
    7. MAAJABU YA KUWEKEZA KWENYE HISA, HATIFUNGANI NA VIPANDE
    8. KIPAJI NI DHAHABU: Jinsi Ya Kugundua, Kunoa Na Kuendeleza Kipaji Chako

    9. JINSI YA KUIBUA UBUNIFU ULIO NDANI YAKO


X